Arusha. Mahakama ya Rufaa ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) imeitupili mbali rufaa iliyokuwa inapinga utekelezaji wa mradi wa Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kutokana na shauri hilo kuwasilishwa nje ya muda.
Awali, EACJ ilitupilia mbali kesi iliyokuwa ikilenga kusitishwa kwa ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya dola 4 bilioni, unaohusisha bomba lenye urefu wa kilomita 1,443 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert (Uganda) hadi Bandari Hindi, Tanga.
Mashirika manne ya kiraia kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Uganda yalikata rufaa mahakamani hapo baada ya kesi ya awali kutupiliwa mbali mahakamani hapo, Novemba 29, 2023 kwa kuwa shauri hilo liliwasilishwa nje ya muda, hivyo haikuwa na uwezo wa kulisikiliza.
Hukumu hiyo imetolewa jana Novemba 26, 2025 na jopo la majaji watano wa EACJ wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Nestor Kayobara. Wengine ni Anita Mugeni, Kathurima M’Inoti, Cheborion Barishaki na Omari Makungu.
Rufaa hiyo namba 4/2023 ilifunguliwa na Shirika la Center For Food And Adequate Living Rights (CEFROHT), African Institute For Energy Governance (AFIEGO), Natural Justice Kenya na Center For Stategic Litigation Limited.
Baada ya kupitia mwenendo na kusikiliza hoja za pande zote, majaji hao walitupilia mbali rufaa hiyo na kukubaliana na uamuzi awali kuwa shauri lilifunguliwa nje ya muda na wakaamua kila upande ubebe gharama zake.
Mashirika hayo yalikata rufaa hiyo Novemba 2023, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Uganda na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).
Rufaa hiyo ilihusu shauri ambalo mashirika hayo yalishindwa awali, kwamba mradi huo ungeathiri wananchi, maeneo ya hifadhi, bioanuwai na usalama wa chakula, pamoja na madai ya kutolipwa ipasavyo kwa watu walioathiriwa na mradi.
Hoja za mashirika hayo zilijengwa kuwa makubaliano baina ya Serikali na Serikali (IGA) pamoja na mkataba wa uwekezaji (HGA) hayakuzingatia misingi ya utawala bora, mazingira, haki za binadamu kinyume na masharti mbalimbali ya EAC.
Walidai mradi wa EACOP unakiuka haki za binadamu na kutozingatia masuala ya mazingira, kama vile hifadhi ya misitu, vyanzo vya maji, maeneo oevu, maeneo ya kimataifa ya uhifadhi, ndege, wanyama na wanyamapori na kwamba utakuwa na athari kubwa kwa usalama wa chakula.
Warufani walidai Mei 2017, wajibu rufaa wa kwanza na wa pili walisaini IGA kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo wakati mradi huo umekiuka Mkataba wa EAC.
Walikuwa wakiomba Mahakama itoe amri ya kudumu ya kuwazuia kujenga bomba hilo katika maeneo yaliyohifadhiwa, wajibu rufaa kuhakikisha kwamba kabla ya kuanza tena utekelezaji wa mradi, mamlaka zilizopewa mamlaka zifanye tathmini ya mara kwa mara ya mazingira, haki za binadamu na athari za kijamii, kwa ushirikishwaji wa umma unaoeleweka.
Warufani hao waliomba kwamba Mahakama hii iruhusu Rufaa, kuweka kando na kutengua uamuzi wake wa awali, kwa kuwa ilikosea kisheria kutupilia mbali kesi yao kufuatia kukubali pingamizi lililowasilishwa na upande wa wajibu rufaa.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali kesi ya awali Novemba 29, 2023 kwa gharama, kutokana na kufunguliwa nje ya muda; na jana rufaa waliyokata kwa kutokubaliana na hukumu hiyo, pia imetupwa.
Baada ya uamuzi huo Wakili kutoka Shirika la Center for Strategic Litigation (CSL) la Tanzania, Noel Mdoe, amesema watajadiliana kuona namna ya kuendelea kupambana kwenye suala hilo.
Amesema kuwa hawataishia hapo kwa sababu hoja zao zina mashiko kisheria, kwani zimejikita katika masuala yanayohusu haki za binadamu, mabadiliko ya tabianchi na mazingira kwa ujumla.
“Tutaendelea, safari bado ni mbichi, tutakaa na wadau wetu, tutashauriana nao ili kuangalia hatua mbalimbali za kisheria, ambazo tunaweza tukazichukua ikiwemo kikanda au kimataifa kwa ajili ya masilahi mapana ya nchi na jumuiya yetu kwa ujumla,” amesema.