Songwe. Serikali inatarajia kutoa Sh200 bilioni kwa ajili ya kutunisha mfuko wa mikopo ya wajasiriamali na vijana nchini, fedha ambazo zitapitia benki ya NMB ndani ya siku 100 za serikali ya awamu ya sita.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana), Joel Nanauka akiwa katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma mkoani Songwe.
Amesema fedha hizo hazikutolewa awali kutokana na uchache wake, hivyo Serikali imeamua kuongeza kiasi hicho ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi, hususan vijana wanaojitafutia kipato.
Ameonya viongozi watakaochelewesha au kukwamisha fursa za vijana, akisisitiza kuwa wizara haitavumilia ucheleweshaji au kutoa taarifa zisizo na matumaini kwa wanaoomba mikopo. Ametaka vijana wapewe elimu ya kutimiza vigezo vya kupata mikopo, na yeyote atakayebainika kukwamisha jitihada hizo atachukuliwa hatua.
Ili kuzuia vitendo vya rushwa katika utoaji wa mikopo kwenye halmashauri, wizara itaunda mfumo maalumu utakaowawezesha vijana kutoa taarifa moja kwa moja wizarani na kubaini viongozi wanaohitaji rushwa wakati wa mchakato wa mikopo.
Waziri Nanauka amewataka vijana kudumisha amani na kujiepusha na makundi yenye nia ya kuvuruga umoja wa nchi.
Awali, Mwenyekiti wa bajaji katika mji wa Tunduma, Mwinyi Haji Khamis amesema kuchelewa kutekelezwa kwa ahadi ya Serikali ya mikopo kupitia NMB kumeondoa imani kwa vijana. Ameomba utekelezaji ufanyike kwa wakati ili kurejesha imani hiyo.
Amesema baadhi ya viongozi wamegeuza mikopo ya asilimia 10 kuwa chanzo cha kipato kupitia rushwa, hali inayopoteza imani ya wananchi licha ya kuwa na mwongozo wa utoaji mikopo. Ameitaka Serikali kuja na mpango madhubuti wa kuondoa mianya ya rushwa na kufuatilia fedha zinazotolewa kupitia NMB ili ziwafikie walengwa.
Bernard Kayange, mmoja wa machinga, ameiomba Serikali kuongeza asilimia za mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kufikia asilimia 25, ili vijana wapate asilimia 15 badala ya asilimia nne za sasa ambazo hazitoshi.
Elizabeth Mwasambube, ambaye pia ni machinga, amesema Serikali inapaswa kutoa ajira za muda kwa vijana ili kuwasaidia kupata kipato na kupunguza vitendo vya uhalifu mitaani.
