Dar es Salaam. Familia ya aliyekuwa kinara wa upinzani na Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, hayati Raila Odinga imepata msiba mwingine baada ya dada wa kiongonzi huyo, Beryl Odinga, kufariki dunia.
Kwa kujibu wa vyombo vya habari vya Kenya ikiwemo Taifa Leo, kifo chake kimetangazwa na dada yao mdogo, Ruth Odinga, ambaye amesema Beryl amefariki leo Jumanne, Novemba 25 ingawa hajasema chanzo cha kifo hicho.
Kifo cha Beryl kinakuja ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu kutokea kifo cha Odinga ambaye alizikwa katika makaburi ya familia.
“Ni kwa moyo mzito lakini tukikubali mapenzi ya Mungu, tunatangaza kifo cha ghafla cha Beryl Achieng Odinga. Binti wa marehemu Jaramogi Oginga Odinga na Mama Mary Ajuma Oginga. Mama yake Ami Auma, Chizi na Taurus.
“Ingawa tumehuzunishwa sana na kifo chake na pengo kubwa aliloliacha maishani mwetu, tunapata faraja tukiamini yuko salama mikononi mwa Bwana na tunashukuru kwa zawadi ya muda tuliojaliwa kushiriki naye,” amesema.
Hata hivyo imeelezwa kuwa Beryl alikuwa mgonjwa kwa muda na hakuweza kuhudhuria mazishi ya kaka yake kutokana na hali yake ya kiafya.
Beryl ni mtoto wa viongozi mashuhuri katika historia ya siasa za Kenya, hayati Jaramogi Oginga Odinga na Mary Ajuma Oginga. Ameacha watoto watatu Ami Auma, Chizi, na Taurai ambao aliwapenda na kuwalea kwa kujitolea.