Dodoma. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetakiwa kutumia mbinu za kisasa kufanya uchunguzi na kuanzisha programu za utafiti, uchambuzi na utoaji wa elimu ya uadilifu kwa umma ili kusaidia kupunguza mmomonyoko wa maadili nchini.
Agizo hilo limetolewa leo Jumatano, Novemba 26, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Makao Makuu jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, Waziri Kikwete ameambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Regina Qwaray na kuzungumza na watumishi wa taasisi hiyo.
Waziri Ridhiwani ameutaka uongozi wa sekretarieti kushirikiana na taasisi nyingine za utawala bora nchini kufanya utafiti wa hali ya maadili, kutoa elimu ya uzalendo na uelewa kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kusaidia kupunguza mmomonyoko wa maadili.
“Lakini, naiagiza Sekretarieti ya Maadili kutowaonea aibu viongozi wa umma wanaolalamikiwa kukiuka maadili kwa sababu ni jukumu lenu kufuatilia tabia na mienendo ya viongozi nchini,” amesema Ridhiwani.
Pia, amesema chombo hicho ni kama msumeno wenye ncha kali, hivyo kinapaswa kutumiwa katika kuimarisha uadilifu kwa kutafuta ushahidi wa ukiukaji wa maadili miongoni mwa viongozi wa umma ili wahusika waitwe, wakemewe inapobidi au wachukuliwe hatua pale wanapobainika kukiuka misingi ya maadili.
“Mmesema hapa kuna baadhi ya viongozi wana hofu ya kujaza tamko kwa njia ya mtandao, hili sio tatizo la Serikali, mmeshaweka mifumo ya kupokea Tamko la Rasilimali na Madeni hakikisheni viongozi wote wanajaza ifikapo Desemba 31, 2025,” amesisitiza.
Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi amesema Sekretarieti ya Maadili katika utekelezaji wa majukumu yake inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo ukosefu wa ushahidi wa baadhi ya malalamiko ya ukiukwaji wa maadili yanayowahusu viongozi wa umma.
Jaji Mwangesi amesema tatizo hilo linatokana na baadhi ya mashahidi kutokuwa tayari kutoa ushahidi mbele ya Baraza la Maadili kutokana na hofu au kuogopa vitisho vinavyodaiwa kutokea sehemu zao za kazi.
Amesema ili kuboresha huduma na kuimarisha utoaji wa elimu, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inapanga kuanzisha ofisi katika mikoa mbalimbali, hatua itakayosaidia kusogeza huduma karibu na viongozi wa umma na wananchi, hasa katika kutoa elimu juu ya mgongano wa masilahi.