Wakili aliyekuwa akiwatetea wenye kesi za maandamano Mwanza afariki

Mwanza. Wakili aliyekuwa akiwatetea watuhumiwa wa kesi za maandamano katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Beatus Linda amefariki dunia siku chache baada ya kutoka kusimamia mojawapo ya kesi hizo.

Linda amefariki usiku wa kuamkia Jumapili Novemba 23, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Agha Khan iliyopo jijini Mwanza.

Wakili huyo ni miongoni mwa mawakili 37 wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) chapta ya Mwanza waliojitolea kutoa huduma ya msaada wa kisheria na kuwatetea watuhumiwa wote wa kesi zilizotokana na maandamano baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, mkoani Mwanza.

Mara ya mwisho Wakili huyo ameonekana Novemba 19, 2025 alipowakilisha upande wa utetezi katika kesi ya watuhumiwa 93 waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana.

Ambapo, Linda alisaidiana na Wakili mwenzake, Duttu Chebwa, huku shauri hilo likiahirishwa, kisha akafanya mahojiano na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa shauri hilo.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Mawakili Mkoa wa Mwanza, Joseph Mugabe amethibitisha taarifa za kifo cha Beatus Linda, huku akisisitiza kuwa wanasubiria ripoti ya uchunguzi wa polisi na madaktari (postmortem ) ili kujua kiundani sababu za kifo hicho.

“Hatujajua bado chanzo ni nini ila jana asubuhi (Jumapili) tumeamka ndio tukaambiwa amefariki, tulifika pia nyumbani kwao ambapo ndugu zake walituambia kuwa Ijumaa ndio alianza kuugua,” amesema Mugabe.

Ameongeza; “Analalamika miguu na tumbo vinauma na kufikia Jumamosi hali ikawa mbaya akapelekwa Aga Khan hospitali na usiku wa kuamkia Jumapili akawa amefariki.” 

Mugabe amesema kuwa taratibu za mazishi upande wa familia zinaendelea na inatarajiwa ifikapo Jumatano wiki hii zitakuwa zimekamilika ambapo marehemu atazikwa nyumbani kwao mtaa wa Nyamongolo jijini Mwanza.