Musoma. Mtoto Mariam Paye, mkazi wa Mtaa wa Zanzibar, Manispaa ya Musoma mkoani Mara, amefariki dunia baada ya kutumbukizwa kwenye shimo la choo na mtu anayedaiwa kuwa na tatizo la akili.
Mtuhumiwa huyo naye amefariki dunia baadaye kutokana na kipigo alichopata kutoka kwa wananchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja mtuhumiwa kuwa ni William Koda (20), ambaye alikuwa akikabiliwa na changamoto za afya ya akili.
Hata hivyo, Kamanda Lutumo amesema Koda alifariki dunia akiwa hospitalini alipokuwa akipatiwa matibabu, kufuatia majeraha aliyoyapata wakati wa kukamatwa na wananchi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Zanzibar, Hamisi Kuyenga amesema wananchi walimkimbiza na kufanikiwa kumkamata mtu huyo, kisha wakaanza kumpiga kabla ya kuokolewa na viongozi wa serikali ya mtaa.
“Tulimchukua na kumpeleka kituo cha polisi kwa usalama wake na hatua zaidi, huyo mtu ni mgeni kabisa hapa mtaani kwetu hatujawahi kumuona tunasubiri taarifa zaidi kutoka polisi,” amesema.
Akizungumzia tukio hilo, baba wa marehemu, Paye Ludala, amesema hana imani na taarifa zinazoeleza kwamba mtuhumiwa alikuwa na tatizo la akili.
Ludala amedai kuwa mazingira ya tukio hayaoneshi uhusiano wowote na madai hayo, ingawa amekiri kuwa bado hajafahamu sababu iliyomfanya mtuhumiwa kutekeleza kitendo hicho.
Akisimulia namna tukio lilivyotokea, Ester Misana, jirani wa familia hiyo, amedai kuwa Novemba 22, 2025, saa 10 jioni, alipokuwa akirejea nyumbani, aliwakuta watoto watatu wamesimama kando ya shimo la choo.
Misana amedai pia alimwona mwanaume mmoja, ambaye hakumfahamu, akiwa ameinama na kuchungulia ndani ya shimo hilo.
“Nilishtuka sana kwani yule baba aliinamia kwenye shimo kabisa kama anataka kutumbukia, harakaharaka nikahisi ni mtu anataka kujiua nikamuuliza wewe ni nani unataka kujiua kwenye mji wangu akashtuka na hapohapo akavua yeboyebo zake akazishikilia mkononi na kuanza kukimbia,” amedai.
Amedai baada ya mtu huyo kukimbia alibaini kuwa alibomoa baadhi ya matofali yaliyokuwa yametumika kuziba tundu la shimo hilo la choo, hali ambayo ilisababisha azidi kuamini kuwa mtu huyo alikuwa na lengo la kujiua.
Misana amedai kuwa, baada ya kuona hali hiyo, alipiga kelele kuwaomba majirani wamsaidie ili waweze kumkamata mwanaume huyo na kubaini sababu iliyomfanya achungulie ndani ya shimo hilo kama mtu aliyekuwa akijaribu kujitumbukiza.
“Watu walifika nikawaelezea ndipo wakaenda kuangalia lile shimo ambapo baba mmoja akasema mbona kuna mtu humu kwenye shimo, nami nikaenda kuangalia kweli nikaona kichwa cha mtu na mkono palepale nikapoteza fahamu,” amedai.
Shuhuda mwingine, Mohamed Malika, amedai alisikia kelele kutoka kwa jirani na akaamua kwenda kuangalia kilichokuwa kimetokea ili kutoa msaada.
Akiwa njiani kuelekea eneo la tukio, alikutana na mtu mmoja aliyekuwa akikimbia huku amebeba viatu mkononi.
“Baada ya kufika na kuambiwa kuna mtu alitaka kutumbukia kwenye shimo la choo nilielekea kwenye shimo hilo na baada ya kuangalia vizuri niliona kichwa cha mtu nikawaambia watu ambao tayari walikuwa wamefika kuwa kuna mtu ndani ya shimo,” amesema.
Kufuatia hali hiyo walianza taratibu za kumuokoa mtu huyo ambaye baadaye ilibainika kuwa ni mtoto.
Amesema walifanikiwa kumtoa akiwa hai ingawa alikuwa amechoka sana kiasi cha kushindwa hata kusimama na kulazimika kumpa huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, mtoto huyo alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitalini.
