Dodoma. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeagizwa kuwa makini katika kupanga ratiba za ukarabati wa miundombinu yake, kwa kuhakikisha kazi hizo zinafanyika nyakati ambazo hazihusiani moja kwa moja na uzalishaji wa umeme.
Wito huo umetolewa leo, Jumatano Novemba 26, 2025, na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, alipotembelea Kituo cha uzalishaji umeme Mtera kwa lengo la kukagua miundombinu ya uzalishaji.
Makamba amesema kwamba mara nyingine miundombinu ya Tanesco inapohitaji kufanyiwa ukarabati, si lazima kuzima umeme katika kipindi ambacho uzalishaji uko juu.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia muda ambao matumizi ya umeme katika uzalishaji ni madogo, ili kuepusha usumbufu kwa watumiaji na kuhakikisha uzalishaji unaendelea bila kukwama.
“Katika mifumo yetu ni lazima kuwe na matengenezo ambayo yatapelekea kuzima kwa maeneo husika kwa muda, sasa naagiza kuwa ni muhimu tuangalie muda wa kuzalisha kama hakuna ulazima tusizime nyakati hizo ambazo wazalishaji wengi wanakuwa kazini,” amesema Makamba.
Naibu Waziri pia amekemea tabia ya Tanesco kuzima umeme bila kutoa taarifa kwa wateja akisema si uungwana na inapaswa wahusika kujirekebisha.
Kuhusu kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera amesema hali aliyoiona inaridhisha na kutoa matumaini kuwa hata kama mvua za masika zitachelewa bado uhakika wa kupata umeme ni mkubwa.
“Hapa niwapongeze sana wenzetu wa Nyanda za Juu Kusini katika bonde la Ihefu na maeneo mengine, wamejitahidi kutunza mazingira ndiyo maana tunapata maji ya uhakika hapa, tuendelee kulinda miundombinu na mwisho tutakuwa salama,” amesema Makamba.
Naibu Mkurugenzi wa huduma za usambazaji umeme nchini, Athanasius Nangali amesema uwezo wa kuzalisha umeme katika kituo cha Mtera ni megawati 80.
Nangali amesema mbali na huduma ambazo zimekuwa zikitolewa katika eneo hilo, lakini Serikali imeongeza nguvu kwa kujenga mitambo ya Umeme wa Vijijini (REA) ambao unahudumia wananchi wa maeneo jirani ya Wilaya za Mpwapwa, Chamwino na Iringa Vijijini.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, awali iliwalazimu wananchi kutegemea umeme unafika Dodoma mjini au Iringa na ukishapozwa ndipo ulirudishwa tena kuwahudumia, lakini sasa watapata huduma moja kwa moja kutoka Mtera.
