Ushirikiano Tanzania, Qatar kufungua fursa za ajira kwa mabaharia

London. Mabaharia watanufaika na maslahi bora na fursa zaidi za kazi kwenye masoko yenye ushindani ushindani wa juu na kuchochea uhamasishaji wa ujuzi  na utaalamu wa kimataifa bada ya kusainiwa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Qatar ya kutambua vyeti vya mabaharia.

Makubaliano hayo yamesainiwa jana, Novemba 24, 2025, jijini London. Kwa upande wa Tanzania, yamesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Mohamed Malick Salum, huku Mhandisi Abdulaziz Abdullah Al-Sulait, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi wa Qatar, akisaini kwa niaba ya nchi yake.

Hafla hiyo imefanyika pembezoni mwa mkutano wa 34 wa Baraza Kuu la Shirika la Bahari Duniani na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya bahari.

Katika makubaliano hayo, mabaharia wataweza kufanya kazi katika majukwaa yenye viwango vya juu vya teknolojia na usalama pamoja na kuimarisha uwezo wa Tanzania katika utoaji wa mafunzo ya ubaharia, kwani vyuo na vyeti vyake vitakuwa na uhalali mpana zaidi kimataifa.

“Tanzania inawakaribisha Qatar kuja kuthibitisha utekelezaji wetu wa matakwa ya STCW, na pia tunajitolea kufanya ziara za tathmini ya pande mbili. Ushirikiano huu utaimarisha uaminifu wa pamoja na ulinganifu na viwango bora vya kimataifa,” amesema Salum alipozungumza katika hafla hiyo.

Kwa upande wake, Mhandisi Al-Sulait amesema, “Qatar inatazamia ushirikiano huu kuwa wa muda mrefu. Ushirikiano huu ni zaidi ya vyeti pekee, ni mwanzo wa uhusiano mpana zaidi katika kujenga uwezo, kuboresha usalama, na kuendeleza sekta ya bahari.”

Pia inaelezwa kupitia makubaliano hayo, pande zote mbili zinatarajia kuboresha viwango vya umahiri, usalama na ubora katika taaluma ya ubaharia, sambamba na kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Qatar.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ajira kwa mabaharia wa Kitanzania katika meli zilizosajiliwa au kuendeshwa na kampuni za Qatar, kwani hawatalazimika kupitia upya taratibu za uthibitishaji wa vyeti pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji baharini kati ya nchi hizo mbili.