Mtanzania ashinda tuzo kubwa ya uhifadhi barani Afrika

Dar es Salaam. Mwanaharakati wa uhifadhi wa mazingira kutoka Tanzania, Rahima Njaidi, ametangazwa mshindi wa Tuzo ya Tusk ya Uhifadhi Barani Afrika, moja ya tuzo zinazoheshimika zaidi barani humo kwa kutambua uongozi wa kipekee na mchango mkubwa katika kulinda wanyamapori na mifumo ya ikolojia.

Rahima, ambaye kitaaluma ni mwanasheria na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa MisituTanzania (MJUMITA), amepokea tuzo hiyo usiku wa kuamkia leo katika hafla iliyofanyika  jijini London, Uingereza. Amekabidhiwa tuzo hiyo na mwanamfalme, William Charles.

Tuzo hizo hutambua wanaharakati wa uhifadhi barani Afrika ambao wameleta ubunifu na athari kubwa katika kulinda bayoanuwai katika bara zima.
Aidha, tuzo hiyo inawaenzi watu walioonyesha kujitolea kwa kiwango cha juu katika uhifadhi shirikishi unaoongozwa na jamii, usimamizi bunifu wa mazingira, na uendelevu wa muda mrefu.

Ametunukiwa kutokana na uongozi wake wa mabadiliko katika usimamizi wa misitu unaoongozwa na jamii, utetezi wake usiochoka kuhusu haki za ardhi na usawa wa kijinsia, pamoja na kazi yake ya ubunifu katika kulinda mustakabali wa misitu ya Tanzania kupitia uhifadhi shirikishi.

Kwa mafanikio haya, Rahima anakuwa mwanamke wa tatu barani Afrika kushinda Tuzo ya Tusk katika kipengele cha uhifadhi na Mtanzania wa kwanza kutunukiwa heshima hii.

Akizungumzia tuzo hiyo, amesema|: ‘’Hii tuzo inanifanya nijisikie mnyenyekevu na pia nimepata msukumo mkubwa. Inathibitisha jitihada za wenzangu na mimi, tukifanya kazi bila kuchoka kuhakikisha kwamba jamii ndizo kiini cha usimamizi na uhifadhi wa misitu.Tuzo hii iwe ukumbusho kwamba kuwekeza katika jamii ni kuwekeza katika uhifadhi, ustahimilivu, na tumaini. Mustakabali wa misitu yetu na sayari yetu unategemea hilo.’’

Rahima amesema hajui ni nani aliyemteua, lakini anaamini tuzo hiyo inaakisi juhudi za pamoja za Mjumita na jamii wanazoshirikiana nazo.

 Rahima Njaidi

“Kwa kweli, sijui ni nani aliyeniteua, lakini naamini tuzo hii inaonyesha athari ya kazi ambayo Mjumita inafanya na jamii. Ni heshima kubwa kwa shirika, kwa Tanzania, na kwa wanawake wanaojitolea maisha yao kwa uhifadhi,” amesema.

Ameongeza:“Kwangu, huu ni mshangao. Sikutarajia kwamba kuna watu wanaotambua jitihada zangu katika uhifadhi. Tuzo hii imenipa motisha ya kufanya kazi kwa bidii zaidi, lakini pia inawatia wananchi moyo wa kuendelea kuunga mkono juhudi za uhifadhi.”

Amebainisha kuwa sekta hiyo kwa muda mrefu imetawaliwa na wanaume, na kwamba tangu mwaka 2013, yeye ndiye mwanamke wa tatu kushinda tuzo katika kipengele hiki.

Tangu aanze uhifadhi mapema miaka ya 2000, amekuwa  akifanya kazi na kujenga hamasa ya kufanya kazi kwa karibu na jamii.

“Tuzo hii itasaidia Mjumita kupanuka hadi katika mikoa zaidi. Cha kutia faraja ni kwamba wanajamii wenyewe wana hamu ya kujiunga na Mjumita, lakini tunakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha na watu. Tunataka Tanzania yenye uoto wa kijani, ambako misitu inachangia ustawi wa wananchi,” amesema.

Ameeleza kuwa anatumai kuona maeneo zaidi ya misitu isiyosimamiwa yakiwekwa chini ya mfumo wa uhifadhi wa vijiji.

Alizaliwa Dodoma, Tanzania, na alipokuwa akikua alikuwa akisikia hadithi za babu yake zilizokemea ukataji miti, hadithi zilizomjengea heshima ya kina kwa mazingira na imani kuwa misitu ni maeneo matakatifu yanayopaswa kulindwa, siyo kutumiwa vibaya. Hadithi hizo ziliunda maadili yake, na kumjengea moyo wa kuheshimu mazingira na jamii zinazoyategemea.

Rahima alianzisha MJUMITA mwaka 2007, mtandao unaoongoza uhifadhi wa misitu kupitia jamii, ili kutoa sauti kwa jamii za vijijini katika kusimamia na kulinda rasilimali zao za asili.

Mjumita inafanya kazi katika mikoa kadhaa ikiwa na malengo ya kuimarisha usimamizi wa misitu unaoongozwa na jamii, kuhakikisha jamii zinanufaika kikamilifu na rasilimali za asili na kukuza elimu ya uhifadhi kwa vijana, wanawake na makundi maalum.

Wadau muhimu wanaoshirikiana na MJUMITA ni pamoja na vikundi vya uhifadhi wa misitu vya vijiji, mamlaka za serikali za mitaa, na mashirika kadhaa ya kimataifa ya mazingira yanayojihusisha na usimamizi endelevu wa ardhi na misitu.

Rahima amesema kuwa katika mkoa wa Pwani, hususan katika kijiji cha Nyamwage, wanatekeleza mradi unaolenga kujenga uwezo wa jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunawafundisha kuhusu utawala bora, miradi ya kiuchumi, na usimamizi wa misitu. Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kuwa watetezi wa misitu yao,” ameeleza.