YANGA baada ya kutua jijini Algiers leo mchana Novemba 25, 2025, imekuwa na safari ya umbali wa takribani kilometa 100 kwa barabara kwenda mji wa Tizi Ouzou ambako ndiko itacheza mechi yao ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wake, JS Kabylie, lakini kuna kufuru ameifanya tajiri wao, Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ ambayo itakuwa ni kama kulipa kisasi, pia kutegua mitego ya wenyeji wao.
Iko hivi; Yanga ilishamalizana na hoteli ya Le Relais Vert ambayo timu hiyo itakaa hapo kuanzia leo jioni mpaka Jumamosi mchana Novemba 29, 2025 itakapoondoka kurejea Tanzania baada ya kumaliza mechi itakayochezwa Ijumaa Novemba 28, 2025.
Klabu ya mwisho kuitumia hoteli hiyo na ikaondoka na pointi tatu ilikuwa Wydad Athletic mwaka 2023 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo JS Kabylie ililala nyumbani kwa mabao 3-0 lakini kwa timu za taifa imetumiwa na mataifa ya Senegal na Uganda ambazo zote zilipokea vipigo mbele ya Algeria.
Alichofanya tajiri huyo wa Yanga ni kwamba, kunzia kesho Jumatano Novemba 26, 2025, hoteli hiyo haitatumiwa na wageni wengine na itabaki kuwa chini ya Yanga mpaka Jumamosi Novemba 29, 2025 watakapoondoka nchini humo.
Yanga imelazimika kutumia akili hiyo ikihofia hasira za JS Kabylie ambayo imetoka kupoteza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Al Ahly ikipigwa 4-1.
Hesabu hizo za GSM zimechangiwa pia na vurugu ambazo Yanga ilifanyiwa kwenye mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika usiku wa kuamkia Juni 9, 2023 ambapo baadhi ya mashabiki wa USM Alger waliingia mpaka ndani ya hoteli waliyofikia.
Kwenye vurugu hizo, afisa mmoja wa Yanga, Hafidh Saleh alilazimika kukimbizwa hospitali kufuatia kuzidiwa na mafataki yaliyopigwa hotelini hapo.
Yanga itashuka uwanjani Ijumaa wiki hii kwenye mechi ya pili ya Kundi B, itakayopigwa Hocine Aït Ahmed uliopo Tizi Ouzou katika mji wa Boukhalifa, Mkoa wa Kabylia nchini Algeria, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 50,766 waliokaa.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, gharama ya kulala usiku mmoja ndani ya hoteli hiyo yenye vyumba 29, inaanzia Dola za Marekani 47.13 ambayo ni sawa na Sh115,388 za Tanzania.
Kwa siku tatu ambazo Yanga italala hapo ikichukua vyumba vyote 29 kuanzia usiku wa kesho Jumatano Novemba 26, 2025 hadi usiku wa Ijumaa Novemba 28, 2025 kabla ya kuondoka Jumamosi mchana Novemba 29, 2025, itakuwa imetumia takribani Sh10 milioni za Tanzania.
Hoteli hiyo ina huduma mbalimbali ikiwamo gym, bwawa la kuogelea na sehemu kubwa ya kupumzika, bila kusahau eneo la kufanyia mikutano ambalo litawafanya wachezaji, viongozi na benchi la ufundi la Yanga kupanga mikakati yao kwa utulivu kwani hakutakuwa na mwingiliano wa wateja wengine hotelini hapo kwa muda wa siku hizo tatu zaidi ya wahudumu pekee.
Mbali na hilo, pia Yanga katika msafara wake, imeenda na wapishi wawili, ambao watakuwa na kazi kubwa ya kusimamia masuala ya chakula kwa timu hiyo, huku pia ikibeba maji yanayozalishwa na kampuni ya bosi wao inayoyatumia inapokuwa hapa nchini katika mechi na mazoezi.