Dar es Salaam. Katika kipindi cha miaka minne, Tanzania imeendelea kushuhudia mfululizo wa matukio ya ukatili wa kijinsia, huku ubakaji ukibaki kuwa moja ya uhalifu unaotikisa jamii za aina zote.
Takwimu zinaonesha matukio ya ubakaji kwa mwaka 2021 yalikuwa 6,305 idadi iliyoongezeka hadi kufikia 8,541 mwaka 2024.
Kwa mujibu wa wadau, ongezeko hilo halipaswi kutazamwa kama mabadiliko ya takwimu kwenye karatasi tu, kwa kuwa linabeba uzito wa mioyo iliyovunjika, ndoto zilizopotea na jamii inayokabiliwa na majeraha ya ndani yanayozidi kutanuka.
Kwa kuwa, kila tukio la ubakaji linaacha alama isiyofutika si kwa waathiriwa pekee, bali pia kwa familia zao, majirani na hata vizazi vijavyo vinavyorithi athari za kimwili, kihisia na kisaikolojia.
Wakati mwingine, simulizi hizi hubaki kimya kutokana na aibu, hofu ya unyanyapaa au ukosefu wa imani katika mifumo ya kisheria na ulinzi.
Hata hivyo, ongezeko la matukio yanayoripotiwa linaibua maswali mazito kuhusu usalama wa watoto, wavulana, wanaume na wanawake, mienendo ya kijamii na uwezo wa mifumo ya ulinzi na haki ya kukabiliana na hali hiyo.
Ripoti hiyo ya Statistical Abstract ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu 2024 (NBS) inaonesha kuwa, kabla ya matukio kufika yale yaliyokuwapo 2024 yaliongezeka kila mwaka kutoka 6,827 mwaka 2022 hadi 8,691 mwaka 2023 kabla ya kupungua kidogo kufikia yale yaliyorekodiwa 2024 (8,541).
Akizungumzia suala hilo leo, Jumatatu Novemba 24, 2025, Wakili Dominick Ndunguru amesema wakati mwingine ongezeko la matukio yanayoripotiwa linaakisi ukuaji wa uelewa wa watu na kuachwa kukalia kimya tatizo linapotokea.
Hiyo ni baada ya kufanyika kwa jitihada mbalimbali, Serikali kwa kushirikiana na mashirika binafsi wameunganisha nguvu kuhakikisha wanapambana na matukio hayo huku wakitangaza namba ambazo wananchi wanaweza kutoa taarifa pindi tukio lolote la ukatili ikiwamo ubakaji linapotokea.
“Hii imepanua wigo wa utoaji taarifa, awali hata utoaji wa taarifa ulikuwa mgumu. Watu wamekuwa na uelewa wa kupaza sauti na wanaona kukaa kimya ni kama kuhalalisha matukio hayo kuendelea kutokea, hivyo wanataka hatua zichukuliwe,” amesema.
Jambo hilo limeongeza msukumo sana japokuwa linaakisi pia kuwapo kwa ongezeko la matukio ya ubakaji katika jamii hali ambayo huenda inachochewa na matumizi ya mitandao ya kijamii, kwa sasa vijana wengi wanamiliki simu za mkononi.
Kupitia simu hizo watu hususani watoto wanakuwa na uwezo wa kuona picha tofauti ambazo wakati mwingine wanalazimika kujaribu.
“Lakini mwisho wa siku kuna haja ya kufanyika tafiti ili kuhakikisha tunajua sababu ya kuongezeka kwa matukio haya ili tuweze kushughulika na kiini cha tatizo husika,” amesema.
Mwanasaikolojia, Charles Kalungu amesema zipo sababu nyingi zinazochangia kuongezeka kwa matuko haya ikiwamo ya kisaikolojia, kimazingira na kukua kwa utandawazi.
“Watu wamepoteza maadili mema na utandawazi umeleta vishawishi vingi sana na hata wanawake siku hizi wanashindwa kujisitiri vizuri jambo ambalo linaleta vishawishi kwa wanaume,” amesema Kalungu.
Pia, kukosekana kwa uwazi wa sheria inayotumika katika kuadhibu watu imetajwa kuwa moja ya sababu kwa kuwa, adhabu za watu waliobaka kutotangazwa hadharani kwa kiwango cha matukio yalivyo kumefanya watu kutoogopa na kuendelea kudhani hata wakifanya hawataathiriwa.
“Kukosekana kwa uwazi wa adhabu umefanya matukio haya kuendelea kufanyika, kwani watu wanaona hakuna aliyechukuliwa hatua alipobaka,” amesema Kalungu.
Katika hilo, Said Said ambaye ni mzazi na mkazi wa Mbezi amesema ni vyema familia zikawa shule ya kwanza kuhakikisha watoto wanaishi katika maadili yao na kuwaondolea uhuru wanaopewa ili wawe salama.
“Turudi katika enzi ambazo wazazi wetu walitukuza, mzazi akikuambia mwisho kwangu kurudi ni saa 12 kamili jioni hakuna anayekuwa nje wakati huo na wote tunafuata. Tuache kuwalea watoto kisasa na kuwapa uhuru wa kufanya kila kitu kwa kusingizia utandawazi,” amesema.
Amesema suala hilo mara nyingi limewaacha wazazi na majuto na kubaki kusema ningejua wakati ambao tayari watoto wameshafanyiwa ukatili wa kijinsia.
“Haya yakitokea mnaanza kutafuta wa kumlaumu lakini ukimuuliza mzazi anayelia mara yake ya mwisho kuzungumza na mwanaye ni lini hakumbuki, mzazi anaweza kukaa wiki hajaonana na mwanaye na haoni tabu, wanalala nyumba moja na kuamka nyumba moja kila mtu yuko na harakati zake,” amesema.
Akizungumzia namna ya kumsaidia aliyekutwa na tatizo hilo, mwanasaikolojia Kalungu amesema mara nyingi tukio kama hili linaweza kuacha alama mbaya katika maisha ya binti au mwanamke na hufanyika katika mazingira anayoishi.
Amesema ili kumsaidia mtu aliyepitia hali hiyo ni vyema kumpa nafasi ya kujisamehe hususan kwa wale waliopata tatizo katika mazingira ambayo ni ngumu kuyazuia.
“Pia, binti kama huyu apate mtu wa kumuelewa, tukio kama hili hakuna anayependa litokee katika maisha yake, wengi katika jamii huwa ni ngumu kuwaelewa, hivyo jamii ni lazima iwaelewe na kuacha kuwalalamikia bali kuwasaidia,” amesema Kalungu.
Kujumuika na jamii ambayo wamewahi kukumbwa na hali hiyo ni moja ya jambo linaloweza kuwasaidia waathiriwa kurudi katika hali zao za kawaida, linaweza kuwafanya wapate tumaini jipya na kurudi katika hali yao ya kawaida ikiwamo kufurahia maisha yao ya kila siku.
“Pia, ni vyema kuweka wazi, wengine huwa wanashindwa kuzungumza. Uponyaji unaanza kwa yeye kuzungumza, akikaa kimya ni ngumu kuweza kusaidika. Baadhi wanashindwa kusema kwa sababu ya vitisho walivyopewa na wabakaji, lakini ukimya hausaidii chochote na matokeo yake baadhi wanaishia pabaya,” amesema Kalungu.
“Usaidizi wa kiroho pia ni jambo linaloweza kuwafanya wapate tumaini jipya, kwani ubakaji wakati mwingine huja na matokeo hasi ikiwamo magonjwa au kupata ujauzito.
“Msaada wa kisheria nalo ni jambo linaloweza kusaidia,” amesema Kalungu.
