Kishapu. Mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Mwajipugila, wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, uliodumu kwa zaidi ya miaka saba umechukua sura mpya baada ya ndugu wa ukoo mmoja kumjeruhi mwingine mkono wakizozana kuhusu umiliki wa ekari sita za urithi.
Akizungumza leo, Novemba 25, 2025, katika kikao cha usuluhishi kilichofanyika wilayani Kishapu, kikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Peter Masindi, pia kimehudhuriwa na mtendaji wa kijiji hicho, John Paulo.
Mgogoro huo uliwahi kutatuliwa na wazee wa ukoo, lakini hawakufanikiwa kuumaliza.
“Wanaukoo walijaribu kumaliza mgogoro huu kwa kugawa ardhi hiyo kwa wajukuu wa familia husika, lakini mvutano umeibuka upya na ndugu John Sawe kumjeruhi nduguye Holo Wales, licha ya makubaliano ya awali,” amesema Mtendaji wa Kijiji, Paulo.
Sawe na Wales, wote wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 60, wanagombea eneo lililozua mzozo tangu mwaka 2018.
Mkazi wa Kijiji cha Mwajipugila, John Sawe (aliyemkata nduguye), amedai eneo lenye mgogoro alipewa mama yake katika mgawanyo wa maeneo ya ukoo baada ya baba yake kufariki dunia.
Amesema eneo hilo ndilo walilogawiwa wajukuu.
“Eneo tulilogawiwa sisi ni ambalo mama alipewa katika mgawanyo wa maeneo ya ukoo baada ya baba kufariki. Kila mtoto alipewa, ila mama alipewa kwa sababu baba hakuwepo.
“Katika maeneo waliyopewa wazazi, wajukuu tumepewa ekari sita kila mtu, ndugu wengine waliuza maeneo yao. Tuliobaki ni sisi wawili,” amesema.
Wales (aliyejeruhiwa mkono) ameeleza: “Mama yake hana eneo katika ardhi ile. Kwa nini apewe? Ameolewa katika familia hii.”
Wananchi wakiwa katika kikao cha usuluhishi.
Diwani wa Busangwa, Magenzi Charles, amesema kurejea kwa mgogoro huo kunatishia ustawi wa familia hizo, akisisitiza umuhimu wa jamii kuheshimu uamuzi wa wazee ili kulinda amani na mshikamano.
“Huu mgogoro uliwahi kutatuliwa na wazee wa ukoo, lakini umeibuka tena. Hatua hii inatishia ustawi wa familia hizi mbili. Ni muhimu jamii kuheshimu uamuzi wa wazee ili kulinda amani na mshikamano katika familia,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, ametoa onyo kwa wananchi, akiwataka wajukuu wa familia hizo kufuata kwa makini uamuzi wa ukoo uliogawanya eneo hilo.
“Wananchi wote mnatakiwa kuepuka kununua ardhi yenye migogoro. Kwa kufanya hivyo kunaweza kuwaletea athari za kisheria na kiusalama,” amesema.
Vilevile, amemtaka John Sawe kugharimia matibabu ya ndugu yake Wales kama hatua ya kurejesha utu na kuimarisha uhusiano wa kifamilia.
