Dar es Salaam. Wadau wameeleza matarajio yao kwa Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo huku wakitaja mambo wanayotamani yapewe kipaumbele ili kuongeza tija kwenye sekta hiyo.
Tayari zimepita siku nane tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipotangaza baraza jipya la mawaziri ambalo Chongolo ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo akipokea kijiti kwa Hussein Bashe aliyewekwa kando.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wadau wamemshauri Chongolo kuyaendeleza mazuri ya mtangulizi wake na kutatua changamoto zilizopo.
Miongoni mwa mambo waliyotamani yaboreshwe ni upatikanaji wa masoko, kuboresha bei za mazao na kutoa elimu kwa wakulima juu ya teknolojia mpya za kilimo.
Wamesema kuna mengine hayakufanyika lakini yana tija wanayotamani Chongolo ayaendeleze yakiwamo mabwawa na mabonde ya umwagiliaji ili kuondokana na kutegemea mvua katika kilimo.
Pia, wametaka mkakati wa kupima udongo urejeshwe na kuboreshwa, kuimarishwa kwa vyama vya ushirika na gharama za pembejeo kuwa rafiki ili wakulima wote wazimudu.
Wadau hao wameshauri pia wakulima wapewe elimu ya usalama wa chakula, kuweka nguvu kwenye kilimo cha asili, kuongeza thamani ya mazao na vijana wajengewe uwezo na kuwekewa mazingira rafiki ya kushiriki katika kilimo.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadau wameonesha matarajio yao kwa Waziri Chongolo katika sekta hiyo, wakiamini kama atashughulikia changamoto kadhaa zilizopo, kutaongeza ufanisi katika sekta hiyo.
Mmoja wa wakulima wa tumbaku, ambaye pia ni mbunge wa Ushetu, Emmanuel Charahani amegusia maboresho ya masoko na bei katika mazao hususani ya kimkakati akisema kama yataboreshwa masoko, yataongeza tija.
Ametaja mazao hayo kuwa ni pamba, korosho, chai, tumbaku, kahawa na la mchikichi ambalo limeanzishwa kwa kasi mkoani Kigoma.
“Upatikanaji wa masoko uwe rahisi na bei za mazao hususani yale ya kimkakati iboreshwe, ili wakulima warudishe gharama za uzalishaji, hii italeta tija,” amesema Charahani.
Pia, amesema mkulima hapaswi kulima kama huduma, anapaswa kulima kama biashara, hivyo Serikali ione namna ya kuongeza masoko na kuboresha bei ili nao warudishe gharama za uzalishaji.
Charahani pia ameeleza umuhimu wa kupima ardhi ili kutambua udongo, mkakati anaosema ulianza lakini haukuwa endelevu na kushauri kwa Waziri Chongolo kuuendeleza kwa kuwa una tija kwa wakulima.
“Jiografia ya ardhi yetu imetofautiana, kuna maeneo yanahitaji mifuko minne ya mbolea, mengine mitano, vilevile yapo maeneo hayahitaji kutumia Urea yanahitaji na mengine hayahitaji hii yanahitaji ile.
“Kadri tutakavyoendelea kupima udongo, tutafahamu ni maeneo gani yanatumia mbolea gani na mengine yanafaa kwa mbolea gani, kwa kufanya hivi kutasaidia kuboresha kilimo chetu,” amesema Charahani.
Pia, ameshauri kuimarishwa kwa vyama vya ushirika na kuwa na mkakati wa kutotegemea mvua kwenye kilimo.
“Maeneo mengi tunahitaji kuwa na mabwawa na mabonde makubwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, bahati nzuri ili lilishaanzishwa, hivyo ni kuliendeleza.
“Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji zisomane, maji yakipatikana mengi hatutategemea mvua, kuwe na benki ya mabwawa, kila kanda kuwe na bwawa la kuvuna maji mvua, badala kutegemea mvua ndipo tulime, inapokata kilimo kiendelee.
“Kuna nchi hazitegemei mvua kulima, nasi tufike huko, tuweze kupata mazao bila kutegemea mvua, tukifanikiwa katika haya tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye kilimo,” amesema.
