Dar es Salaam. Wakati swali la uhuru na nafasi ya vyombo vya habari vya ndani nchini Tanzania likishamiri, wadau, wataalamu wataka Serikali itengue vikwazo vya uhuru wa vyombo vya habari.
Wakati wadau wakitaka hayo, Serikali imetoa mwelekeo ikiondoa hofu kuwa vyombo hivyo vina uhuru wa kutosha.
Hayo yamedhihirika kufuatia kauli iliyotolewa na Serikali katika kikao maalumu cha Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana Novemba, 25, 2025.
Katika kikao hicho, ambacho Waziri Mkuu alitolea ufafanuzi masuala mbalimbali yakiwemo hali ya nchi tangu kuibuka kwa mzozo wa kisiasa uliochochewa na maandamano na vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, wahariri wa vyombo vya habari walipata nafasi ya kuuliza maswali kwa Serikali.
Miongoni mwa maswali magumu ambayo wahariri hao wa vyombo mbalimbali vya habari nchini waliuliza, ni lile lililoulizwa na Neville Meena, mmoja wa wahariri walioshiriki kikao hicho, ambaye alihoji juu ya Serikali kuingilia mamlaka ya vyombo vya habari akiomba ufafanuzi wa Serikali kuviwezesha vyombo hivyo kufanya kazi kwa misingi ya kitaaluma bila kuingiliwa uhuru wake.
“Tunapozungumza hivi, vyombo vya habari hatuna pa kusimama tunaonekana watu wa hovyo kuwa hatukufanya kazi yetu ipasavyo wakati wa uchaguzi, na hii ilitokana na tabia ya taasisi ya Serikali kututisha kwa kile tulitaka kufanya ikiwemo TCRA kutuandikia barua, ni nini mkakati wa Serikali kuhusu taasisi za Serikali kutuingilia kufanya kazi yetu? alihoji Meena.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, aliwatoa hofu wadau wa vyombo vya habari akisema wanapaswa kufanya kazi yao kwa uhuru.
“Vyombo vya habari vinatakiwa kufanya kazi yake kwa uhuru, vinapokosoa vinatoa njia ya kipi kifanyike. Siyo hayo tu Serikali pia itaweka mifumo kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari vilevile. Niwaombe wahariri na waandishi wa habari wakati wowote kukiwa na jambo ofisi yangu ipo wazi,” alisema.
Profesa Kabudi aliweka wazi nia ya Serikali kuwa ipo katika mchakato wa kupitia sera ya vyombo vya habari ya mwaka 2013 ili kuweka mazingira rafiki kwa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Akizungumzia majibu hayo ya Serikali, Mevin Meena aliliambia Mwananchi kuwa majibu ya Serikali yameonesha nia njema, lakini bado ipo hofu kuhusu nia ya dhati ya usimamizi wake katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari.
“Sisi waandishi wa habari ni wanataaluma tunafanya kazi kwa misingi ya taaluma. Kwa mujibu wa sheria ya vyombo vya habari ya mwaka 2016, uandishi wa habari ni taaluma, hata Bodi ya ithibati (Jab) pia inasema na inatoa vibali vya kumtambua mwandishi wa habari kama mwanataaluma, hivyo tunaijua na tunaifanya kazi yetu kama wanataaluma,” amesema.
Meena ameeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari unapasa kulindwa kwa misingi ya kitaaluma badala ya kupangiwa namna ya kufanya kutoka katika mamlaka zingine za Serikali ili kutoa nafasi kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru.
“Kuna nyakati Serikali inaingilia uhuru wa wanahabari kinyume na misingi ya kitaaluma. Mfano kipindi cha uchaguzi tulizimiwa mitandao, redio na TV nazo zikazuiwa kurusha matangazo ya mashirika ya nje wanayoshirikiana nayo kama Deutche Welle (DW) na British Broadcasting Cooperation (BBC). Mimi ninasisitiza waache kuingilia uhuru wa vyombo vya habari,” amesisitiza.
Akizungumzia kauli hiyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema bado uhuru kamili wa vyombo vya habari hautaimarika bila mabadiliko ya sheria.
Yeye anaona kuwa matatizo yanayoathiri uhuru wa vyombo vya habari yametokana na misingi ya kisheria akibainisha kuwa sheria haiwezi kutolewa kwa tamko bila kutungiwa sheria mpya ya utekelezaji wa uhuru huo.
“Kauli ya waziri ni tamko la kisiasa haliwezi kuvipatia uhuru vyombo vya habari bila kuangaliwa misingi ya kisheria. Mabadiliko ya kisheria ni msingi bora wa kulinda vyombo hivyo,” amesema.
Dk Mbunda ameongeza kuwa inahitajika kuwekwa mifumo ya kudhibiti maamuzi ya mamlaka za Serikali zinazosimamia vyombo vya habari ili maamuzi ya mwisho juu ya haki za vyombo hivyo yatolewe na Mahakama za haki badala ya mamlaka kuliona kosa na kutoa adhabu bila kuwepo na mzani wa haki.
“Vyombo vyetu vya habari ili viwe huru, lazima sheria zibadilike, waziri kama kweli anayo nia ya kuvisaidia vyombo vya habari kufanya kazi kitaaluma na kwa uhuru anapaswa aandae muswada uende bungeni itungwe sheria ya kuondoa mamlaka ya taasisi za usimamizi wa vyombo hivyo zilizopewa mamlaka ya kujiamulia kufungia vyombo vya habari bila kupitia mahakamani,” amesema.
Dk Mbunda ameongeza kuwa, Serikali haipaswi kuwa msimamizi na mtoa adhabu badala yake isimamie na pale inapohisi kuna chombo kimefanya kosa badala ya kukiadhibu kishtakiwe mahakamani sheria na misingi ya haki ifuatwe katika kuona kosa la chombo husika na adhabu inayostahili.
Mtazamo kama huo unaungwa mkono na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Fulgence Massawe, ambaye amesema changamoto za sekta ya habari nchini zinatokana na mifumo ya kisheria akitoa wito kwa Serikali kufanya mapitio ya sheria hizo ili kuimarisha uhuru wa sekta hiyo muhimu nchini.
“Ili kuifanya sekta ya habari iwe huru nchini lazima mifumo yote ya sheria za habari ifumuliwe, kwani sheria ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 imevipa mamlaka makubwa sana vyombo vya Serikali vinavyosimamia tasnia ya habari, hivyo kufanya uhuru wa habari kuminywa,” amesema.
Wakili Massawe amesema kuwa kauli iliyotolewa na Serikali jana, haitatosha kutoa uhuru wa vyombo hivyo bila kuingilia na kufumua mifumo ya sheria kandamizi zinazobana uhuru huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahiri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amepongeza kauli hiyo ya Serikali akiwataka wadau wa vyombo vya habari kutumia fursa hiyo kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo serikalini ili kupata utatuzi.