Dodoma. Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amewataka watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara na kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya umeme ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la kukatika umeme nchini.
Makamba ametoa agizo hilo leo Novemba 25, 2025, jijini Dodoma alipofanya ziara katika kituo cha kupooza umeme cha Zuzu.
Amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miundombinu ya umeme, na kubainisha kuwa kituo hicho kimeongezeka uwezo maradufu tangu kianzishwe mwaka 1986.
“Tunajivunia kama Taifa. Wakati kituo hiki kinaanzishwa mahitaji ya umeme yalikuwa megawati mbili, lakini leo mahitaji ni megawati 86. Kituo kina uwezo wa kutoa zaidi ya megawati 200 na hivyo kukidhi mahitaji ya Mkoa wa Dodoma unaokua kwa kasi,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kukiongezea kituo hicho nguvu kwa kujenga njia ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, mradi unaotarajiwa kukamilika mwaka 2026.
Kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha nchi kusafirisha umeme wote kutoka Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
“Huu ni uwekezaji mkubwa tunaoujivunia. Nchi jirani zinatamani kufika tulipo. Wananchi watembelee kifua mbele kwa sababu kazi inayofanyika inalenga kuhakikisha umeme wa uhakika unawafikia,” amesema Makamba.
Aidha, amewataka watumishi wa Tanesco kuhakikisha hakuna uharibifu wa mitambo na kusisitiza matengenezo ya mara kwa mara pamoja na ulinzi wa karibu wa miundombinu hiyo ya mabilioni ya pesa.
“Tunataka umeme upatikane saa 24 bila kukatika. Hii itawawezesha wananchi na viwanda kuzalisha ipasavyo. Mafundi na wahandisi wahakikishe matengenezo yanatekelezwa kwa wakati,” amesisitiza.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Athanasius Nangali, amesema shirika litaendelea kulinda na kusimamia miundombinu hiyo ili iendelee kuleta tija kwa Taifa. Amewataka pia wawekezaji kuendelea kujitokeza kwa kuwa uzalishaji wa umeme ni wa uhakika kupitia kituo hicho.
Ziara ya Makamba ni sehemu ya juhudi za Serikali kufuatilia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya nishati ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wa kuaminika.
