…………………
Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetoa kibali maalum cha Mwaka mmoja kwa waliotumia nyaraka za kughushi pamoja na waliotoa taarifa za udanganyifu kufanya mabadiliko ya taarifa zao ili waweze kutambuliwa na kupata Vitambulisho.
Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa NIDA James Kaji wakati akizungumza na wanahabari ambapo amesema serikali imetoa kibali hicho ili kushughulikia maombi hayo ya kubadilisha taarifa ambayo awali hayakuweza kufanyika kutokana na kukinzana kwa miongozo inayosimamia mabadiliko ya taarifa.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa kibali hicho kimetolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Oktoba 2025 ambapo kitahusisha makundi manne likiwemo waathirika wa vyeti vya kughushi,waliofukuzwa katika ajira za serikali kwa kutumia vyeti vya shule vya kughushi ambapo walivitumia kujisajili NIDA
Aidha amewasisitiza wananchi kutambua kuwa maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale yatakayokidhi masharti na vigezo vilivyowekwa baada ya wahusika kuwasilisha nyaraka zinazotakiwa kuthibitisha taarifa zao.
Hata hivyo amesema NIDA inaendelea na utekelezaji wa jukumu la msingi la usajili na utambuzi wa watu pamoja na kutoa vitambulisho vya Taifa kwa rais,wageni,wakaazi,wakimbizi na walowezi waliokishi vigezo hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa sahihi na ukweli wanapokwenda kujisajili.