TFS yakabidhiwa magari ‎kuimarisha uhifadhi Uzungwa, Kilombero

Iringa. ‎Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) umesema shughuli za uhifadhi misitu ya Udzungwa na Kilombero zinatarajiwa kuimarika kupitia matumizi ya magari mapya ya doria, yatakayowapa wahifadhi uwezo wa kufika kwa ufanisi zaidi katika maeneo muhimu ya misitu hiyo iliyopo mkoani Iringa na Morogoro.

TFS wameeleza kuwa magari hayo mapya ya doria aina ya Toyota Land Cruiser kutoka Mpango wa Mandhari ya Udzungwa (ULS) unaoratibiwa na STEP, yataimarisha ulinzi wa misitu na kufungua maeneo muhimu ya Udzungwa na Kilombero yaliyokuwa hayafikiki kwa urahisi na kuongeza ufanisi wa doria katika kulinda misitu ya asili.

‎Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo Jumatatu Novemba 24, 2025 katika ofisi za STEP, Wilolesi mkoani Iringa ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa uhifadhi kutoka TFS, STEP, ULS na wadau wengine wa misitu,  ambapo TFS imesema inatarajia kasi ya ufuatiliaji, kupunguza uharibifu wa misitu na kuimarisha juhudi za uhifadhi katika moja ya mandhari muhimu zaidi ya bioanuai nchini.

‎Akizungumza wakati wa hafla hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali wa TFS, Dk Zainabu Bungwa ‎akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za misitu Tanzania, Profesa Dos Santos Silayo amesema kuwa magari hayo yatatumika kikamilifu katika kuongeza ufanisi wa doria na shughuli za ulinzi wa misitu, huku akisisitiza kuwa sheria za uhifadhi zipo na zinafanya kazi.

‎”Magari haya ni muhimu si tu kwa TFS, bali pia kwa jamii zinazozunguka maeneo ya misitu na kwa taifa kwa ujumla, kwani yatasaidia kulinda bioanuai na kupunguza uharibifu wa misitu,” amesema Dk Zainabu.

‎Aidha TFS imeeleza kuwa katika kipindi cha mvua baadhi ya maeneo ya misitu huwa hayafikiki kabisa kutokana na changamoto za miundombinu, lakini magari hayo mapya yatawapa uwezo wa kufika hata maeneo hatarishi zaidi.

‎Pia TFS imetoa maombi kwa ULS kuongeza maeneo ya Rungwe na Kalambo katika miradi ya uhifadhi kutokana na umuhimu wake kwa ikolojia na changamoto ya uvamizi wa misitu.

‎Magari hayo mawili yenye thamani ya Sh323.09 milioni yameelezwa kuwa ni msaada mkubwa katika kupanua wigo wa shughuli za ufuatiliaji, tathmini na kujifunza katika maeneo ya misitu.

Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali wa TFS, Dk Zainabu  Bungwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Southern Tanzania Elephant Program (STEP), Frank Lihwa wakiwa nje ya ofisi ya STEP iliyopo Wilolesi halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakisaini makabidhiano ya magari mawili mapya ya Toyota Land Cruiser. Picha na Christina Thobias



‎Naye Mkurugenzi Mtendaji wa STEP, Frank Lihwa amesema kuwa ushirikiano kati ya TFS na STEP umeanza miaka 10 iliyopita na umezaa matunda makubwa katika kusimamia misitu ya udzungwa.

‎ ‎Katibu wa Sekretarieti ya ULS, Trevor Jones amesema TFS ni mshirika muhimu katika uhifadhi wa misitu ya Udzungwa na Kilombero na amepongeza ushirikiano mzuri uliodumu kwa muda mrefu.

‎Pia Jones ametoa wito kwa TFS kuhakikisha magari hayo yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa misitu.

‎ Mhifadhi wa Misitu Asili ya Udzungwa, Michael Urio amepongeza hatua ya kukabidhiwa magari hayo akisema kuwa jiografia ya Udzungwa ni changamoto na kwa muda mrefu wamekuwa na gari moja pekee kwa eneo kubwa.