Kocha JS kabylie akuna kichwa, Pedro ashtukia mchongo

PRESHA inapanda na kushuka kwa Kocha wa JS Kabylie, Mjerumani Josef Zinnbauer, huku kichwa kikimpasuka pamoja na benchi lake la ufundi ikiwa zimesalia siku chache kabla ya mechi ya  pili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga.

Zinnbauer anaingia wiki  nyingine ngumu, baada ya kikosi hicho kuanza vibaya hatua hiyo kwa kuchapwa mabao 4-1 na Al Ahly, Misri.

Kwa upande mwingine, Yanga imeanza vizuri na hii ni mara ya tatu mfululizo kucheza hatua ya makundi, baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya FAR Rabat katika dimba la Amaan, Zanzibar.

KOJS 01

Taarifa kutoka Algeria zinaeleza uongozi wa JS Kabylie umeanza kuweka presha  kwa Zinnbauer kuhakikisha timu inarejea kwenye reli baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo katika mashindano yote, moja ikiwa ya ligi ya Algeria dhidi ya Constantine kwa bao 1-0.

Kocha huyo alipohojiwa na moja ya vyombo vya habari nchini humo, amesema; “Tunajua  ukubwa wa kazi iliyopo mbele yetu hasa ukizingatia tumeanza kwa kupoteza, huu ni wakati wetu kujibu maswali uwanjani.”

Licha ya maneno hayo ya kishujaa, Zinnbauer anakabiliwa na presha ya matokeo ya ushindi kwani anajua mashabiki wa Kabylie hawawezi kuvumilia sare achilia mbali kipigo kwenye uwanja wao wa nyumbani.

KOJS 02

Kocha huyo, alipata kibarua cha kukinoa kikosi hicho, Januari 20, 2025 kisha Juni 2025, baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Algeria ya msimu wa 2024-25, aliiongoza JSK kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025-26,  kwa sasa wapo nafasi ya saba kwenye ligi yao ya ndani na kimataifa ndio kama hivyo wameanza kwa kipigo.

Yanga, kwa upande wao, imeanza kupanga mipango kimya kimya nchini humo  lakini kwa umakini, wakijua mazingira ya Kaskazini mwa Afrika mara nyingi huwa magumu. Mara ya mwisho kwa Yanga kucheza mechi ya makundi nchini humo, ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Belouzdad.

KOJS 03

Benchi la ufundi la Yanga linatajwa kufanya mapitio ya mechi iliyopita ya wapinzani hao ili kubaini makosa yanayoweza kuwa kama silaha kwao.

“Hatutadanganywa na matokeo yao ya kwanza. Timu ikicheza nyumbani huwa tofauti, lazima tuwe na mpango wa kupambana dakika zote,” amesema Kocha wa Yanga, Pedro  Goncalves.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo historia itaandikwa katika mechi hiyo.