Dar es Salaam. Kifo cha Ali Ameir Mohamed kimeacha kumbukumbu kuwa alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza wa CCM Zanzibar, alikabiliana na changamoto za kisiasa zilizojitokeza baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1995.
Pia, kifo chake kimeacha kumbukumbu kuwa akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alikabiliana na msukosuko wa mivutano ya kisiasa na kidini uliotokea katika hatua za mwanzo za mfumo wa vyama vingi nchini.
Huyo ndiye Ali Ameir Mohamed aliyezaliwa mwaka 1944 huko Donge, Mkoa wa Kaskazini B, Unguja.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 26, 2025, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amesema Ali Ameir amefariki dunia jana Novemba 25, 2025 katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Mbeto, maziko ya Ali Ameir yatafanyika kesho Novemba 27, 2025 kijijini kwao Donge.
Mbeto amesema enzi za uhai wake, Ali Ameir alikuwa jasiri wa kutetea masilahi ya chama, akitolea mfano uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kati ya wagombea— Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF na Dk. Salmin Amour.
Kwenye uchaguzi huo, Ali Ameir alidaiwa kwenda Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kulalamika kwamba tume hiyo ilishirikiana na na tume.
Malalamiko hayo yalielezwa CUF kuibia kura za CCM, wakati matokeo rasmi yakiwa hayajatangazwa kusikika na baadhi ya watu waliokuwa pale, ikiwemo waandishi wa habari.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi kuamini kuwa Maalim Seif alishinda uchaguzi huo, huku kituo kimoja cha televisheni jijini Dar es Salaam kikitangaza matokeo hayo yasiyo rasmi.
Akimzungumzia zaidi, Mbeto amesema kuwa Ali Ameir atakumbukwa kwa namna alivyoshiriki katika shughuli mbalimbali za chama, ikiwemo kushiriki ujumbe wa kamati ya maridhiano kati ya CCM na CUF.
Pia amesema kwenye nafasi yake ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alionesha ujasiri katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kisiasa na kidini kwa kuwa alishika nafasi hiyo mwanzoni mwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Ali Ameir enzi za uhai wake mara kadhaa alitoa msimamo mkali dhidi ya tabia au viongozi ndani ya CCM ambao kwa mtazamo wake, walikuwa na “mwelekeo wa kutishia misingi ya chama.”
Pia alisisitiza umuhimu wa uwazi, nidhamu na itikadi thabiti ndani ya chama, akionya dhidi ya “kubembelezwa” kwa watu walio na mienendo isiyokubalika.
Kwenye uhai wake alitoa matamko ya kuchangia mjadala wa uongozi bora, haki na uwajibikaji kwa misingi ya sifa na uwezo binafsi.
Waziri Serikali ya Muungano
Wakati Ali Ameir akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ni kipindi ambacho Tanzania ilikuwa katika hatua za mwanzo za kujenga mfumo wa vyama vingi, mabadiliko ya kiuchumi, na ongezeko la uwazi wa kisiasa.
Mabadiliko hayo yaliambatana na ongezeko la hisia, misuguano ya kijamii na changamoto za kiusalama ambazo wizara yake ililazimika kushughulikia.
Miongoni mwa changamoto ambazo Ali Ameir alikumbana nazo kwenye uongozi wake ni mauaji ya Waislamu katika msikiti wa Mwembechai, jijini Dar es Salaam.
Mauaji ya Mwembechai ni tukio lililotokea Februari 13, 1998, eneo la Mwembechai jijini Dar es Salaam ambapo vikosi vya polisi vilidaiwa viliwatupia risasi Waislamu waliokuwa wakikusanyika katika msikiti kwa ajili ya ibada.
Changamoto hiyo ilitokana na madai ya “kuikashifu dini ya ukristo,” na hivyo kusababisha mvutano kati ya baadhi ya waumini wa dini hizo mbili.
Waziri alikutana na changamoto ya madai kutoka kwa Waislamu wakitaka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi ili kubaini waliohusika na kuwawajibisha. Hata hivyo, ombi hilo halikufanikiwa.
Tukio hilo pia liliwasukuma baadhi ya waandishi kuandika kitabu, kikiwamo kitabu cha Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania kilichoelezea kwa undani matukio hayo. Hata hivyo, kilipigwa marufuku na Serikali mwaka 2000.
Licha ya tukio hilo ambalo kulikuwa na madai ya vifo na majeruhi, ikiwamo kuzua mjadala wa haki za binadamu, uhuru wa dini na uwajibikaji wa Serikali, wizara ya Ali Ameir ikiwa ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha amani na utaratibu ndani ya taifa ilishughulikia changamoto hizo bila kuongeza madhara kwenye jamii.
Licha ya kumzungumzia Ali Ameir akiwa tayari amefariki dunia, lakini majukumu aliyokuwa nayo ya kusimamia usalama wa taifa, kudhibiti vikundi vya dini na kudumisha amani wakati taifa linapitia mabadiliko ya kisiasa na kijamii hayakuwa kazi rahisi.
Kwa upande mmoja wizara yake ilichukua hatua za kiusalama wakati wa migogoro, lakini kwa upande mwingine nchi ilikumbwa na lawama za ukandamizaji, ukosefu wa uwazi na matatizo ya imani na haki za dini.
Uhariri kwenye gazeti la huru
Ali Ameir hakuwa mwanasiasa tu, pia alikuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya CCM— Uhuru, Mzalendo na Burudani, kazi aliyoifanya kwa weledi, ambapo hadi anaondoka magazeti hayo yalikuwa kwenye ubora wa hali ya juu.
Kwenye nafasi yake hiyo pia aliwajibika kusimamia uamuzi ya sera za uandishi na uenezi ili magazeti ya chama yaelezee msimamo wa chama, kampeni, siasa na sera za Serikali kwa uwazi au kulingana na itikadi ya chama.
Mchango wa Ali Ameir katika nafasi hiyo ulilenga kuimarisha mawasiliano ya chama, kusimamia uzingatiaji wa sera za chama katika habari, na kusaidia chama kudumisha mwelekeo wake wa kisiasa kupitia vyombo vya habari vya ndani.