Dodoma. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amezifuta leseni 73 za uchimbaji na utafiti, akisisitiza kuwa kazi hiyo itakuwa endelevu kwani hakuna leseni inayotolewa kama mapambo.
Leseni zilizofutwa zinajumuisha 44 za utafiti na 29 za wachimbaji wa kati.
Leseni hizo ni miongoni mwa 205 ambazo wamiliki wake waliandikiwa hati za makosa na kutakiwa kujibu kwa kuyarekebisha na kuanza uendelezaji. Wengine hawakujibu hali inayoonyesha wameshindwa.
Akizungumza leo Novemba 25, 2025 katika kikao cha waandishi wa habari na watumishi wa Tume ya Madini Tanzania jijini Dodoma, Mavunde amesema mkakati wa kufuta leseni zinazokiuka masharti utaendelea kila wakati.
Amesema haiwezekani Tanzania ikafanywa kuwa nchi ya mtego.
“Kuna watu wanakuja kuchukua leseni halafu wanahodhi maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi, hawalipi hata kodi na hawatoi ajira, huku baadhi ya leseni zikionyesha zilitolewa tangu 2013 lakini bado wanazo na hawaanzishi shughuli za uchimbaji madini ila wanajiita ni wachimbaji wakati siyo kweli, hao ndio nimeagiza wafutiwe,” amesema.
Amesema ukubwa wa eneo ambalo limefutiwa leseni kama litaunganishwa ni kilomita za mraba 3,002 sawa na ekari 742.
Mavunde ameagiza Tume ya Madini kupitia ofisi za mikoani kufanya uchunguzi na kuwafuatilia wote wanaomiliki leseni lakini hawaziendelezi ili wanyang’anywe maeneo hayo.
Amesema Serikali itayagawa maeneo hayo lakini kipaumbele kitakuwa kwa vijana wazawa ili kuwasaidia wapate maeneo ya kufanyia kazi.
Mavunde amesema halmashauri zimekoseshwa mapato kwa mujibu wa mikataba na masharti kwenye leseni ambazo zinawataka kutoa mchango kwenye mambo ya kimaendeleo.
Hata hivyo, amesema kati ya leseni zilizofutwa iwapo kuna mtu ameonewa au wizara ilipata taarifa zisizo sahihi anaweza kuwasiliana na ofisi ili kujiridhisha iwapo kulikuwa na maendelezo kwenye mgodi kabla ya leseni kufutwa ili arejeshewe.
Kwa waombaji amewataka kutumia anuani sahihi zinazowezesha wapatikane kwa urahisi, kwani baadhi yao huandika barua za maombi ya leseni lakini wanatumia anuani za halmashauri.
Hali hiyo amesema husababisha kunakosekana ukaribu wa kushauri na kushauriana.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba, amesema wako tayari kwa utekelezaji wa maagizo wanayopewa, lengo likiwa kusimamia na kuhakikisha wizara hiyo inakuwa miongoni mwa za kupigiwa mfano katika mafanikio.
Mchimbaji mdogo wa madini wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma, Saul Mwita amesema uamuzi wa kufuta leseni unapaswa kushuka zaidi ngazi ya chini, kwani wapo wachimbaji wadogo wasioendeleza maeneo.
Mwita amedai baadhi ya leseni zimetolewa kwa uchimbaji mdogo lakini uhalisia ni wachimbaji wakubwa ambao wanazuia maeneo.
Amesema ni muhimu kuwa na kipaumbele cha uchunguzi na ufuatiliaji.
