Vijana Tunduma wamtwisha Nanauka zigo la mikopo

Baadhi ya Vijana katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe wamesema ukosefu wa uelewa wa pamoja na jukwaa la kuwasemea ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha kushiriki kikamilifu katika maendeleo, licha ya kuwepo kwa mipango ya maendeleo ya vijana.

Vijana hao wametoa kero hiyo wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi Ya Rais, Maendeleo ya Vijana,  Joel Nanauka, ambapo kiongozi huyo  alizungumza na makundi mbalimbali katika mji huo.

Vijana walizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na  ufinyu wa bajeti ya mikopo, ukosefu wa ajira na kutosikilizwa.
Akizungumza kwa niaba ya vijana Mwenyekiti wa bajaji katika halmashauri ya mji wa Tunduma, Liziki Mwampamba, amesema changamoto inayowakabili vijana licha ya kupewa mikopo na halmashauri bado kiwango cha marejesho ya mikopo hiyo kimekuwa kikubwa kuliko muda pamoja na faida wanayoipata katika shughuli zao za kila siku.

Hali hiyo inawalazimu baadhi ya vijana kukopa fedha nyingine ili kukamilisha marejesho, jambo linalosababisha presha kubwa kifamilia na kiuchumi.

Mwampamba amemwelekeza Waziri Nanauka kuwa Serikali inatakiwa kupunguza kiwango cha marejesho au kuongeza muda wa kurejesha mikopo, ili kuwawezesha Vijana kutekeleza majukumu yao bila kubanwa kiuchumi na bado waweze kurejesha mikopo kwa wakati.

“Kwa sasa vijana wanaenda kukopa mikopo ya kausha damu ili kurejesha mkopo hali inapelekea  kutumikia kurejesha mikopo , huku familia zao zikiendelea kuishi maisha ya shida tunaomba sana serikali itusikize,” amesema Mwampamba.

Samweli Ngao amesema rushwa ni miongoni mwa vikwazo katika upatikanaji wa mikopo katika halmashauri zetu pamoja na masharti kuwa magumu kitendo ambacho baadhi ya vijana kukata tamaa kuomba mikopo.

“Wizara hii mpya imeundwa kwa lengo la kuleta suluhu ya changamoto zinazowakabili vijana tuwaombe muache tu kupiga makofi, mshaurini Rais atatue changamoto za vijana kwani Tanzania ni yetu sote na tunahitaji mafanikio ya Pamoja,” amesema Ngao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodaboda wilaya ya Momba, Paulo Muywanga amemwomba Waziri Nanauka kuwasaidia vijana waliojiajiri kwenye bodaboda kuwapunguzia gharama ya upatikanaji wa leseni inayotozwa hivi sasa ambayo ni Sh30,000 wanayoshindwa kuimudu, licha ya kupunguzwa kutoka Sh70,000.

Akijibu kero za vijana hao ikiwemo za mikopo Waziri Nanauka amesema Serikali inatarajia kutenga Sh200 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana wanawake na watu wenye mahitaji maalumu ili kukidhi mahitaji yao na kupata fedha kwa wingi.

Waziri Nanauka amesema kutokana na wingi wa mahitaji fedha zilizopo bado hazitoshi hivyo zitakapotolewa na Serikali amewataka viongozi wa halmashauri kote nchini kuwasaidia vijana ambao hawajakidhi vigezo, ili waweze kupata mikopo hiyo kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, Waziri Nanauka amesema wizara imekusudia kuanzisha mfumo maalumu wa kiteknolojia utakaowawezesha vijana wote nchini kuwasilisha maoni na changamoto zao moja kwa moja, ambapo watumishi wa wizara pamoja na waziri watazipitia taarifa hizo na kutoa majibu au ufumbuzi stahiki.

Aidha  Nanauka ametoa maagizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe , Jabir Makame kukutana na vijana wajadiliane namna ya kutoa marejesho ambayo yatakuwa na faida pande zote mbili, kwani dhamira ya mikopo ni kuwatoa wananchi kwenye umaskini.