Veta yaagizwa kurejesha kozi za kilimo, ufugaji na ujasiriamali

Dodoma. Serikali imeitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kurejesha kozi mbalimbali ambazo awali ziliondolewa ikiwemo kilimo, ufugaji na ujasiriamali ili ziendane na mazingira na fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo husika, lengo likiwa kuwawezesha wananchi na vijana kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa eneo hilo.

Agizo hilo limetolewa leo, Novemba 26, 2025 wilayani Chemba mkoani Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za Veta na uzinduzi wa ugawaji vifaa vya mafunzo kwa vyuo 63 vya mamlaka hiyo.

Wanu amesema kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa kuwa inampa fursa ya kujionea kwa karibu namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.

Amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua katika ujenzi wa viwanda, maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa sekta za madini na utalii, sekta ambazo zinahitaji wafanyakazi wenye ujuzi mahiri unaotokana na mafunzo ya ufundi stadi.
“Veta ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi. Ni lazima tuhakikishe mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya sasa, hasa katika eneo la Tehama na fani nyingine zinazohitajika sokoni,” amesema Wanu.
Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuipatia mamlaka hiyo vifaa vya kisasa pamoja na kuajiri walimu wapya kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira, kwani tayari Serikali imepata kibali cha ajira 300, na Veta Chemba itapewa kipaumbele katika mgao wa watumishi hao.

Hata hivyo, Wanu ameuagiza uongozi wa chuo hicho kutumia vijana wanaosoma hapo kujenga uzio kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo ili kuwasaidia wanafunzi wanaoishi bwenini.

Awali, Mbunge wa Chemba, Kunti Majala, aliwasilisha ombi la kupatiwa walimu katika kozi nne ambazo kwa sasa hazina wakufunzi, akisisitiza umuhimu wa kurejesha kozi za kilimo na ufugaji ili wananchi wanufaike na fursa hizo.
Serikali imeagizwa kurejesha kozi hizo fupi ikiwemo kilimo, ufugaji na ujasiriamali ili wananchi waweze kunufaika moja kwa moja katika maeneo wanayoishi, hatua itakayosaidia kuinua uchumi wa sehemu husika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Veta Tanzania, Anthony Kasore, amesema vifaa hivyo vitasaidia kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo, ambapo takribani Sh1.7 bilioni zimetolewa na Serikali kununua vifaa hivyo.