KIKOSI cha Azam FC tayari kimeshaanza mazoezi ya kujifua na mechi ya kesho dhidi ya Wydad, huku mastaa wakionekana kuwa na morali ya kutosha.
Mastaa hao waliopokelewa kwa vaibu na shangwe na mashabiki waliojitokeza nje ya Uwanja wa New Amaan Complex kabla ya kuanza mazoezi na hali ikiwa hiyo hiyo.
Kwa kuwatazama tu usoni, utaona ari kubwa waliyonayo huku wakiwa wamegawanywa katika makundi mawili.
Mwanaspoti imeshuhudia wachezaji hao wakiwa katika hali ya umakini na utulivu mkubwa, huku wakifuata maelekezo wanayopewa na makocha wao wakiongozwa na Florent Ibenge.
Wachezaji hao ambao wameanza mazoezi Saa11:00 jioni, wanatumia uwanja mdogo ambao upo pembezoni mwa ule watakaoutumia kesho dhidi ya Wydad ambayo tayari ipo visiwani hapa.
Ikumbukwe kuwa, Azam itakutana kesho na Wydad, huku ikitoka kupoteza 2-0 ugenini mbele ya Maniema ya DR Congo katika mechi ya kwanza ya michuano hii ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wydad yenye nyota kadhaa maarufu akiwamo Stephane Aziz Ki ilishinda nyumbani kwa mabai 3-0 dhidi ya Nairobi United.
