Sababu mechi za Wagosi kuondolewa usiku Tanga

KAMA ni shabiki wa Coastal Union (Wagosi wa Kaya) na ulikuwa na mipango ya kutaka kushuhudia mechi za usiku kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati wababe hao wa zamani wa Ligi ya Bara wakicheza, taarifa ikufikie kwamba zinapigwa mchana kweupe.

Coastal iliamua mechi zote za nyumbani kupigwa usiku kutokana na uwanja huo kufungwa taa kama ilivyo kwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, lakini ghafla mipango imebadilika na Bodi ya Ligi (TPLB) imeweka bayana sababu ya kufanya uamuzi huo ikianza na mechi ya jana dhidi ya Mbeya City iliyopigwa saa 8 mchana.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa bodi hiyo, Karim Boimanda alisema wamezuia  Uwanja wa Mkwakwani kutumika kwa mechi za usiku sababu ikiwa ni kutokana changamoto ya umeme uwanjani hapo.

“Hakutakuwa na mechi za usiku ni sababu ya kuweka michezo ya wenyeji mchana licha ya kuwepo kwa taa ambazo zinaweza kuifanya timu hiyo icheze usiku kutokana na changamoto ya umeme,” alifafanua Boimanda, huku Meneja wa Uwanja wa Mkwakwani, Akida Machai akisema wamepokea barua kutoka bodi kutoruhusu mechi za usiku kutokana na changamoto ya umeme na wao kama wamiliki wa uwanja wanaendelea na marekebisho ili taa ziendane na kile kinachotakiwa.

“Marekebisho makubwa yanaendelea kufanyika wana Tanga watarudishiwa burudani ya kuiona timu yao ikicheza usiku. Kwa sasa mambo yataendelea kama ratiba inavyotaka kwa timu kupangiwa mechi za mchana na jioni,’’ alisema Matai.

“Ubora unaotakiwa kwa mujibu wa kanuni unaendelea kufanyiwa kazi. Kilichopo sasa ni wadau na wapenzi wa timu kuendelea kutupa ushirikiano ili kuipambania iweze kufanya vizuri. Bila mashabiki hakuna mpira nawaomba mjitokeze kwa wingi kuipa sapoti Coastal Union.”