Mbeya Jiji yaanza kuchukua hatua kukabiliana na kipindupindu

Mbeya. Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kushirikiana na wadau wa afya wameanza mkakati wa kutokomeza magonjwa ya mlipuko ikiwamo kipindupindu, kwa kutoa elimu kwa mama lishe kuhakikisha wanazingatia usafi na huduma bora katika maeneo yao ya kazi.
Ikumbukwe Desemba mwaka jana, Jiji la Mbeya lilikuwa miongoni mwa Halmashauri tatu za Mkoa wa Mbeya kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu kilichoathiri mwenendo wa shughuli za baadhi ya wananchi ikiwamo mama lishe waliofungiwa maeneo yao ya kazi.
Kwa sasa tayari mvua zimeanza kunyesha jijini Mbeya, ambazo huchangia kutiririsha maji machafu hadi katika makazi ya watu, hali ambayo imeiamsha mapema halmashauri hiyo kuanza kuchukua hatua.
Akizungumza leo Novemba 26,2025 wakati wa kukabidhi vifaa kazi kwa mama lishe baada ya kumaliza mafunzo ya siku mbili, Ofisa Lishe wa Jiji hilo Itika Festo amesema programu hiyo inaenda kukabiliana na changamoto ya magonjwa ya mlipuko.
Amesema Halmashauri inaendelea na jitihada za kutoa elimu kupitia siku za afya na lishe kwa kuifikia pia jamii kuhusu afya na virutubisho ili kuondokana na magonjwa mengine ikiwamo udumavu.
“Hii programu itaongeza nguvu kutokomeza kipindupindu na magonjwa mengine na imekuja muda sahihi, tunachoomba kwa mama lishe na baba lishe watoe ushirikiano ili kujenga jamii imara na Taifa lenye afya bora” amesema Itika.
Elina John mkazi wa Must amesema mafunzo hayo na vifaa vya kazi walivyopewa vinaenda kuwabadilisha katika majukumu yao, kwani awali walikutana na changamoto kubwa iliyowashusha kiuchumi.

“Mbeya Jiji tulikumbwa na kipindupindu, tulipoteza wapendwa wetu, shughuli zilisimama hivyo mafunzo haya tunaenda kufanya kazi kwenye mazingira bora na kuondokana na kero iliyojitokeza” amesema Erina.
Naye Fibe John mkazi wa Inyala, amesema matarajio yao ni kufanya kazi kwa kuzingatia usafi kwa ustawi wa jamii, akieleza kuwa changamoto kubwa waliyokuwa nayo ilikuwa ni vifaa bora.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amewataka mama lishe kuwafikishia wengine elimu waliyopata.
“Tuzingatie usafi katika maeneo yetu ya kazi, tuoneshe upendo kwa wateja wetu, lakini mafunzo haya muwe mabalozi kwa wengine, niwashukuru Agra na niwakaribishe Wilaya ya Mbeya Vijijini”
“Lakini pia mama lishe ambao hawajapata mikopo, mlango uko wazi hapa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwani mwaka wa fedha 2024/25 tumetoa Sh3.5 bilioni, ambao hawakunufaika nazo njooni mpate mwongozo” amesema Itunda.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Anna Minja amesema programu hiyo imeanza mwaka huu kuwafikia mama lishe inayohusika na uboreshaji lishe, afya na usafi wa mazingira.

“Tunatarajia mabadiliko kwa wananchi wa jiji la Mbeya, ile changamoto ya magonjwa ya milipuko yanaondoka kwa kuwa elimu tumeitoa na tunaendelea kuitoa kwa mama lishe” amesema Anna.