Afrika, Ulaya kuimarisha uchumi, wagusia kuheshimu utawala wa sheria

Luanda. Viongozi kutoka Afrika na Ulaya waliokutana katika mji mkuu wa Angola, Luanda, kuanzia juzi Jumatatu, wamekubaliana kuimarisha biashara na kukabiliana na wimbi la uhamiaji haramu huku mkutano huo ukigusia kuheshimu utawala wa sheria kwa kuwa pasipo kufanya hivyo, kinachotokea ni kuwapo machafuko.

Wakisherehekea miaka 25 ya mahusiano kati ya AU na EU, mazungumzo ya siku mbili yameshuhudiwa Umoja wa Ulaya ukiahidi kusaidia mataifa ya Afrika kukuza, kuendeleza viwanda na kupanua wigo kwa bidhaa kutoka Afrika ili kuziuza nje.

Katika mazungumzo hayo walifungua milango kwenye kutekeleza Mpango wa Uwekezaji wa Global Gateway Afrika–Ulaya, unaolenga kuhamasisha fedha za umma na binafsi kwa ajili ya miundombinu, nishati na muunganisho wa kidijitali.

Mpango huo utakaogharimu Euro 150 bilioni unakusudiwa kuimarisha ukuaji na kuharakisha mabadiliko ya tabianchi na ya kiteknolojia.

Tamko lililotolewa mwishoni mwa mkutano huo jana Jumanne lilionyesha nia ya Ulaya kupata madini muhimu na ya Afrika kuendeleza uchumi wake.

Rais wa Baraza la Ulaya, António Costa amesema ni muhimu kupunguza tofauti za kiuchumi na kuleta  maendeleo kwa nchi hizo za Afrika.

“Ni muhimu kuwekeza katika elimu, kuunga mkono ujasiriamali, kuhamasisha ubunifu wa vijana wa Afrika na kuhakikisha kuwa minyororo ya thamani inazalisha utajiri,” amesema.

Ulaya iliahidiwa msaada katika kukabili uhamiaji haramu na kuboresha urejeshaji wa waomba hifadhi waliokataliwa kurejea katika nchi zao za asili suala ambalo mara nyingi hulalamikiwa katika nchi nyingi 27 za EU.

Mkutano huo ulilenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kiusalama kati ya mabara hayo mawili, huku wajumbe wakisisitiza umuhimu wa kufanikisha amani kupitia mfumo wa kimataifa unaoheshimu sheria.

“Hakuna mbadala wa utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria, kwa sababu mbadala wake ni machafuko na tunahitaji kuyazuia,” Costa amesema.

Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika,  João Lourenço amesema viongozi wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali.

“Tumeafikiana kuhusu haja ya kupanua ushirikiano katika masuala ya amani na usalama, na kuimarisha hatua za pamoja dhidi ya ugaidi na misimamo mikali ya vurugu,” amesema.

Ameongeza kuwa wataendelea kushirikiana kuimarisha hatua za kukabili mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ufadhili kwa ajili ya uhimilivu na ustahimilivu, pamoja na kuunga mkono mabadiliko ya nishati barani Afrika.

Pia, washirika wameazimia wataimarisha uhusiano wa kiuchumi kwa ahadi za kukuza uwekezaji katika miundombinu endelevu, uzalishaji viwandani na kilimo na kupanua fursa za uhamaji wa watu kati ya mabara hayo.

Ulaya ndiyo chanzo kikubwa zaidi cha uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika. Hata hivyo, wachambuzi wanapendekeza kuwa uhusiano kati ya AU na EU unahitaji kuboreshwa ikiwa Ulaya inataka kuendelea kuwa mshirika mkuu wa bara hilo.