‘Dk Mapana ni chachu ya mabadiliko kwa vijana’

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Dk Kedmon Mapana kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, wadau wameeleza namna kiongozi huyo alivyosaidia vijana kimaendeleo.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Mapana alikuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na alijulikana kwa karibu na wasanii wanaojihusisha na sekta ya muziki, sanaa na ubunifu.

Akiwa katika baraza hilo, Dk Mapana alikuwa akisema hawamvizii msanii akosee ili wamfungie kwa kuwa, suala hilo sio ajenda yao bali ni kusaidia wasanii.

Tofauti na Basata, pia alikuwa Mhadhiri Mkuu wa Sanaa Bunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hapo alijenga msingi wa kitaaluma na uelewa wa changamoto zinazowakabili wasanii na vijana.

Kutokana na ukaribu wake na vijana, uteuzi wake wa kuwa Naibu Katibu Mkuu unatarajiwa kuleta uwazi, uratibu bora na kuimarisha juhudi za Serikali katika kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi na maendeleo.

Katika hotuba yake alipolizindua Bunge la 13 Novemba 14, 2025 Rais Samia alisema zaidi ya asilimia 60 ya watu nchini ni vijana, Serikali itaweka kipaumbele kwenye sera na programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi na ajira, kuongeza wigo wa hifadhi za jamii na kuwajengea kesho bora.

Alisema lengo ni kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki kujenga mustakabali mwema wa Taifa.

“Tutaweka ushirikishwaji wa vijana katika masuala ya maendeleo yao. Natambua kumekuwa na majukwaa mengi ya kufikia vijana ila bado shughuli zao zinafifishwa na masuala ya kisiasa na majukwaa hayo kupoteza malengo na mvuto kwa vijana,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo, vijana wanaomfahamu Dk Mapana humuita, “Mbani,” neno linalomaanisha mtu anayekaribisha na kulea, akiwasaidia kugundua uwezo wao na kupata mwongozo wa maisha.

Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki iliyopita, Placidi Lala, mmoja wa vijana waliopitia katika mikono yake amesema, “Dk Mapana si mwalimu wa darasani pekee, ni kiongozi anayeshuka hadi chini, kukaa na vijana, kuwasikiliza na kuwaongoza kwenye fursa zinazobadilisha maisha. Anatutoa kwenye mazingira magumu na kuunganisha na dunia ya ubunifu.”

Lala amesema moja ya miradi aliyoianzisha ni Festival ya Jude, jukwaa linalowawezesha vijana kuonesha ubunifu wao katika muziki, maigizo, ngoma, filamu na maonesho ya magari.

Amesema watu wengi walitoka hapo wakiwa na fursa na waliona maisha yakibadilika, kwa kuwa tamasha hilo limekuwa chombo cha kupata kazi na kuwaandaa vijana kuingia kwenye tasnia ya sanaa kwa njia ya kitaalamu.

Amesema pia, alianzisha mashindano ya timu za vyuo vya juu, mradi unaowaunganisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali kujionesha katika uimbaji, utunzi na sanaa za maonesho.

“Mpango huu umeibua nyota chipukizi na kuongeza kujiamini kwa vijana wanaoingia kwenye tasnia ya sanaa,” amesema Lala.

 “Alikuwa akitufundisha namna ya kuelewana na wasanii, kuwasaidia na kuwapa huduma bora. Haya mambo sasa yanaonekana ndani ya Basata.”

Amesema nafasi ya Dk Mapana ipo katika kuelewa na kujiweka karibu na vijana, kuwaongoza kwa moyo wa kujitolea na kuamini uwezo wao. Ni mtu mwenye mawazo mapana.

“Kwa vijana, Dk Mapana ni hazina kila hatua yake ni jembe linalopanda kwenye maisha ya vijana, na kuonesha kuwa kesho inaweza kuwa bora.”

 Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere, Dk Ahmed Sovu amesema Dk Mapanani mtu mvumilivu na mstahamilivu, sifa ambazo ni muhimu hasa kwa viongozi wa wizara zinazogusa vijana.

Amesema vijana mara nyingi wanapenda mambo ya haraka, lakini Dk Mapana ana tabia ya kupumzika, kuchambua hali na kutafuta matokeo bora kabla ya kuchukua uamuzi.

“Kijana anapenda kuona matokeo haraka, lakini Dk Mapana anaweza kupumzika, kutathmini hali na kisha kufanya uamuzi sahihi. Hii ni sifa muhimu kwa kiongozi wa wizara hii,” amesema Dk Sovu.

