Mvua wilayani Sumbawanga zakata mawasiliano ya vijiji

Rukwa. Mvua zinazoendelea   katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Sumbawanga zimesababisha kusombwa kwa daraja linalounganisha vijiji vitano vya Ilemba A, Ilemba B, Lyanza, Sakalilo na Kasteka, na kusababisha adha ya usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo.

Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Sakalilo, Kata ya Ilemba, Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa wamesema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri na usafirishaji baada ya daraja la Sakalilo kusombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea.

Mmoja wa wakazi hao, Andrea Siame, amesema kuharibika kwa daraja hilo kumesababisha wananchi kushindwa kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji na pia kushindwa kuvuka kwenda katika maeneo jirani.

Ameeleza kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kati ya vijiji vya Ilemba A, Ilemba B, Lyanza, Sakalilo na Kasteka, na kusombwa kwake kumeathiri mawasiliano kati ya kata za Ilemba, Muze na Mtowisa.

Siame amesema kuwa kila msimu wa masika daraja hilo huwa halipitiki, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri na wafanyabiashara wanaohitaji kusafirisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo mazao.

Andrea Siame kutoka katika kijiji cha sakalilo akizungumza adha wanayokutana nayo baada ya daraja la sakalilo kusombwa na maji ya mvua

Ameongeza kuwa wakati mwingine wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka Zahanati ya Ilemba kwenda Kituo cha Afya Muze hujikuta wakipata shida kufika kwa wakati, jambo linaloweza kuhatarisha maisha yao.

 “Mvua hizi zimekuwa kikwazo kikubwa hasa pale barabara zinapokatika wananchi hukosa huduma muhimu za kijamii na kiuchumi,” amesema Siame

Amezitaja athari wanazokutana nazo ni pamoja na mvua zinaponyesha nyakati za usiku hulazimika kutoka nje kwa kuwa maji hujaa ndani na wakati mwingine mifugo na vyombo vya ndani  husombwa na maji.

“ Mvua zikianza kunyesha usiku tunalazimika kutoka nje kuokoa maisha yetu kwa kuwa maji hujaa ndani na kukuta vyombo na mifugo yetu Ziwa Rukwa, tunaiomba Serikali iharakishe kuja kutengeneza daraja hili na miundombinu ya barabara ili kuendelea kupata huduma za kijamii,” amesema.

Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile akizungumza mara baada ya kufika kwenye daraja lililosombwa na maji

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Chirukile ameliomba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuweka kambi katika daraja hilo kwa lengo la kuokoa maisha ya watu na kuweka zuio la wananchi kutopita katika eneo hilo nyakati za jioni.

Chirukile amesema mwanzoni waliweka vizingiti vya miti ili kuwasaidia wananchi kupita kwa urahisi, lakini hata vizuizi hivyo vimesombwa na maji.

DC Chirukile amesema kuwa eneo hilo liliathirika na mvua za mwaka 2023/2024, pamoja na hizi za mwaka 2025 ambazo zimeanza kunyesha, na hivyo kulitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuweka kambi katika daraja hilo ili kuimarisha shughuli za uokoaji.

Aidha, ameliomba jeshi hilo kutoa elimu kwa wananchi kuacha tabia ya kuogelea katika eneo hilo, hususan watoto, kutokana na kasi kubwa ya maji ambayo inaweza kuhatarisha maisha yao.

Akielezea athari za mvua hizo, Chirukile amesema kuwa zaidi ya nyumba 38 zimebomoka katika kata za Mpui na Ikozi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, hali iliyowaacha wakazi wake bila makazi na kulazimika kuhifadhiwa kwa ndugu na jamaa.

Amesema watu watatu walijeruhiwa katika tukio hilo, walipewa matibabu na wanaendelea na shughuli zao.

Hata hivyo, kamati ya maafa ya wilaya hiyo imefanya ziara katika maeneo yote yaliyoathirika na mvua kali zilizoambatana na upepo mkali.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwalimu Misana Kwangura, amesema kuwa tathmini ya maafa hayo inaendelea na ripoti kamili itawasilishwa katika ngazi ya wilaya kwa ajili ya hatua zaidi.

“Tahadhali ya usalama tumeitoa kwa wananchi kwenye maeneo yenye athari za umeme hadi mamlaka husika zitakapotoa msaada,” amesema Kwangura.