Mv Liemba kurudi kivingine, Ziwa Tanganyika

Kigoma. Ukarabati wa meli kongwe ya MV Liemba, ambayo ilisitisha safari zake mwaka 2018 kutokana na uchakavu wa mitambo, umefikia asilimia 42.

Kazi za ukarabati huo, unaogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 13 (zaidi ya Sh32 bilioni), zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24.

Akizungumza leo, Jumatatu, Novemba 24, 2025, Kaimu Meneja wa Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) tawi la Kigoma, Humphrey Mwambungu amesema ukarabati huo ulianza Julai 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026.

Mwambungu amesema mkandarasi ameshafanya maagizo ya vifaa muhimu vitakavyofungwa kwenye meli hiyo, ikiwemo injini mbili mpya na majenereta ya umeme.

Aidha, meli hiyo tayari imepandishwa chelezoni kwa ajili ya shughuli za kusafisha na kupaka rangi sehemu ya chini ya umbo lake.

 “Tayari injini za meli hii zimeshakamilika kutengenezwa nchini Marekani na zinatarajiwa kuwasili nchini ndani ya mwezi ujao, hadi sasa mkandarasi ameshalipwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 7 na mradi umefikia asilimia 42 ya utekelezaji wake,” amesema Mwambungu.

Naye Mhandisi wa Ubora na Usalama, David Matala, amesema kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na ukarabati wa umbo la meli, kubadilisha vipuri vilivyoharibika na kuweka mabomba mapya, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 90.

Ameeleza kuwa hatua inayofuata ni kufunga mfumo wa umeme kwenye meli hiyo, kusakinisha injini mpya pamoja na mashine nyingine zinazoiwezesha kufanya kazi.

Matala amewahakikishia wananchi kuwa meli hiyo itakuwa na ubora zaidi kwani maboresho yanayofanyika ni makubwa na ya kisasa.

 “Meli ikikamilika abiria wataweza kusafiri wakiwa huru na salama kutokana na maboresho yaliyofanyika ya kisasa ambayo itaondoa kero kwa wananchi waliokuwa wakikabiliana nazo hapo awali,”amesema Mhandisi Matala

MV Liemba meli iliyotumika vita vya kwanza vya dunia ina zaidi ya miaka 100 ambapo ilitengenezwa mwaka 1913 nchini Ujerumani na ikapewa jina la Graf von Goetzen, likiwa ni jina la gavana wa jimbo moja nchini humo.

Baada ya kutengenezwa ilifunguliwa vipandevipande na kisha kupakiwa kwenye maboksi 5,000 na kusafirishwa kwa meli mpaka Dar es Salaam kisha kusafirishwa mpaka Tabora na kubebwa na watumwa mpaka Kigoma.

Baada ya kufika Kigoma ikaingizwa kwenye chelezo na mnamo mwaka 1915 ikaanza kazi rasmi ikiwa na mizinga miwili mbele na nyuma.

Pia, ilikuwa inatumika kusafirisha wanajeshi wa Ujerumani kuwapeleka katika bandari tofautitofauti kwa ajili ya kupigana vita ikiwa ni pamoja na Bandari ya Kassanga na Mbala iliyopo nchini Zambia.

Mwaka 1957 ilibadilishwa jina na kuitwa Liemba, neno linalotoka kwenye jamii ya Kifipa likiwa na maana ya Maji.

Mwaka 1961 ilikabidhiwa kwa Serikali ya Tanganyika na ikafanyiwa marekebisho yaliyojumuisha kubadilisha mfumo wa injini wa awali uliokuwa unatumia mvuke na kuweka mfumo wa Injini unaotumia dizeli.