BEKI wa kushoto wa Coastal Union, Ally Ramadhan ‘Oviedo’ amefichua sababu ya kupenda kusaini mkataba wa mwaka mmoja kila timu anayopita ikiwamo ishu za ofa.
Oviedo aliyejiunga na Coastal msimu huu akitokea Pamba Jiji aliwahi pia kuzitumikia Mashujaa, Ihefu na Pamba Jiji ambako kote alicheza msimu mmoja, huku KMC akitumikia misimu saba tangu ikiwa Ligi Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza , FDL) hadi ilipopanda 2018.
Akizungumza na Mwanaspoti, Oviedo amesema sababu ya kubwa anapomaliza mkataba ni kama viongozi wanamchunia hawarudi kuzungumza kuhusu mkataba mpya hivyo anapopata ofa timu nyingine hutimka.
Aliongeza, sababu nyingine timu nyingi alizocheza hushindwa kuendelea nao kutokana na ofa ndogo wanayompatia tofauti na matarajio yake.
“Uongozi unakupigia simu hatutaendelea na wewe au wanakufuata tunataka kukuongezea mkataba mwingine ofa yako vipi, nasema kiasi changu tunashindwana hapo hawarudi tena na mimi naangalia timu nyingine iliyoleta ofa ninayoitaka, nasaini mkataba,” amesema Oviedo.
“KMC tu ndio nilicheza muda mrefu kwa sababu walikuwa wananipa ofa niliyoitaka na tangu hapo sijawahi kudumu misimu miwili kwenye timu nyingine.”
Nyota huyo wa zamani wa Mashujaa alisajiliwa Coastal kama mbadala sahihi wa Miraji Abdallah ‘Zambo Jr’ aliyejiunga na Dodoma Jiji.
Akizungumzia nafasi yake kwenye kikosi cha kocha Mohamed Muya amesema; “Ligi imekuwa ngumu kwahiyo kocha anaangalia yupi anaanza naye kwenye mechi husika.”