Uchaguzi wa mbunge Siha kufanyika Desemba 30

Siha. Ikiwa zimebaki siku 33 kabla ya kufanyika uchaguzi wa mbunge Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro wananchi wametakiwa kujitokeza kupiga kura Desemba 30, mwaka huu katika uchaguzi huo.

Uchaguzi huo ulisogezwa mbele na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufuatia kifo cha aliyekuwa mgombea wa ubunge kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Daud Ntuyehabi kilichotokea Oktoba 7, 2025 katika Kijiji cha Kilingi, wilayani Siha.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za CCM Sanyajuu, jana Novemba 25, 2025, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Wilaya ya Siha, Emanuel Mushali, ametoa wito kwa wana-CCM na wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuhakikisha wanatunza kadi zao ili wawe na sifa ya kupiga kura.

Amesema kushiriki uchaguzi ni haki ya kikatiba inayomruhusu kila mwananchi kumchagua kiongozi anayemtaka ambaye atawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Emanuel Mushali,Mwenezi CCM ,Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro,akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake

“Nichukue fursa hii kuwataka wana-CCM na wananchi wote wenye sifa, kutumia haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kwa wingi Desemba 30, 2025 kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo,” amesema Mushali.

Ameeleza kuwa wananchi wote waliotimiza umri wa miaka 18 na waliojiandikisha na kupatiwa vitambulisho vya kupigia kura wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kujitokeza kupiga kura, ili kuimarisha demokrasia na kuhakikisha sauti zao zinasikika kupitia sanduku la kura.

Mushali amesema kampeni za uchaguzi zimeanza rasmi Oktoba 22, 2025 na zinaendelea katika kata, vijiji na kupitia vikao vya ndani, akibainisha kuwa mwitikio wa wananchi ni mkubwa na unaridhisha hadi kufikia sasa.

Ameongeza kuwa ni muhimu wananchi kuendelea kudumisha amani, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Idrisa Mndeme, mmoja wa wananchi wa jimbo hilo, amesema amejipanga kushiriki uchaguzi huo na kuwataka wananchi wengine wajitokeze kwa wingi kwani ni jukumu la msingi kwa maendeleo ya eneo hilo.

Vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ni CCM, NRA, MAKINI, ACT-Wazalendo na SAU.