Vikundi 82 vyanufaika mkopo wa Sh789 milioni Chunya

Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imetoa mkopo wa zaidi ya Sh789.5 milioni kwa vikundi 82 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Mikopo hiyo imetolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali linaloelekeza halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya kuwezesha makundi hayo kiuchumi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Novemba 24, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga, amesema mikopo hiyo ilitolewa Novemba 21, 2025, ikiwa na lengo la kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuanzisha au kuendeleza shughuli za kujiajiri na kukuza uchumi wao.

“Mpango wa Serikali ni kuhakikisha vijana wanakuwa na shughuli za kiuchumi  za kuwaingizia kipato na kuajiri wengine,” amesema.

Batenga ameonya wanufaika wa mkopo huo kutumia kwa malengo yaliyo kusudiwa na kurejesha kwa wakati ili wengine wanufaike.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Mbaraka Batenga akizungumza na wanufaika wa mkopo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo

“Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kuhakikisha  makundi ya  vijana yananufaika na mapato ya ndani ya halmashauri  ili kuondokana na  utegemezi hususani kundi la watu wenye ulemavu, ambapo kati ya vikundi 82, vitatu vya walemavu,” amesema.

Katika hatua nyingine Batenga amesema  ni wakati sasa jamii kuchangamkia fursa za kiuchumi kupitia mikopo asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamim Kambona amesema wataendelea kutenga mapato ya ndani kwa ajili ya utoaji wa mikopo lengo ni kuona kundi la vijana, wanawake na walemavu kuinuka kiuchumi.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Chunya,  Tamim Kambona akizungumza na wanufaika wa mikopo asilimia 10 ya wanawake,vijana na walemavu.

Amesema mbali na utoaji wa mikopo halmashauri imetenga maeneo na kufanyia utafiti wa madini na kutoa vibali 11, kwa lengo la kuwezesha vijana kujiajiri.

“Kuna maeneo tunaenda kufanyia utafiti wa kina kama kuna madini ya dhahabu ili kuwezesha vijana kufanya shughuli za uchimbaji  na kujikwamua kiuchumi.

“Kuna vijana ambao hawana ajira wamekuwa wakifanya vibarua kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo na wakubwa hao ndio tutakao wagusa maeneo yalifanyiwa tafiti, na  tutatoa vibali na kuwapa mikopo ili waweze kujiajiri kupitia shughuli za uchimbaji wa madini,” amesema.

Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo,  Neema Jeremia ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kutoa mikopo kwa makundi ya vijana na kwamba utawasaidia kuondokana na wimbi la umaskini .