Profesa Kabudi: Sekta ya habari yapiga hatua, waandishi 3,200 watambuliwa kitaaluma

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema jumla ya waandishi wa habari 3,200 nchini wamepatiwa ithibati na kutambuliwa rasmi kufanya kazi ya kitaaluma.

Akizungumza katika mkutano baina ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, na wahariri pamoja na waandishi wa habari uliofanyika leo Novemba 25, 2025, katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Profesa Kabudi amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maboresho ya Serikali kwenye sekta ya habari, ikiwemo marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari.

Amesema kuwa usajili na utoaji wa ithibati kwa wanahabari ni mchakato unaolenga kuimarisha taaluma na kuhakikisha tasnia ya habari inafanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa.

“Bodi ya Ithibati imeundwa na imeanza kazi. Hadi leo, waandishi wa habari 3,200 pamoja na mimi mwenyewe wameshapewa ithibati na kutambuliwa kitaaluma,” amesema Profesa Kabudi.

Amefafanua kuwa lengo la kuanzishwa kwa chombo hicho si kudhibiti wanahabari, bali ni kulea, kukuza na kuimarisha taaluma ya habari nchini.

Profesa Kabudi pia amewashukuru wahariri na vyombo vya habari kwa kudumisha utulivu nchini, hususan wakati wa kampeni na baada ya uchaguzi mkuu, akisema wameendelea kutanguliza masilahi ya Taifa.

“Niwashukuru wahariri na vyombo vya habari kwa kuendelea kuhakikisha kuna utulivu miongoni mwa Watanzania. Kipindi cha kampeni na baada ya uchaguzi mmeonyesha uadilifu na weledi mkubwa,” amesema.

Sambamba na hayo, Profesa Kabudi amesema Serikali inakamilisha mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003.

“Baada ya muda si mrefu tutawasiliana nanyi ili kupata maoni yenu kuhusu mapitio ya sera hiyo, ili tuiimarishe zaidi kwa masilahi ya vyombo vya habari na Watanzania kwa ujumla,” amesema.