Dar es Salaam. Katika kudhibiti matumizi ya akaunti feki pamoja na wale wanaotoa taarifa za uongo mtandao wa X (zamani Twitter), umekuja na kipengele kipya kitakachoonyesha mahali alipo mtumiaji wa akaunti husika.
Kupitia kipengele hicho cha ‘About this Account’ inatonesha nchi ambayo akaunti imefunguliwa, mtumiaji amebadili jina la akaunti mara ngapi, mtumiaji anatumia akaunti husika kupitia simu ya Android au Iphone.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, lengo ni moja: kuwapa watumiaji muktadha wa kutosha ili kutambua kama akaunti ni ya kweli au inajaribu kusambaza taarifa potofu. Kwa mfano, akaunti inayodai kuwa Marekani lakini taarifa zinaonyesha imekuwa ikitumia mtandao kutoka nchi nyingine inaweza kuzua maswali juu ya uhalisia wake.
Taarifa hizo sasa zinapatikana juu ya ukurasa wa wasifu (profile), chini ya jina la mtumiaji. Ukibonyeza sehemu ya “Joined,” utapelekwa kwenye ukurasa unaoitwa About this account.
Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye The New York Times, BBC na mitandao ya teknolojia kipengele hicho, kimetangazwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Bidhaa wa X, Nikita Bier.
Bier amesema hatua hii ni kwanza muhimu ya kulinda uadilifu wa jukwaa hilo la mazungumzo duniani, na kuongeza kuwa wataendelea kuboresha mbinu za uthibitishaji wa maudhui kwenye mtandao.
Aidha, kwa mujibu wa Bier, watumiaji waliopo kwenye nchi zenye ukomo wa uhuru wa kujieleza wanaweza kuchagua kuonyesha tu eneo (mkoa) badala ya nchi ili kujikinga dhidi ya madhara.
Aidha, taarifa za eneo zitasasishwa mara kwa mara (updates) kwa kuchelewa ili kulinda faragha.
Hata hivyo, X inayomilikiwa na bilionea kutoka nchini Marekani Elon Musk imekuwa ikipambana kwa muda mrefu na akaunti bandia na roboti (bots) ambazo zimekuwa zikitumika kusambaza taarifa potofu kuhusu uchaguzi, COVID-19 na nadharia za njama (conspiracy)
Kwa miaka mingi, watafiti wameonya kuwa bots zimewahi kutumiwa kuchochea migawanyiko katika chaguzi ndani na nje ya Marekani.
Tangu Elon Musk anunue jukwaa hilo mwaka 2022, kumekuwepo ongezeko la kauli za chuki, ikiwemo zile za kibaguzi na zinazokashifu makundi mbalimbali.
Hata hivyo, kufuatilia hatua hiyo mjadala umeibuka mitandaoni kuhusu faragha ya watumiaji wa mtandao huo. Hata hivyo, TechCrunch imeripoti ingawa watumiaji wengi wanaweza kuona taarifa zao wenyewe, bado hawajapewa uwezo wa kuona taarifa hizo kwa akaunti nyingine.