Daktari aliyeweka historia ya upandikizaji moyo afariki dunia

London. Daktari bingwa aliyefanikisha upandikizaji wa kwanza wa moyo uliodumu nchini Uingereza, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93.

Sir Terence English, alimfanyia upasuaji huo Keith Castle (52), aliyekuwa na uraibu wa uvutaji sigara, Agosti 1979.

Castle, shabiki wa timu ya soka ya Fulham, ambaye pia alipenda bia, aliendelea kuishi kwa takribani miaka sita zaidi. Shughuli zake za kuchangisha fedha zilipata umaarufu zaidi kwenye vyombo vya habari.

Kabla ya mafanikio ya upasuaji huo, hakuna mgonjwa wa moyo aliyeishi Uingereza kwa miezi kadhaa baada ya kupandikizwa moyo.

Sasa, zaidi ya miaka 45 baadaye, takribani wagonjwa 9,000 wamepandikizwa moyo nchini humo.

Sir Terence, aliyefariki dunia Jumapili Novemba 23, 2025 alijulikana pia kwa mapenzi yake ya magari. Katika maisha ya kustaafu alimiliki Rolls-Royces tatu na Mercedes 250S ya mwaka 1965.

Baadaye alihudumu kama rais wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji cha Uingereza, pia Mkuu wa Chuo cha St Catharine’s, Cambridge, kati ya mwaka 1993 na 2000.

Alikuwa na watoto wanne na mke wake wa kwanza Ann, lakini baadaye aliungana tena na mpenzi wake wa zamani Judith Milne, waliyekutana wakiwa madaktari wanafunzi mwishoni mwa miaka ya 1960. Wawili hao walifunga ndoa mwaka 2002.

Sir Terence aliyezaliwa mwaka 1932 katika Jiji la Pietermaritzburg, alisoma shule ya bweni Afrika Kusini.

Baba yake alikuwa mhandisi wa migodi na aliwahi kuwa rubani wakati wa Vita vya Kwanza ya Dunia, ambako alinusurika baada ya kupigwa risasi na kuathiriwa na gesi.

Lakini alifariki dunia kutokana na silikosisi (ugonjwa wa mapafu unaowakumba wachimbaji). Wakati huo Sir Terence alikuwa mtoto mchanga.

Baada ya shule, aliamua kuingia kwenye kazi ya uchimbaji madini akirithi mikoba ya baba yake, licha ya upinzani wa mama yake.

Alianza kazi kama mchimbaji almasi nchini Zimbabwe (wakati huo Rhodesia). Hata hivyo, alibadili mawazo akajiunga na masomo ya udaktari akahitimu mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 30.

Mwaka uliofuata alianza kazi chini ya daktari bingwa wa upasuaji wa moyo, Sir Russell Brock, katika Hospitali ya Guy’s.

Sir Terence baadaye aliteuliwa kuwa daktari bingwa wa upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Papworth, jirani na Cambridge, ambako aliandika historia.

Lakini ndoto yake ya kufanya upandikizaji wa kwanza wa moyo uliodumu Uingereza ilikabiliwa na upinzani mkali, hata kutoka kwa wataalamu wenzake.

Mbali ya maswali ya kidini, kulikuwa na tatizo la kiwango duni cha uhai kwa wagonjwa wa awali.

Mgonjwa wa kwanza mwaka 1968 aliishi siku 45 pekee baada ya upandikizaji. Aliyefuata aliishi siku mbili tu. Jaribio lingine lilifanikiwa zaidi na mgonjwa aliishi siku 107.

Baada ya serikali kukataa kumpa ufadhili wa kufanya jaribio jingine, alitafuta msaada kutoka mamlaka za Cambridge na kuendelea bila kusubiri serikali.

Hata hivyo, mgonjwa wake wa kwanza Charles McHugh, baba mwenye miaka 44 aliishi siku 17 baada ya upasuaji Januari, 1979.

Sir Terence alikabiliwa na ukosoaji mkali na hata kushutumiwa kwamba, amechelewesha maendeleo ya fani hiyo kwa miaka mitano.

Lakini baadaye mwaka huo ndipo Castle alipojitokeza.

Akizungumza mwaka 2004, Sir Terence alisema: Kwa kuangalia kwenye makaratasi, Keith Castle hakuwa mgonjwa ‘bora’ kwa kupandikizwa moyo. Alikuwa na ugonjwa mbaya wa mishipa ya moyo, alikuwa mvutaji sigara aliyetopea na umri wake wa miaka 52 ulikuwa juu ya kiwango chetu (cha miaka 15 hadi 50).

Lakini nilipokutana naye, nilijua ataweza. Mwili wake ulikuwa umedhoofu, lakini macho yake na ucheshi wake vilinionyesha uthabiti wa tabia ulioweza kumvusha,” alisema.

Castle alipata moyo wa kijana wa miaka 21 aitwaye Duncan Prestt, mchezaji wa gofu kutoka Cambridgeshire aliyefariki dunia kwa ajali ya gari, huko Ely.

Baada ya moyo wa mfadhili huyo kupatikana, Sir Terence alimfanyia Castle upasuaji huko Papworth.

Castle alikuwa katika hali mbaya; alishawahi kupata mshtuko wa moyo mwaka 1976 na kulazimika kuacha kazi. Hadi alipofanyiwa upasuaji, alikuwa ameshapata mishtuko kadhaa ya moyo.

Mchakato mzima wa ulidumu saa tano na nusu.

“Keith alizinduka haraka. Alijihisi vizuri na akaanza kutupa vichekesho kama kawaida yake,” Sir Terence alisema.

Baada ya saa chache, Castle alikuwa mzima kiasi cha kunywa glasi ya maziwa na kuuliza: Fulham wamepata matokeo gani?”

Akiungwa mkono na mkewe Doreen na familia, Castle alianza kazi ya kuchangisha fedha, ikiwa ni pamoja na kukusanya Pauni 70,000 (zaidi ya Sh220 milioni) kwa ajili ya Papworth.

Hata hivyo, Castle hakuwahi kuacha kuvuta sigara. Ugonjwa wa moyo ulimrudia na alifariki akiwa nyumbani kwake kwenye bustani mwaka 1985 akiwa na miaka 58.