Wananchi Dar, Pwani walia uhaba wa maji Serikali yafafanua

Dar es Salaam. Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na Pwani wamedai kukabiliwa na adha kubwa ya upatikanaji wa maji, wakikosa huduma kwa zaidi ya wiki mbili.

Hali hiyo imewalazimu wakazi wengi kutumia muda mwingi kutafuta maji, huku gharama zikipanda maradufu na kuongeza mzigo katika maisha yao ya kila siku, wengine wakihofu kupata magonjwa ya mlipuko.

Katika maeneo ya Kibaha (Pwani) na Msasani, Kinondoni na baadhi ya maeneo ya Tabata na Goba jijini Dar es Salaam, wakazi wanasema maji yamekuwa yakitoka kwa nadra au kutotoka kabisa, hali inayowalazimu kununua maji ya madumu kwa bei kubwa ambayo imepanda ghafla kutokana na uhaba uliopo.

“Wiki ya pili sasa hatujapata maji, tuliambiwa huwa yanatoka saa 8 usiku, tumeamka wiki nzima muda huo ili kuona kama tutapata maji lakini napo hayatoki,” amesema Odiria Lutumo wa Kibaha kwa Mfipa.

Mkazi wa Kinondoni Biafra, Neema Mussa amesema kila wanapofikiria watapata wapi maji ya kupikia na kuoga, wanakata tamaa na kuichukia nyumba yao.

“Tunapika kwa kupima maji, kuoga imefikia hatua tunaona si lazima tena, kwangu tulikuwa tunaoga asubuhi na jioni lakini sasa ni mara moja tena kwa maji kidogo sana ili kupunguza matumizi, achilia mbali hata kufua tumeshindwa, maisha bila maji yamekuwa ya mateso,” amesema.

Wahofia magonjwa ya mlipuko

Wananchi katika maeneo hayo wamedai uhaba huo  umeathiri karibu kila jambo, wengine wakihofia kupata magonjwa ya mlipuko.

“Kuanzia upishi, usafi, hadi shughuli nyingine nyingi za kila siku zinategemea maji, imefikia hatua tunawalazimisha watoto kujisaidia porini, maana choo cha kuflashi ndani utanunua maji madumu mangapi kila siku ili yatoshe?,” anahoji Abia Adonias wa Kibaha kwa Mathias.

Huku akionyesha hofu ya kupata magonjwa ya mlipuko, Abia amesema siku ya nne leo  (jana) watoto wake wakitaka kujisaidia wanachukua jembe wanachimba shimo shambani nje ya nyumba wanamaliza haja zao huko wanafukia ili kupunguza matumizi ya maji vyooni, ambayo  gharama za maji ya madumu ni kubwa.

Nashoni Jumbura wa Goba amedai wanaingia gharama zisizo kwenye bajeti za kununua maji ya madumu kwa Sh2,000, wakati walistahili huduma hiyo.

“Hatuna maji wiki ya pili, mwanzoni tulikuwa tunadunduliza yaliyokuwepo ndani tukitarajia yatatoka lakini tangu Jumamosi ya Novemba 8 yalipokatika hadi leo hayajatoka, tunanunua ya madumu kwa ajili ya kupikia na kunywa ili kupunguza gharama,” amesema.

Baadhi ya familia katika maeneo ya Dar es Salaam zimedai  kutumia maji ya visima, ambavyo vingi katika maeneo hayo ni vya maji yenye chumvi.

Kwa Kibaha, maji ya chemchem yamegeuka ‘lulu’ familia zisizomudu kununua kwenye madumu zinapanga foleni kusubiri kuchota maji hayo katika baadhi ya maeneo hususani ya Kibaha Galagaza na Kumba ambako nako kutokana na wingi wa mahitaji chemchem zinakauka.

Kutokana na uhaba huo wa maji kwenye maeneo hayo, wauzaji wa maji ya madumu nao wameongeza bei kwa kiwango kisichokuwa cha kawaida.

Inaelezwa kwenye maeneo mengi dumu la maji la lita 20 ambalo awali lilikuwa likiuzwa Sh5,00 hadi 1,000, sasa linauzwa kati ya Sh1,500 hadi 2,000.

Mmoja wa wauzaji wa maji ya madumu, Rashid Juma amesema licha ya upatikanaji wa maji kuwa mgumu, hata wanakoyanunua nao wanauziwa kwa bei kubwa ndiyo sababu nao wanauza hadi Sh2,000 ili wapate faida.

“Mwanzoni tulikuwa tunauziwa dumu Sh100, sisi tuliuza Sh500 hadi 1,000 lakini sasa tunauziwa Sh150 hadi Sh200, ili tupate faida lazima tuuze Sh1,500 hadi 2,000 kwa dumu,” amesema muuzaji huyo anayefanya shughuli zake Kibaha.

Mmoja wa wanaouza maji kwa ndoo katika mitaa baadhi inayopata huduma ya maji aliyekataa kuandikwa jina amesema hivi sasa wanauza ndoo kwa Sh150 ili nao kufidia usingizi wao.

“Hatulali tunakesha kuuza maji kuanzia usiku wa manane hadi saa 10 alfajiri yanakatika hivyo tunafidia usingizi wetu,” amesema

Muuzaji mwingine, Nelson Elisha wa Kinondoni amesema kutokana na uhaba wa maji wanalazimika kutembea umbali mrefu ili kuchota maji kwenye maeneo machache yanakotoka.

“Tunatumia nguvu na muda mwingi kuyapata, wakati mwingine mwenye bomba anaamua tu kupandisha bei, kwa kuwa una shida utanunua tu, hivyo ili na sisi tupate faida hatuna budi kuongeza bei na kama hayatatoka hivi karibuni si ajabu tukauza hadi Sh2,500 kwa dumu,” amesema.

Akifafanua hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema wao wanatoza gharama kwa mteja kulingana na bei iliyopo kisheria kwa uniti.

“Mtu akiuza maji mtaani au kupandisha bei atakavyo, hiyo haipo kwetu ipo Ewura (Mamlaka ya udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji), sisi (Wizara) tunatoza bei ya uniti iliyopo kisheria,” amesema.

Kuhusu uhaba wa maji Dar es Salaam na Pwani, Mwajuma amesema kwa wiki mbili ambazo baadhi ya wananchi wanadai kutopata huduma, hakuna taarifa ya kuwepo kwa changamoto kwenye mitambo, hivyo huenda kuna changamoto kwa mteja mmoja mmoja au vinginevyo.

“Dawasa (Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam Dawasa)), inaweza kulizungumzia kwa ufasaha hilo,” amesema.

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro alipoulizwa na Mwananchi juu ya uhaba huo wa maji katika baadhi ya maeneo ya Pwani na Dar es Salaam amesema, kwenye uzalishaji hakuna changamoto ya maji.

“Mpaka sasa hatuna changamoto kwenye uzalishaji wa maji, kwa siku na hata inapotokea tumepata hitilafu katika mitambo na kunahitajika matengenezo tunatoa taarifa mapema,” amesema.

Amesema ikitokea kuna hitilafu huduma ya maji inaweza kukosekana kwa siku moja na si zaidi ya siku tatu.

“Maji kutotoka kwa zaidi ya siku tatu hadi tano hiyo ni changamoto, kama nilivyokwishasema hatuna changamoto kwenye uzalishaji wa maji kwa siku, kwenye hayo maeneo ambayo wanasema zaidi ya wiki hawana maji, wacha nifuatilie ili kujua tatizo ni nini,” amesema.