Danadana uzinduzi Soko la Kariakoo zaendelea

Dar es Salaam. Wakati wafanyabiashara wakilalamikia danadana za uzinduzi wa Soko la Kariakoo, uongozi umekuja na ahadi mpya ukisema sasa litazinduliwa katikati ya Desemba, 2025.

Mkwamo wa uzinduzi wa soko hilo ulianza tangu ukarabati ulipokamilika Mei, 2024 ukigharimu Sh28 bilioni.

Ukarabati ulifanyika baada ya soko hilo kuungua moto mwaka 2021 na kuteketeza mali za wafanyabiashara.

Wakizungumza na Mwananchi leo Novemba 26, 2025 wafanyabiashara wameeleza mazingira magumu wanayokabiliana nayo wakisubiri soko kufunguliwa.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, maeneo wanayotumia kufanya shughuli zao ni madogo, hayana mpangilio na yamekuwa chanzo cha adha kwa makundi maalumu kama wajawazito, watoto na wazee wanaohitaji huduma kwa haraka na salama.

“Tunafanya kazi chini ya jua kali na kwenye vumbi, muda mwingi tunahangaika kuliko kufanya biashara. Hatuna usalama, magari yanapita karibu sana na maeneo tunapokaa,” amesema Omary Ali.

Amesema ufunguzi wa soko hilo ni muhimu ili kurejesha utulivu, usalama na mazingira bora ya biashara kama ilivyokuwa awali.

Mfanyabiashara huyo amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika, akihoji ni nini kinachosababisha lisifunguliwe.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Tasiana Selestin, anayeuza nyanya, ambaye aliwahi kufanya kazi ndani ya soko hilo kabla ya kupisha ukarabati.

Anaeleza hali ilivyo sasa ni changamoto kwa afya na usalama wao.

“Changamoto tunazopitia hapa ni nyingi. Hatuko salama kiafya, kuna vurugu na wakati mwingine watu wanagongwa kwa kuwa tupo barabarani. Ni vumbi kila kona,” amesema.

Amesema wengi wao wamepangiwa vizimba, wamepewa namba za kulipia kodi na ujenzi wa soko umekamilika, hivyo kuchelewa kufunguliwa kwa soko hilo kunawafanya waendelee kupata hasara na kuhatarisha maisha yao.

“Cha kushangaza ni kwamba, soko limekamilika lakini halijafunguliwa. Hapa nje tunateseka kuna mvua, jua, vurugu za magari. Tunaomba lifunguliwe ili tufanye kazi sehemu salama,” amesema.

Kwa upande wake, Rashid Juma, amesema maeneo wanayotumia sasa ni madogo na hatarishi, hasa kutokana na msongamano wa magari na watembea kwa miguu.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko Kariakoo, Hawa Ghasia amesema lengo la bodi ni kuhakikisha mkandarasi anakamilisha kila sehemu muhimu kabla ya kukabidhi rasmi.

Amesema kwa mujibu wa ahadi alizotoa, ukarabati unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 15, mwaka huu.

“Shughuli kubwa ni kwamba milango bado haijafika. Watu wakianza kufanya kazi bila kuweka milango ni changamoto, lakini tunaona ni afadhali uchelewe ufike, kuliko kuanza nusunusu. Wafanyabiashara wameshavumilia sana, tunaomba waendelee kuvumilia,” amesema.

Ghasia amesema uwekaji wa milango ni muhimu kwa usalama, ikiwa ni pamoja na kupunguza athari endapo kutatokea ajali kama moto, kwani bila milango hiyo ni vigumu kuzuia au kuhamia upande mwingine wa soko kwa urahisi.

Amewataka wafanyabiashara kuwa na subira wakati ukarabati na ukamilishaji wa baadhi ya miundombinu ukiendelea.

Ahadi za ufunguzi zilianza Julai 5, 2024 pale Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Masoko Kariakoo, Hawa Ghasia alipoahidi litaanza kutumika Agosti, 2024.

Akiwa ziarani sokoni hapo kujionea maendeleo ya ujenzi, alitaka wafanyabiashara ambao hawaoni majina yao katika orodha ya watakaorudishwa wakasikilizwe.

Kauli hiyo iliibua mgogoro uliosababisha baadhi ya wafanyabiashara kwenda ofisi Ndogo za CCM Lumumba, kulalamika ikaundwa kamati kushughulikia malalamiko yao.

Septemba 4, 2024 kamati hiyo iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ilikabidhi ripoti na suala la majina ya wafanyabiashara likashughulikiwa.

Kwa mara nyingine Ghasia aliahidi soko lingeanza kutumika Februari, 2025 baada ya kukamilisha kuwapanga wafanyabiashara, lakini hilo halikutimia.

Mbali na ahadi hizo, Aprili 4, 2025 Ghasia akimkabidhi ofisi meneja mpya wa shirika, Ashraph Yusufu Abdulkarim aliahidi soko lingefunguliwa mwezi huo (Aprili), nayo haikutimia.

Ahadi ya mwisho kuhusu ufunguzi wa soko hilo ilitolewa Mei 28, 2025 na Chalamila alipozungumzia maendeleo ya soko hilo.

Alisema tayari soko limeshakamilika, kinachofuata ni maandalizi ya kulifungua ingawa hakuweka wazi tarehe rasmi.

Akizungumza na Mwananchi Agosti 25, 2025, Chalamila aliahidi soko lingefunguliwa kabla ya Septemba 15, mwaka huu.

Alieleza wafanyabiashara tayari wameshaonyeshwa maeneo yao. Hata hivyo, mpaka sasa halijafunguliwa.

Kwa wakati huo, Chalamila alisema ucheleweshwaji umetokana na mkandarasi aliyekuwa akijenga soko hilo, kwamba hakuwa amekamilishiwa malipo ya shughuli aliyofanya.

Alisema walishamlipa na muda wowote wangefungua soko hilo, ahadi ambayo haijatimizwa.