Rais Samia afufua matumaini ya kuwa na Baraza la Vijana la Taifa

Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuanzisha wizara mpya ya Maendeleo ya Vijana, wadau wa siasa wameeleza kwamba hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la Vijana ambalo limekuwa likililiwa kwa muda mrefu.

Novemba 17, 2025, Rais Samia alitangaza baraza lake la mawaziri lenye wizara 27 hukua akianzisha wizara hiyo mpya kwa lengo la kushughulikia masuala ya vijana pekee kwa mustakabali na ustawi wao.

Kuanzishwa kwa wizara hiyo kumesukumwa na kilichotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambapo vijana maarufu kama Gen Z, katika mikoa mbalimbali, walifanya maandamano yaliyotawaliwa na vurugu na kusababisha baadhi yao kuuawa.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ni vijana. Hivyo, kuanzishwa kwa wizara hii kumepokelewa kwa mikono miwili kama hatua muhimu kuelekea kuundwa kwa Baraza la Taifa la Vijana.

Wito wa kuwa na Baraza la Vijana nchini Tanzania ni suala lenye historia ndefu. Tangu miaka ya 1980, zimeshuhudiwa juhudi za kuunda baraza la kitaifa la uwakilishi wa vijana.

Hata hivyo, mara nyingi juhudi hizi hazikufanikiwa mpaka pale serikali ilipoamua kupokea madai hayo na Bunge kutunga sheria rasmi ya kuanzishwa kwa baraza hilo.

Ikumbukwe kuwa Sheria ya Baraza la Vijana ilitungwa mwaka 2015 na kanuni za Baraza hilo zilitangazwa kwenye gazeti la Serikali namba 348, Septemba 15, 2017. Ni miaka 10 sasa imepita lakini bado hakuna kilichotekelezwa.

Dhamira ya sheria hiyo ni kuwa na chombo kitakachoweza kuwaunganisha vijana wote nchini bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, kidini na kikabila katika kutambua, kuchambua na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Pamoja na kutungwa sheria hiyo ambayo kwa zaidi ya miaka 10 sasa haijawahi kutekelezwa, baraza la vijana siyo jambo geni katika mataifa mbalimbali duniani hata hapa Afrika.

Barani Afrika, mataifa mengi yana mabaraza rasmi ya kitaifa ya vijana, baadhi yake ni Kenya, Uganda, Rwanda, Afrika Kusini, Namibia na nyinginezo.

Hata kwa hapa Tanzania, ni Tanzania Bara pekee ndiyo haina Baraza la Vijana, lakini upande wa Zanzibar wana Baraza hilo lililoundwa tangu mwaka 2013.

Nje ya Afrika, mataifa kama Uingereza, India, Canada na mengineyo yana mabaraza ya vijana ambayo ni jukwaa la kushirikisha vijana kutoa maoni na mchango wao kwa nchi kuhusu masuala yanayowahusu ikiwemo elimu, afya na ajira.

Aidha, wadau wengi wanaonyesha matumaini yao kuwa Rais Samia huenda akatimiza ndoto hii wakirejea vipaumbele vyake na hatua yake ya kuanzisha wizara rasmi kwa ajili ya masuala ya vijana.

Katika hatua inayofufua matumaini hayo, Juni 15, 2025, Rais Samia alipozungumza na vijana jijini Mwanza, alionyesha nia ya kukamilishwa kwa utekelezaji wa ajenda ya kuundwa kwa baraza hilo.

“Tutakwenda kuangalia kwa undani kwanini ombi hilo la muda mrefu la baraza la vijana halijaundwa. Tutafanya hivyo ili kuunda baraza litakalowawezesha vijana kueleza ajenda zao za kitaifa bila kujali tofauti zao za kisiasa, kijiografia, kielimu wala kiuchumi,” alisema Rais Samia.

Miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele kuzungumzia uanzishwaji wa baraza hili ni Nusrath Hanje, aliyekuwa mbunge wa viti maalumu katika Bunge la 12.

