Wakili kesi ya uhaini Mwanza azikwa, Padri adokeza ndoa aliyopanga kufunga mwakani

Mwanza. Wakili wa kujitegemea, Beatus Linda amezikwa leo Jumatano Novemba 26, 2025 nyumbani kwao Mtaa wa Mtakuja, Kata ya Nyamhongolo wilayani Ilemela, Mwanza saa 10 jioni, huku mamia ya waombeleaji wakishiriki mazishi hayo.

Linda ambaye ni mmiliki wa ofisi ya uwakili ya Linda & Co. Advocates alifariki usiku wa kuamkia Jumapili Novemba 23, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Agha Khan jijini Mwanza.

Linda alikuwa ni miongoni mwa mawakili 37 wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Mwanza waliojitolea kutoa huduma ya msaada wa kisheria na kuwatetea watuhumiwa wa wote wa kesi zilizotokana na maandamano baada ya uchaguzi mkuu Okotba 29, 2025 katika mkoa wa Mwanza.

Waombolezaji wakiaga jeneza lililobeba mwili wa Wakili Beatus Linda kwa ajili ya mazishi, leo Novemba 26, 2025 Nyamhongolo wilayani Ilemela, Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Ambapo, mara ya mwisho Novemba 19, 2025 aliongoza jopo la mawakili kuwatetea na kuwawakilisha vijana 93 waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini, uporaji wa kutumia silaha, fujo na kuharibu mali kutokana na maandamano ya baada ya uchaguzi.‎

Mazishi hayo yamevuta hisia za mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza ambapo mawakili wenzake, wanasheria, mahakimu, wananchi, waumini wa Kanisa Katoliki, wanafunzi aliosoma nao, ndugu, jamaa na marafiki wameungana  kumsindikiza katika safari yake ya mwisho mpendwa wao.

Akisoma historia ya marehemu, Makamu Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Mwanza, Erick Mutta amesema Linda ameacha watoto watatu, Lincoln, Kendrick na Eliah huku akiacha mchumba wake, Ruth Mwakitalu ambaye walikuwa na malengo ya kufunga ndoa mapema mwakani (2026).

Amesema wakili huyo alikuwa mpenda michezo, Mkatoliki wa kweli, ‎‎aliyetimiza wajibu wa mahakama, wateja, na mawakili wenzake nyakati zote kwa miaka yote aliyodumu kwenye uwakili. 

“Alikuwa muungwana, mcheshi, kijana mpole, mtanashati aliyejali pia maisha ya wanyonge wasioweza kumudu gharama za uwakili, ambapo alijitolea kwa ajili yao,” amesema Padri Mutta.

Waombolezaji wakiaga jeneza lililobeba mwili wa Wakili Beatus Linda kwa ajili ya mazishi, leo Novemba 26, 2025 Nyamhongolo wilayani Ilemela, Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Ameongeza kuwa; “Maisha yake ndani na nje ya viunga vya Mahakama yalisukumwa zaidi na kiu ya haki, weledi na maarifa, matumizi sahihi ya muda, tafsiri ya Sheria na msaada kwa aliowawakilisha na Mahakama ili kutoa maamuzi ya haki.”‎‎

Amesema kutokana na utumishi wake uliotukuka, maisha ya Wakili Linda yatazidi kusomwa vizazi na vizazi kwenye kurasa za maamuzi ya mahakama na daima ataendelea kuishi.

Innocent Mwakitalu ambaye ni kaka wa mchumba wa Beatus, amesema kifo hicho ni pigo kwa familia yao kwani ni miezi mitatu tu na siku 10 tangu walipomtambulishana kwa ajili ya uchumba wao jijini Dar es Salaam (Engagement) na walipanga kufunga ndoa yao Juni, 2026.

“Ni pigo kubwa sana kwetu tunatoa pole kwa familia na TLS, tumeumia sana, Beatus alikuwa ni rafiki, kaka, shemeji na tunategemea pengine yangekuwa makubwa zaidi kuliko hapa alipofika. Lakini imekuwa ni muda mdogo sana kwetu na pengine tulipanga Juni 2026 tungeweza kufanya harusi lakini hatujafika huko,” amesema Mwakitaku.

Akiongoza ibada ya mazishi, Paroko wa Parokia ya Nyamhongolo Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Padre George Nzungu amempongeza Beatus kwa kutimiza wajibu wake wa kutenda haki  ikiwemo kutetea wananchi wanyonge waliokamatwa kwenye vurugu zilizotokana na maandamano ya baada ya uchaguzi mkuu.

Nzungu amekemea tabia ya wasomi na watu waliopewa nafasi ya kutumikia wananchi kuhalalisha uongo na kupindisha ukweli bila kuwasikiliza wanyonge na masikini, jambo linalowafanya washindwe kutafsiri vyema vitendo vinavyochukuliwa kwa hasira na wananchi hao.

“Tunapoelekea sasa hivi Tanzania kuhalalisha uongo uwe ukweli, wasomi wakubwa wanasomeshwa kwa gharama ya nchi wanapindisha ukweli. Linda (marehemu) hakutaka hivyo, mnapopindisha ukweli na kuonea wanyonge, maskini, yatima, mjane mnamkosea Mungu,” amesema Nzungu.

Ameongeza kuwa; “Tusimame katika haki, leo kuna watu wetu wanaandamana kuna fujo zimetokea mtu anaenda kuiba bia huyo ana njaa, wanaenda kuvamia godoro za watu huyo analala chini, lazima tutafsiri changamoto za wananchi mnapindisha nini hamuwaoni hapo?.”

Mwenyekiti wa mtaa wa Mtakuja Kata ya Nyamhongolo, Magina Adamu amesema Beatus alikuwa akishiriki shughuli za kijamii katika mtaa huo na kuheshimu kila mtu, huku akiwahimiza wananchi kuomboleza kwa amani na utulivu na kulishika neno la Mungu.

“Nimekuwa nikimfahamu mwenzetu, tulikuwa naye bega kwa bega kwenye mtaa wetu, alikuwa ni mtu anayeshirikiana na kila jamii, na hata utakapokutana nae barabarani husimama na kusalimia nae,” amesema Adamu.

Alizaliwa Oktoba 23, 1989 katika familia ya Beatus Linda, akabatizwa kwa jina la Yohana Desemba 18, 1989 na kupewa Komunio na Kipaimara Februari 2003‎‎.

Alisoma Shule ya Msingi Green View, mwaka 2005 akasoma Shule ya Sekondari Kahunda, kisha Sekondari ya Nsumba na kuhitimu mwaka 2011.‎‎

Mwaka 2011 – 2015 akajiunga na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (Saut) Mwanza kwa masomo ya Shahada ya kwanza ya Sheria.‎

Mwaka 2016 alitunukiwa Astashahada ya juu ya sheria kwa vitendo (Post Graduate Diploma in Legal Practice)‎‎

Desemba 14, 2018 alikubaliwa rasmi kuwa Wakili wa Mahakama Kuu na Mahakama za chini yake‎‎.

Mwaka 2023 alifanikiwa kufungua ofisi yake ya uwakili akipita Linda & Co. Advocates