Pia, amesema Dk Mapana anapenda maendeleo na anaweka muda wake wote kuhakikisha kazi zinafanyika kwa wakati. Tabia hii inaendana na mahitaji ya vijana.

“Anaweka wazi muda wa kufanya jambo na kuhakikisha linafanyika kwenye muda uliopangwa. Hii itasaidia kuimarisha nidhamu kwa vijana,” amesema Dk Sovu.

Akizungumzia uzoefu wao huku akitaja safari yao ya kitaaluma Cuba, amesema kiongozi huyo aliweza kupanga jukwaa la Tamasha la Kiswahili, licha ya changamoto zilizokuwa zinawakabili, jambo linaloonesha ni kiongozi mbunifu na mwenye maono.

 “Dk Mapana ana uwezo wa kushirikiana na wizara nyingine, kuhakikisha miradi ya vijana inafanikiwa na kila kiongozi atakayekuwa naye anaweza kumtumia kwa sababu anazoeana na watu haraka, hivyo watafanikiwa kwa hili la vijana,”amesema.

Pia, amebainisha kuwa Dk Mapana anafuatilia mambo hadi yafanyike kwa usahihi, jambo linalothibitisha kuwa ni kiongozi anayejali maendeleo ya watu wake.

Mwanamuziki Selemani Mnindi, maarufu kwa jina la Afande Sele, amesema Dk Mapana anaeleweka na anaufahamu mpana kuhusu changamoto zinazowakabili vijana na wasanii, hivyo anatarajiwa kuleta mabadiliko ya kweli.

“Kwa muda mrefu tumekuwa hatupati kiongozi anayetuangalia kwa jicho la karibu. Tulikosa mwongozo, ushirikishwaji na hamasa, lakini kuingizwa kwa Dk Mapana kunatupa matumaini, kwa sababu ana uzoefu, ana uwazi na anajua kilio cha vijana,” amesema Afande Sele.

Amesema awali kabla ya Dk Mapana kuingia Basata mara kadhaa kulikuwa na ukosefu wa uratibu unaozingatia mazingira halisi ya wasanii.

Amesema anaamini Dk Mapana atakwenda kuihuisha wizara hiyo kwa kusimamia ubunifu bila kuiumiza tasnia, dhamira ya Serikali ni kuwatambua vijana kama nguvu kazi yenye mchango mkubwa, hususani katika sanaa na ubunifu.

Afande Sele amesema nafasi aliyopewa ni kubwa, inataka mtu mwenye maono na uthubutu. Vijana wana changamoto nyingi, ukosefu wa ajira, mitaji na  mazingira rafiki ya ubunifu kama ataendelea na msimamo wake wa kuwashirikisha vijana, basi wanaamini kutakuwa na matokeo makubwa.

“Kazi yake haitakuwa rahisi, lakini anaweza, vijana tukishirikishwa, tukapewa mazingira mazuri ya ubunifu, tutajenga Taifa lenye matumaini. Serikali imeshaonesha njia, sasa ni zamu yetu,” amesema Afande Sele.

Msanii wa muziki wa singeli, Selemani Jabir maarufu Msaga Sumu amesema kwa muda mrefu, Dk Mapana amejitambulisha kama kiongozi anayeiona fursa kubwa kwa vijana na asiyechagua wala kubagua.

Amesema hii ni nafasi ambayo ameiweka kwa vitendo, akihakikisha vijana wanapata usaidizi wa kweli bila ya masilahi binafsi. Dk Mapana ameweza kufanya muziki wa singeli kutambuliwa na kuthaminiwa.

“Wakati watu wanatukataa, wanasema singeli ni kelele, ni muziki wa watoto wa mtaa, yeye hakuwaona hivyo. Alitupeleka kwenye majukwaa makubwa, alituondoa kwenye hofu ya Basata na kutufundisha jinsi ya kufanya kazi zenye maudhui bila kupoteza utambulisho wa singeli,” amesema Msaga Sumu.

Amesema Dk Mapana amekubali mialiko kutoka maeneo ya ndani, ikiwamo matamasha madogo yaliyopangwa na wanamuziki wa singeli wenye nia ya kuibua vipaji.

Amesema amepandisha muziki wa singeli kwenye majukwaa ya kisiasa na kitaasisi, hivyo kuipa heshima inayostahili bila kuangalia ukubwa wa msanii.

Msaga Sumu amesema kwa hatua hizo, singeli sasa inachukuliwa kama muziki wa kitaifa, unaoshiriki kwenye maonesho makubwa na kuendeleza vipaji vya vijana.