Nusrat anasema ni wakati mwafaka kwa Serikali kuona haja ya kuanza utekelezaji wa sheria ya kuanzisha barazaa hilo iliyotungwa kipindi cha uongozi wa awamu ya nne ili kuisaidia wizara mpya ya Maendeleo ya Vijana.

“Sasa vijana tunafurahi kuwa hatimaye tuna wizara ya vijana, sheria ya kuundwa kwa Baraza la Vijana ilitungwa tangu mwaka 2015, kwa hiyo kwa sasa chini ya wizara hii ni suala la utekelezaji tu,” amesema mwanasiasa huyo.

Kwa upande wake, Mkazi wa Dar es Salaam, Janeth Mwambije anasema: “Baraza hili litaisaidia wizara kutekeleza majukumu yake kwa sababu linaweza kuwa moja ya chombo cha wizara katika kupokea changamoto za vijana na mitazamo halisi ya vijana juu ya masuala mbalimbali.”

Sheria ya Baraza la Vijana ya mwaka 2015 imeweka muundo wa Baraza la Vijana katika ngazi tano. Kifungu cha 3.0(a) cha sheria hiyo kinataja ngazi hizo ni katika mkoa, wilaya, kata na sekretarieti.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu 4(3), uanachama wa Baraza unaanzia kwenye ngazi ya kata na utakuwa wa wazi na wa hiari kwa vijana kutoka kata husika, asasi za vijana zilizosajiliwa kitaifa na vijana waliochaguliwa na kamati ya maendeleo ya kata.

Kwa mujibu wa sheria, katika ngazi ya taifa, Baraza hilo litakuwa na wajumbe 29 ambao ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu mtendaji na wajumbe 26 kutoka mikoa ya Tanzania Bara.

Kuunda Baraza la Vijana kunatajwa kuwa hatua yenye manufaa makubwa kwa vijana. Wadau wanaona Baraza litasaidia wizara kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa ajenda zake, kwani uamuzi unayochukuliwa utatokana na ushahidi na maoni ya vijana wenyewe.

Aidha, litakuza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii, jambo linaloongeza fursa za ajira na uwekezaji kwa vijana. Pia, litawapa vijana fursa ya kujifunza uongozi wa kijamii na kisiasa kwa mtazamo wa taifa na kuchochea uzalendo na uadilifu.

“Baraza la vijana ni daraja kati ya Serikali na vijana, na kuanzishwa kwake kutaiwezesha wizara mpya kutekeleza majukumu yake kwa nguvu, ufanisi na mwamko mkubwa wa kitaifa ikiwemo kutoa ushauri wa kisera na ushahidi wa takwimu kuhusu mahitaji na changamoto za vijana,” anasema Dk Onesmo Kyauke, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na utawala bora.

Dk Kyauke anasema Baraza hilo pia litasaidia katika kuratibu programu za vijana kutoka wizara na taasisi mbalimbali ili kuepusha urudiaji na kuongeza ufanisi, kutoa sauti ya vijana isiyo ya kisiasa, hivyo kuongeza ushirikishwaji na kupunguza migogoro ya kijamii.

“Baraza litakuza ubunifu, ajira na uchumi wa kidigitali kupitia tafiti na mapendekezo ya sheria na mfumo rafiki kwa vijana. Pia, litawezesha kuwakilisha nchi kimataifa kwenye majukwaa ya AU, UN na EAC yanayohitaji wawakilishi wa mabaraza ya vijana,” anaongeza Dk Kyauke.

Mataifa mbalimbali ya Afrika yana mabaraza ya vijana ambayo yamekuwa yakiwakutanisha katika umoja huo.

Mwaka huu, kongamano la vijana wa Afrika limefanyika Nairobi, Kenya ambapo Tanzania pia iliwakilishwa na baadhi ya vijana kwenye kongamano hilo.

hata hivyo, kumekuwa na sauti za vijana kutaka kuwa na baraza hilo ili kuwaunganisha vijana wote nje ya misingi ya itikadi zao za kisiasa, dini zao, hali yao kiuchumi au mahali wanapotoka, jambo ambalo litajenga umoja.