Misime: Tuepuke kuongeza chumvi kwenye kidonda

Dodoma. Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, amewataka waandishi wa habari kutotoa taarifa zenye kuongeza maumivu kwa wananchi walioathiriwa na matukio, bali kuonyesha suluhu katika tukio husika.

Akizungumza leo, Novemba 27, 2025, katika mafunzo ya uandishi wa habari wa amani yaliyofanyika jijini Dodoma, Misime ameeleza kuwa waandishi wa habari wasitoe taarifa ili kuwavutia wasomaji, bali wangalie matokeo yake yatakuwaje.

“Wengi tumeumia kwa kupoteza ndugu zetu, kuharibiwa mali zetu, lakini kutokana na kilichotokea, ili kuweka usalama kwa wananchi, waandishi wa habari tuepuke kuongeza chumvi katika kidonda kwa sababu kunachochea na kuhatarisha amani. Pia, tuangalie matokeo baada ya kutoa taarifa hiyo,” amesema Misime.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk Dotto Bulendu, ameongeza kuhusiana na suala la uandishi wa habari jengefu, ambapo amesema kuwa uandishi unabadilika kutokana na misimu, lakini waandishi wa habari wanapaswa kuwa na uandishi unaojenga (Constructive Journalism).

“Uandishi wa habari jengefu unatafuta suluhisho la changamoto husika kwa ushahidi, haufichi uzito wa tatizo, lakini pia haufanyi mambo yaonekane mabaya. Kwa kuweka mzani sawa kati ya mazuri na mabaya, waandishi tutajenga jamii. Tusiruhusu kuweka petroli kwenye moto,” amesema Dk Bulendu.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Ofisa mawasiliano mwandamizi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Robin Aulikale, ameeleza kuhusu usalama wa kidigitali katika kuhakiki taarifa huku akiwaonya wananchi kuweka maisha yao mtandaoni, hasa picha za watoto, ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya mtoto sasa na baadaye.

“Ni muhimu kuhakiki taarifa kabla ya kuzitoa kutoka vyanzo vya kuaminika kama taasisi husika. Ni muhimu kulinda hadhi ya taaluma ya habari. Pia, msiweke maisha yenu mtandaoni kwa ajili ya usalama wa taarifa binafsi, hasa katika suala la kuweka picha za watoto mtandaoni, kwani ni hatari kwa mtu yoyote mwenye nia mbaya,” amesema Aulikale.