Dodoma. Mara baada ya kuingia kwenye chumba cha mafunzo yaliyoandaliwa kwa ajili ya wadau wa elimu, nilibaini jambo lililonishangaza. Ilikuwa mara ya kwanza kukutana na mkufunzi asiyesikia.
Alikuwa akizungumza kwa kujiamini akitaka watu wamsikilize vizuri, kwa haraka ilikuwa ni vigumu kwangu kubaini kwamba yeye mwenyewe hasikii anachokisema hadi pale mwenyewe alipoliweka wazi hilo na pale aliposogea kwa mkalimani wa lugha ya alama alipotaka kusikia kinachozungumzwa na mtu mwingine.
Huyu ni Daniel Reuben mbombezi wa masuala ya elimu jumuishi aliyevunja ukuta kwamba watu wenye uziwi ni vigumu kuwasiliana na wasio na changamoto hiyo.
Kupitia mafunzo yaliyoandaliwa na shirika la Hakielimu kupitia mradi wa Sauti Zetu, kijana huyu mwenye miaka 27 ambaye kitaaluma ni mwalimu wa elimu maalumu alionesha umahiri wa hali ya juu katika kufundisha na kulifanya darasa lake kuwa shirikishi licha ya kuwa yeye hasikii kabisa.
“Mimi sisikii ila naamini nyie mnanisikia vizuri, kwa maana hiyo ni imani yangu tutaelewana na tutafikia lengo la mafunzo haya. Kama mimi kiziwi lakini niljifunza nikaelewa naamini nyie mnaosikia itakuwa rahisi zaidi na nahitaji kuwa na darasa shirikishi,” anasema Daniel wakati akianza kufundisha.
Alichokisema ndivyo ilivyokuwa muda wote wa uwasilishaji wa mada yake iliyohusu uwajibikaji na ujumuishwaji wa kijamii katika kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ikiwemo wenye ulemavu kwa kuzingatia mahitaji yao.
Mahojiano naye
Hilo lilinipa shauku ya kuzungumza ya kufanya mahojiano naye kwa msaada wa mkalimani wa lugha ya alama, aliyenisaidia kuwasilisha maswali yangu kwake na yeye akayajibu kwa ustadi mkubwa.
Katika mahojiano hayo ndipo nilipobaini Daniel hakuwa amezaliwa na uziwi, lakini kadiri alivyokuwa anakua masikio yake yalianza kupoteza uwezo wa kusikia na alipofika kidato cha tatu hali ikawa mbaya zaidi.
Hata hivyo, si yeye mwenyewe wala wazazi wake walioweza kung’amua hilo, kila alipoambiwa kitu na kutofanya kama alivyoelekezwa au kutoitika kwa wakati alipoitwa alionekana kuwa na kiburi.
“Nilianza kuonekana mkorofi, inaweza kutokea nimeitwa au nimeambiwa kitu lakini sifanyi kama inavyotakiwa kwa sababu sijasikia. Sasa ikitokea labda nafokewa na mimi sikubali nabisha basi hapo ndipo tatizo linapoanza nikaonekana ghafla nimekuwa mtukutu,”
Hali iliendelea hivyo hadi alipofika kidato cha tatu ambapo mmoja wa walimu wake alianza kuhisi tatizo, hisia hizo zilianza baada ya kuonekana anaanza kushuka kitaaluma na hajibu maswali kama ilivyokuwa hapo awali.
“Mwalimu yule alikuwa mtu wangu wa karibu, hivyo alishtushwa na mabadiliko yangu na akawasiliana na wazazi wangu kuwaeleza kile alichohisi na kuwashauri wanipeleke hospitali kwa ajili ya vipimo na matibabu.
“Ushauri huo ulizingatiwa nilifanyiwa uchunguzi nikabainika kwamba masikio yangu yanapoteza uwezo wa kusikia, nikaanzishiwa matibabu lakini hiyo haikusaidia kadiri siku zilivyozidi kwenda nikawa sisikii kabisa kila sauti kwangu niliona kelele,” anasema.
