Tani 131,000 za mahindi zakosa soko Chunya, sababu yatajwa

Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, imesema wastani wa tani 131,000 za zao la mahindi katika msimu huu zimekosa soko.

Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 25, 2025 na Msimamizi wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Cuthbert Mwinuka, akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu changamoto za soko la zao hilo na mikakati iliyopo.

Mwinuka ametaja sababu ya wakulima kuhamasika kuzalisha ni baada ya Serikali kutoa pembejeo za kilimo, hususan mbolea ya ruzuku kwa wakati.

“Wakulima walihamasika sana kuzalisha licha ya uhaba wa soko, lakini tumeomba Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)  kuona namna ya kununua ili kuwasaidia wakulima,” amesema.

Amesema idadi ya wakulima waliofaidika na mbolea ya ruzuku imeongezeka kutoka 16,984 hadi 32,000 kati ya mwaka 2021 na 2025, sambamba na ongezeko la pembejeo kutoka tani 10,000 hadi 17,000.

“Tunaomba Serikali kuona namna NFRA inaweza kununua ziada ya mahindi iliyohifadhiwa na wakulima ili kuwasaidia kuondokana na changamoto na kufanya maandalizi ya msimu huu wa kilimo,” amesema.

Anita David, mkazi wa Kijiji cha Lupa, amesema Serikali iingilie kati kwani wakulima walitumia nguvu kubwa katika uzalishaji, lakini bado changamoto ni masoko.

“Idadi kubwa tunategemea kuendesha maisha kwa kilimo. Sasa hali ni tofauti na tulivyokusudia. Wengine waliachwa bila mitaji ya kuwekeza katika msimu huu wa kilimo. Tunaomba Serikali kulitupia macho,” amesema.

Daniel Mturo, mkazi wa Itumbi, amesema wanaomba Serikali kutatua changamoto ya soko kwa kutafuta wanunuzi watakao nunua kwa bei nzuri.