Tanzania ipo katikati ya enzi ya malipo ya kidijitali ambapo matumizi ya mifumo mbalimbali ya malipo kielektroniki imekuwa njia pendwa ya kufanya miamala ya kifedha baina ya mamilioni ya watu kila siku.
Hata hivyo, Mashine za Kutolea Pesa (ATM) bado zinaendelea kuongezeka na kuendelea kuwa sehemu muhimu ya utoaji wa mfumo wa kifedha, jambo linaloweza kuibua maswali katika mfumo wa utoaji huduma za fedha kwa sasa, kuna umuhimu wa kuendelea kuwa na ATM katika zama hizi za huduma za fedha kielektroniki?
Taarifa ya ripoti ya BoT ya mwenendo wa mifumo ya malipo nchini 2024 inaonesha kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya miamala ya malipo inayofanyika kupitia huduma za pesa za simu mkononi.
Thamani ya fedha zilizotolewa kwa njia hiyo zimeongezeka kutoka shilingi trilioni 155 mwaka 2023 kufikiria trilioni 199 mwaka 2024. Hivyo unaweza kusema kwa mwenendo huu bila shaka miundombinu ya utoaji huduma hizo kama ATM zinaweza kutoweka katika kipindi kifupi kijacho.
Hata hivyo, matumizi ya ATM bado yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya utoaji huduma za kifedha, idadi ya mashine za ATM nazo pia zimeongezeka kutoka mashine 1981 kufikia 2174 kwa kipindi cha mwaka mmoja 2023/2024, na jumla ya Sh13.8trilioni zimetumwa au kupokewa kwa njia ya ATM kwa mwaka huo.
Mwenendo huu utaoa taswira moja kubwa, licha ya maendeleo ya huduma za fedha kielektroniki nchini, mfano huduma za malipo kwa simu, ATM pia bado ni sehemu muhimu katika miundombinu ya utoaji huduma hizo, sababu kadhaa zinachangia hali hiyo;
Kwanza, bado kuna kundi kubwa katika jamii linalotumia fedha taslimu kufanya malipo, licha ya huduma fedha kidijitali. Kwa mfano, biashara ndogondogo; wauzaji wa sokoni, migahawa, mamalishe, daladala, na wengineo. Matumizi ya fedha taslimu kwao ni njia kuu ya malipo.
Hata kwa mtu mwenye akaunti ya benki, au anayetaka kulipa kwa mtandao wa simu, kwenye maeneo hayo, atalazimika kutoa fedha ATM au kwa wakala kisha alipe taslimu mkononi bila hivyo anaweza kukosa huduma.
Pili, elimu ya matumizi ya huduma fedha kidijitali ndio inakuwa, hivyo si kila mtu ana uelewa wa kutosha kutumia huduma hizo. Kwa mfano inatokea katika mazingira yetu kwamba mtu ana kadi yake ya benki na angeweza kulipia kwa njia hiyo, lakini hajui, au haamini njia hiyo ya malipo, anaona bora kwanza aende ATM atoe fedha.
Tatu, ipo dhana kuwa wengine bado wanasita kutumia huduma fedha kimtandao kwa kuhofia ada au makato ya muamala ni makubwa, anaona bora atoe pesa zake kutoka ATM kisha ndio afanye malipo anayotaka kuliko angelipia kwa njia ya kadi au kibenki.
Nne, huduma fedha za kisasa zinatumika zaidi maeneo ya mijini ukilinganisha na vijijini, ambapo pia upatikanaji wa huduma za intaneti kufanikisha huduma fedha kimtandao wakati mwingine sio za uhakika. Hayo yote yanafanya miundombinu ya utoaji huduma fedha mfano mashine za ATM kama njia ya kupata fedha kukidhi mahitaji yao mbalimbali.
Hivyo, ninachojaribu kusema ni kuwa ni mapema kutoa kauli kwamba ATM hazina umuhimu tena. Ongezeko la idadi ya ATM na kuongezeka kwa miamala inayofanyika kupitia njia hiyo vinaonesha dhahiri kuwa bado ATM ni kama mzee wa busara anaendelea kuwepo ili kuwasaidia vijana wake ambao ni mifumo mipya ya utoaji huduma fedha, na ATM bado zina jukumu muhimu katika kukidhi mahitaji ya pesa taslimu kwa Watanzania.
Mfumo huo utaweza kuondoka au kuisha kabisa siku moja matumizi ya pesa taslimu yatakapofutika kabisa.
