Tuwasomeshe kisha tuwaajiri wenye ulemavu

Dar es Salaam. Katika jamii yoyote inayotaka kuwa ya haki, usawa na maendeleo ya kweli, hakuna kundi linalopaswa kuachwa nyuma.

Moja ya makundi ambayo mara nyingi husahaulika au kupuuzwa ni watu wenye ulemavu. Hili ni kundi muhimu ambalo, kama litapewa nafasi sawa katika elimu na ajira, linaweza kuwa nguzo imara ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Hivyo basi, tunapaswa kusimama kwa kauli moja tukisema: ‘’Tuwasomeshe na kuwaajiri wenye ulemavu.’

Elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto na mtu mzima, bila kujali hali yake ya kimwili au kiakili. Hata hivyo, kwa miaka mingi, watu wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi katika kupata elimu bora. Wengine hukatishwa tamaa mapema kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki kama madarasa yanayoweza kufikika kwa walemavu wa viungo, nyenzo za kielimu kama maandishi ya nukta nundu kwa wasioona, na walimu wenye uelewa kuhusu mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.

 Hili limesababisha kundi kubwa la watu wenye ulemavu kubaki bila elimu ya msingi, ya kati au ya juu, hali inayozuia mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Ni muhimu jamii na Serikali kwa ujumla kuitazama upya dhana ya elimu kwa watu wenye ulemavu. Hatua ya kwanza ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye ulemavu wanapatiwa fursa sawa ya kujiunga na shule, iwe ni za kawaida au maalum, kwa kutumia mfumo wa elimu jumuishi.

Shule zinapaswa kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi wa aina zote, zikiwa na miundombinu, vifaa na walimu waliopata mafunzo ya kushughulikia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.

Kwa kufanya hivyo, tunakuwa tumewaweka katika nafasi nzuri ya kutumia vipaji vyao, kujiamini na hatimaye kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

Lakini elimu pekee haitoshi. Ni kweli kuwa kuwapa watu wenye ulemavu elimu ni hatua muhimu ya kwanza, lakini haitakuwa na maana yoyote ikiwa baada ya kumaliza masomo yao hawapati ajira. Katika hali ya sasa, changamoto ya ajira kwa watu wenye ulemavu ni kubwa kuliko kwa watu wasio na ulemavu.

Mara nyingi, waajiri hutoa kisingizio cha kutokuwa na mazingira rafiki kwa walemavu, au wanaamini kimakosa kuwa watu hawa hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi.

Matokeo yake ni kuwa watu wengi wenye ulemavu, hata wale wenye elimu ya juu, hukosa fursa za ajira na kuishia kuwa tegemezi kwa familia au jamii.

Ni wakati sasa kwa Serikali na sekta binafsi kubadili mtazamo na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanaajiriwa kwa haki na kwa misingi ya uwezo wao.

Taifa linahitaji sera mahususi na miongozo ya wazi inayolazimisha mashirika ya umma na ya binafsi kutenga asilimia fulani ya nafasi za ajira kwa watu wenye ulemavu.

Sera hii isijikite tu kwenye kutoa nafasi, bali ihusishe pia kuhakikisha mazingira ya kazi ni jumuishi ikiwa ni pamoja na majengo yanayofikika, vifaa vya kazi vinavyokidhi mahitaji ya kila mmoja, na mafunzo kwa waajiri kuhusu namna ya kuwajumuisha walemavu kazini.

Aidha, kuna haja ya kuwa na takwimu sahihi kuhusu watu wenye ulemavu waliomaliza elimu katika ngazi mbalimbali, ili kusaidia kupanga ajira zao kwa ufanisi.

Hii itasaidia pia kufuatilia utekelezaji wa sera za ajira kwa watu wenye ulemavu, na kuhakikisha kuwa hazibaki kwenye makaratasi pekee bali zinaakisi hali halisi kazini.

Kwa kufanya hivyo, tunawapa watu hawa si tu hadhi ya binadamu bali pia nafasi ya kuchangia kwa namna yao katika maendeleo ya Taifa.

Sekta binafsi nayo inapaswa kuchukua jukumu la kuajiri watu wenye ulemavu kwa kutambua kuwa wao pia ni sehemu ya wateja, wafanyakazi, na wabunifu wa suluhisho mbalimbali za biashara. Kampuni nyingi duniani zimeonyesha kuwa kuwaajiri watu wenye ulemavu huongeza ubunifu, huruma kazini, na hata tija ya jumla.

Kwa mfano, watu wengi wenye ulemavu wamekuwa wakionyesha ufanisi mkubwa, uadilifu, na kujituma kazini,  mambo ambayo ni tunu kwa kila taasisi.

Hii inapaswa kuwa somo kwa mashirika na taasisi nchini Tanzania kuona kuwa kuajiri watu wenye ulemavu si hisani, bali ni uwekezaji wa busara.

Zaidi ya hilo, Serikali inapaswa kuanzisha au kuimarisha mifumo ya motisha kwa mashirika au kampuni zinazojitolea kwa dhati kuajiri watu wenye ulemavu.

Hii inaweza kuwa katika mfumo wa punguzo la kodi, kutambuliwa rasmi kupitia tuzo za kitaifa, au hata fursa za zabuni na mikataba ya kipaumbele kwa kampuni zenye ajira jumuishi. Kwa njia hii, sera zitakuwa na meno, na sio maneno tu.

Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na mtekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu, ina wajibu wa kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu na ajira kwa watu wenye ulemavu inalindwa na kutekelezwa ipasavyo.

 Hii ni pamoja na kutunga sheria rafiki, kutoa elimu kwa jamii kuhusu uwezo wa watu wenye ulemavu, na kuondoa dhana potofu zinazowadhalilisha au kuwabagua.

Hatuwezi kuwa na taifa lenye usawa, haki na maendeleo ya kweli bila kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika kila hatua ya maendeleo. Tuwasomeshe ili wajiandae kwa maisha ya kujitegemea na kuchangia kwa weledi, lakini pia tuwape ajira ili wawe sehemu hai ya jamii yetu. Elimu bila ajira ni sawa na kujenga daraja lisiloelekea popote.

Ni wakati wa kuwa na sera na mifumo madhubuti ya kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawabaki nyuma tena. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumedhihirisha kwa vitendo kuwa kweli Tanzania ni nchi ya wote.