Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kiwango cha uharibifu kilichotokea katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam hakikubaliki na hakioneshi taswira ya taifa linalotaka kusonga mbele. Akizungumza kuhusu tukio hilo, Waziri Mkuu amesema uharibifu huo umeathiri mali za serikali, sekta binafsi na maisha ya wananchi wa kawaida.
Dkt. Mwigulu alieleza kuwa hadi sasa takwimu za awali zinaonesha uharibifu wa:
-
Ofisi za Serikali 756
-
Vituo vya mabasi yaendayo haraka (mwendokasi) 27
-
Mabasi sita
-
Mali binafsi ikiwa ni nyumba 273
-
Vituo vya polisi 159
-
Vituo binafsi vya mafuta 672
-
Magari binafsi 1,642
-
Pikipiki binafsi 2,268
-
Magari ya serikali 976
Waziri Mkuu amesema vitendo hivyo vimeathiri pakubwa maisha ya wakazi wa Dar es Salaam ambao kwa kawaida hutegemea kusafiri kutoka hatua moja kwenda nyingine kila siku. Ameeleza kuwa hakuna Mtanzania aliyejilimbikizia mali kiasi cha kuweza kukaa ndani kwa mwaka mzima bila kutoka.
“Haya si maisha ya Serikali… na hizi ni takwimu za mwanzo,” alisema Dkt. Mwigulu.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua na kufanyia kazi taarifa zote za uhalifu, akisisitiza kuwa suluhisho la jambo baya si kuruhusu mabaya zaidi kutokea.
“Tuna mambo tunayoyaona na tunaendelea kuyafanyia kazi. Jambo baya likitokea, dawa yake si kuruhusu mengine mabaya zaidi. Wapo wasioutakia mema nchi yetu, wangetamani jambo baya litokee,” alisema.
Katika uchambuzi wake, Waziri Mkuu alionya kuwa mataifa yenye rasilimali nyingi, kama Tanzania, ndiyo yanayolengwa zaidi na njama za kuchochea migogoro.
“Hivi ndivyo hufanyika kwa nchi zenye rasilimali nyingi. Nchi maskini zisizo na rasilimali hazijawahi kugawanyika. Waliowahi kuharibikiwa walifanya mizaha, hawakujua matokeo. Walikuja kujua kwenye majuto.”
