Wafungwa watatu raia wa China watinga mahakamani kutoa ushahidi kesi ya kughushi msamaha wa Rais

Dar es Salaam. Mashahidi watatu raia wa China ambao pia ni wafungwa wanaotumikia vifungo gerezani wametinga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutoa ushahidi katika kesi ya kughushi msamaha wa Rais kwa wafungwa inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili.

Mkama na wenzake, Sibuti Nyabuya, aliyekuwa ofisa Tehama wa Gereza la Ukonga na mfanyabiashara, Joseph Mpangala, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 25517 ya mwaka 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Mashahidi hao ni Song Lei, Xiu Fu Jie na Haung Quin, ambao wamepelekwa mahakamani hapo leo Jumanne Novemba 25, 2025, wakitokea gerezani.

Hata hivyo, licha ya mashahidi kuwepo mahakamani hapo, kesi hiyo imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa upande wa mashtaka kutokana mmoja wa mawakili wa utetezi Amini Mshana kuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu.

Awali, kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa Serikali Mwandamizi Daisy Makakala aliiambia Mahakama kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji na tayari upande wa mashtaka wana mashahidi watatu.

Makakala aliwataja mashahidi hao kuwa ni Song Lei, Xiu Fu Jie na Haung Quin, ambao ni wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani.

Baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Henry Munisi anayemtetea mshtakiwa wa kwanza ( Mkama) na mshtakiwa wa tatu (Mpangala) alidai kuwa wakili mwenzake wa utetezi Amini Mshana anayemtetea mshtakiwa wa pili (Nyabuya) yupo Mahakama Kuu kwenye kesi ya Ardhi namba 25692 ya mwaka 2025 kati ya Sophia Sagawe dhidi ya Mohamed Matendo, ambayo inasikilizwa mbele ya Jaji Steven Magoiga.

“Nimejaribu kumpigia simu mchana huu bila mafanikio, hivyo kutokana na hali hiyo naomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji,” alidai Wakili Munisi.

Munisi baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili Makakala aliomba kesi hiyo kama inaahirisha basi ipangiwe tarehe ya karibu kwa kuwa upande wa Jamhuri leo walikuwa na mashahidi.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 2025 itakapoendelea na usikilizwaji.

Pia hakimu Mhini alielekeza mawakili wa utetezi siku hiyo wawepo mahakamani na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Katika kesi hiyo, wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Desemba Mosi, 2022 hadi Januari 30, 2023 jijini Dar es Salaam,
Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu raia wa China, wenye namba 585/2019 Song Lei; namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliofungwa katika kesi tofauti kwa makosa ya nyara za Serikali.

Inadaiwa kuwa Machi 18, 2016 wafungwa watatu wenye asili ya China, ambao ni mfungwa mwenye namba 585/2019 Song Lei; namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliohukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo katika gereza la Ukonga.

Wafungwa hao walihukumiwa vifungo tofauti kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali na wote walikuwa hawajuani.

Hata hivyo, Desemba 21, 2022, Mkama kwa wakati huo alikuwa Mkuu wa Gereza hilo na Nyabuya ambaye alikuwa ofisa Tehama wa gereza hilo kwa kipindi hicho , walitengeneza nyaraka ya kughushi yenye kichwa cha habari, ‘Nyongeza ya msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru’.

Nyaraka hiyo ambayo ni barua ya Desemba 21,2022, iliyosainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Raisi.

Tayari shahidi watano wa upande wa mashtaka ameshatoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa mashahidi hao ni aliyekuwa Mkuu wa Huduma kwa wafungwa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza nchini, Boid Mwambingu, ambaye aliieleza Mahakama namna alivyotumwa kwenda kufanya uchunguzi wa malalamiko ya wafungwa watatu katika gereza la Ukonga na kubaini barua ya msamaha wa rais kwa wafungwa hao, aliyoonyeshwa na Mkama ilikuwa haina saini ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kubaini kuwa ilikuwa imeghushiwa.