Mdau mwingine wa kilimo, Laurencia Mulalo kutoka Buchosa hakutofautiana na Charahani naye aligusia mkakati wa kupima udongo ambao amesema, ulitoa mwanga kwa wakulima lakini haukuendelezwa vizuri.
“Kama utaboreshwa na kufanyika kwa usahihi utakuwa na tija kwa kuwa, mkulima atafahamu udongo wa shamba lake unataka nini,” amesema.
“Pia, gharama za pembejeo ziwe rafiki kwa kila mkulima kuzimudu; hivi sasa gharama za pembejeo ni kubwa, hivyo kusababisha uendeshaji kuwa mgumu, wenye uwezo ndiyo wanamudu wale wakulima wadogo wanakwama, kama Waziri ataliangalia ili na kulegeza gharama wengi watazimudu na kutakuwa na tija,” amesema.
Hata hivyo, Mulalo ameonesha wasiwasi juu ya kuwa na mabwawa na mabonde kwa ajili ya kuhifadhi maji na kufanya kilimo cha umwagiliaji.
“Kutotegemea mvua katika kilimo, hili jambo limeshakuwa wimbo, lakini kama wakati huu litapewa mkazo tukawa na skimu nyingi za umwagiliaji, sekta ya kilimo ingepiga hatua.
“Kitendo cha kuwa na uhakika wa maji, maana yake kwa mwaka tungezalisha hadi mara tatu,” amesema Mulalo.
Pia, ameshauri elimu kwa wakulima itolewe mara kwa mara, akibainisha teknolojia zinabadilika, hivyo zinapokuja teknolojia mpya wakulima wafahamu kwa kupewa elimu.
“Vilevile ikitokea ikaingizwa mbegu mpya basi wakulima pia waeleze mapema, maana kuna wakulima wamekariri mbegu, isipokuwepo mbegu hii, kuna nyingine basi hawapandi, wakidai siyo mbegu yao na muda unapita,
“Ni vema mbegu zote ziwepo ili wakulima wenyewe wachague na ikitokea kuna mbegu mpya napo wakulima waeleze mapema,” amesema Mulalo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kilimo Halisi ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Meshack Lwenje yeye pia ameshauri kuwa na kilimo cha umwagiliaji.
“Duniani kote tunakabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kama nchi tukifanya kilimo umwagiliaji itatusaidia kutotegemea mvua.
“Vilevile waziri anafahamu mazingira yaliyopo, vijana wengi hawana ajira, solution (jibu) pekee ni kujiajiri kwenye kilimo, hivyo kama nchi iweke mazingira rafiki huko kwa kuwajengea uwezo,” amesema Lwenje.
Amesema bado kuna changamoto pia ya kufikia malengo ya matakwa ya soko, akitolea mfano mteja anapohitaji tani sita za bidhaa fulani na kuitaka kila Ijumaa, aliyepata soko hilo anaweza kupeleka wiki ya kwanza, wiki nyingine zinazofuata ikawa changamoto.
“Kuna changamoto nyingi katika masoko, Serikali ingekutana na wakulima na kuzifahamu, lakini kwa vijana pia, wajengewe uwezo waingie kwenye kilimo, lakini ili nao wakipende, lazima nacho kipendeke kwa kuwa na mazingira rafiki,” amesema.
Lwenje pia ameshauri kuwekeza nguvu kwenye matumizi ya kilimo cha asili na kuondokana na mbegu za kisasa.
“Kwenye mbegu za kisasa sawa utapata mazao mengi, lakini tuweke nguvu kwenye kilimo cha asili, tuvae uhalisia wetu, ni sawa tunatafuta pesa kwenye kilimo lakini bila afya huwezi kuitumia hiyo pesa,” amesema.
Amesema pia kuwe na elimu za mara kwa mara kwa wakulima juu ya usalama wa chakula na kufundishwa namna ya kuyaongezea thamani mazao yao.
Chongolo amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uongozi wa Awamu ya Tano.
Pi, amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
