Dar es Salaam. Wakati kesho Novemba 26, 2025 dunia ikiadhimisha siku ya kupinga uzito uliokithiri (anti-obesity day) wataalamu wametahadharisha hali hiyo kuwa ni hatari ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kiharusi, moyo, saratani, kisukari, shinikizo la juu la damu.
Kitaalamu uzito uliokithiri ni hali ya uwepo wa hifadhi ya chakula kisichotumika (mafuta) mwilini ambayo kiafya ni hatari kwani muhusika anakuwa karibu kupata magonjwa hayo yasiyoambukiza (NCDs).
Ikumbukwe takwimu mpya za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi duniani (UNHCR), zinaonesha asilimia 71 ya vifo vyote duniani sawa na vifo milioni 41, vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza.
Uzito uliopitiliza ni kuwa na uzito mkubwa kupita kiwango kinachoshauriwa kwa urefu wa mtu. Kwa kawaida, hii hupimwa kwa kutumia BMI (Body Mass Index). Ili kujua mtu ana uzito ulipitiliza wataalamu hufanya vipimo vya uwiano wa uzito na urefu.
Uzito uliokithiri unatokana na ulaji usiofaa, urithi wa familia, unywaji wa pombe, kutokufanya mazoezi pamoja na mtindo wa maisha.
Watu wengi wamekuwa wakifanya jitihada za kupunguza uzito ikiwemo kujiunga na sehemu za mazoezi (gym), kukimbia katika vikundi vya jogging sambamba na kujinyima kula. Ingawa baadhi yao hawapati matokeo kama wanavyotarajia baada ya kuchukua hatua hizo
Kwa nini ni vigumu kupunguza uzito
Akifanya mahojiano maalumu na gazeti hili leo Jumanne Novemba 25, 20225 mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Dk Cecilia Mshanga anasema kitendo cha kupungua uzito si cha muda mfupi kama wengi wanavyodhani.
“Mtu anayekula chakula kingi hasa wanga na mafuta bila kukitumia kwa maana wengi hatufanyi mazoezi tafsiri yake chakula hicho kinahifadhiwa ndipo unakuta mtu ni mzito sana.
“Ukila chakula mwili unachukua kile unachohitaji kingine inahifadhi kila siku kama akiba. Asubuhi unaweka akiba, mchana, jioni mwili unachakata inakuwa mafuta inahifadhi. Kwa hiyo kila siku unaweka akiba. Mwili ukitaka utumie hiyo akiba hadi ukose chakula kinachoingia,”amesema.
Ameongeza kwamba kitendo cha kufanya mazoezi na kujinyima kula ili uzito upungue si cha muda mfupi kama watu wengi wanavyodhani kwani linaweza kuchukua zaidi ya mwaka.
“Tafsiri ni kwamba lazima mtu ujinyime kula kwa kupunguza kiasi cha chakula unachokula kisha ufanye mazoezi hadi pale mwili utakapoanza kukosa chakula cha nje, kisha uanze kutumia kile cha ndani ambacho kimehifadhiwa,
“Mwili ukishtuka ukaanza kuhisi kipimo cha chakula kinachoingia kimepungua ndipo kitaanza kutumia chakula kilichohifadhiwa, maana mwili utakuwa unajichoma kupunguza mafuta na chakula hicho,”amesema
Amesema jambo hili si la siku moja kama wengi wanavyodhani kwani huchukua muda kidogo hadi pale mwili utakapoanza kuzoea mabadiliko hayo.
“Kupunguza uzito ni ngumu kuliko kuongeza kwa kuwa ukitaka kuongeza ni jambo rahisi kutokana na ulaji mbaya. Leo hii ukitaka kuongeza uzito wewe kula tu vibaya usifanye mazoezi utaona matokeo ndani ya muda mfupi sana,”amesema.
Dk Cecilia anashauri watu kupungua kiasi cha chakula wanachokula kwa sasa hadi pale saizi inayohitajika ili kuepusha kurundika chakula kingi mwilini.
Akizungumza na Mwananchi, Diana Reuben kutoka Dar es Salaam anasema amekuwa akifanya juhudi za kupunguza uzito kwa muda wa miezi miwili sasa tangu apate ushauri wa daktari, ingawa hajaona matokeo.
“Nilipima mara ya mwisho nikiwa na kilo 90 nikashauriwa kupunguza uzito huu ni hatari kwa sasa nakula mara mbili kwa siku, nafanya mazoezi lakini nimepima nimekuta nina kilo 89. Sijakata tamaa naendelea nikitumai nitapungua,” amesema.
Siku yenyewe
Anti-Obesity Day, ni siku maalumu inayolenga kuongeza uelewa kuhusu hatari za afya zinazotokana na uzito uliopitiliza, sambamba na kuhimiza jamii kuchukua hatua za kuboresha maisha kwa kuzingatia lishe bora na kufanya mazoezi.
Siku hii, iliyoanzishwa mwaka 2001 na kampuni ya huduma za afya ya VLCC, inalenga kuikumbusha jamii umuhimu wa kuzuia ongezeko la uzito kupita kiasi, tatizo ambalo limeendelea kuongezeka katika mataifa mbalimbali, ikiwamo Tanzania, kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha na ulaji wa vyakula visivyo na uwiano sahihi.
Katika kuadhimisha siku hii, mataifa mbalimbali huandaa matukio ya mazoezi ya pamoja, warsha za lishe na kampeni za uhamasishaji. Wakazi wa mijini na vijijini wanahimizwa kushiriki matembezi, kukimbia, kufanya mazoezi ya viungo pamoja na kusikiliza ushauri wa wataalamu.
Kampeni za Anti-Obesity Day pia zinahimiza jamii kupunguza unyanyapaa dhidi ya watu wenye uzito mkubwa na badala yake kutoa ushirikiano na ushauri unaowasaidia kufanya mabadiliko ya afya kwa njia rafiki na endelevu.
Tangu kuanzishwa kwake, siku hii imesaidia kuanzisha mjadala mpana kuhusu afya ya jamii, huku mataifa mengi yakitumia fursa hiyo kuweka mikakati ya kudhibiti ongezeko la uzito kwa watu wa rika zote.
Kwa ujumla, Anti-Obesity Day inabeba ujumbe mmoja muhimu:
Afya njema inaanza na hatua ndogo kula vizuri, fanya mazoezi, na chukua hatua mapema.