Huo ukawa mwanzo mpya wa maisha ya Daniel baada ya kubaini uwezo wa masikio yake kusikia ulizidi kupotea, hata hivyo hakutaka kukubaliana na uhalisia huo hivyo akawa analazimika kuikataa hali hiyo mbele ya wenzie.
“Ilifikia hatua nikikaa na wenzangu nashindwa kwenda sambamba na stori, mimi ni mtu wa kujichanganya lakini ile hali ikanifanya nianze kuwa tofauti. Mbaya zaidi wenzangu wakawa wananicheka na kunidhihaki kuwa sisikii hapo nikaanza kujitenga na kujiweka mbali na watu,’’ anaeleza.
Aliendelea hivyo hadi pale alipomaliza kidato cha nne na kufanikiwa kupata ufaulu uliomwezesha kuchaguliwa kidato cha tano katika shule ya sekondari Mara, hata hivyo wazazi wake walishauriwa wasimpeleke huko badala yake wamtafutie shule yenye miundombinu itakayoendana na hali yake ya ulemavu.
Hivyo ndivyo ilivyofanyika akapelekwa sekondari ya Kazima ambayo licha ya kutoa elimu jumuishi ilikuwa na kituo maalumu cha kupima hali ya ulemavu sambamba na vifaa saidizi vinavyotolewa kwa mlengwa kulingana na hali yake ya ulemavu.
Akiwa shuleni hapo, alisoma kwa bidii na juhudi zake zikazaa matunda, alipomaliza kidato cha sita akachaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dodoma alikoenda kusomea shahada ya ualimu akijikita kwenye elimu maalumu.
“Nilitamani niwe sehemu ya kutatua changamoto ya uhaba wa walimu maalumu, kuna watoto wenye mahitaji maalumu wana nia ya kujifunza lakini wanakosa walimu wanaokidhi viwango vya kuwafundisha kwa sababu waliopo ni wachache.
Nilienda chuoni nikiwa na shauku kubwa, sikuishia kusoma nilijihusisha na programu kadhaa zinazopigia chapuo elimu jumuishi. Hata hivyo nilipohitimu shahada yangu sikupata kazi ya ualimu licha ya kutuma maombi kadhaa,”anasema.
Anasema hali hiyo haikumkatisha tamaa badala yake ikamfanya afikirie nje ya boksi kitu gani kingine anaweza kukifanya kwa kutumia taaluma yake na maarifa aliyoendelea kuyatafuta tangu alipojikubali kuwa yeye ni kiziwi.
Hapo ndipo alipoamua kujikita kwenye saikolojia eneo la watu wenye ulemavu akitumia maarifa aliyoyapata kwenye ualimu na uzoefu kujichanganya na kundi hilo.
“Nilianza kuomba nafasi za kujitolea kwenye mashirika yanayohusika na watu wenye ulemavu huku nikiendelea kujijengea uwezo na sasa naweza kueleza kwa kujivunia kabisa kwamba nimebobea kwenye ushauri kwenye elimu jumuishi nikijikita kwenye eneo la watu wenye ulemavu,”.
Katika eneo hilo amekuwa akifanya utafiti, akiandaa na kusimamia maandiko ya miradi na wakati mwingine kutakiwa kuwasilisha kwenye vikao ambapo analazimika kuwa na mkalimani ambaye wakati mwingine analazimika kumlipa yeye mwenyewe ili kazi yake ifanyike kwa ufanisi.
Licha ya dhihaka, unyanyapaa na vikwazo kadhaa alivyokutana navyo, neno kukata tamaa ni marufuku kwa Daniel na anaamini kwamba hata watu wengine wenye ulemavu wanaweza kufanya vitu endapo watapewa nafasi.
Anasema ni vyema jamii ikaachana na dhana ya kuangalia ulemavu wa mtu badala yake iangalie anaweza kuwa na mchango gani na kumuwekea mazingira wezeshi ili aweze kutoa mchango huo.
“Kuwa mlemavu haimaanishi hawezi kufanya vitu vingine, ifike pahala jamii iache kumuangalia mtu kwa ulemavu alionao ila aangaliwe ni kitu gani anaweza kufanya na kama kuna vikwazo basi asaidiwe kuviondoa ili aweze kutoa huo mchango wake,’ anasema.