Shangwe, vilio washtakiwa 198 wakiachiwa huru Dar

Dar es Salaam. Shangwe, vilio vya furaha na huzuni vilitawala kwa muda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati washtakiwa 198 kati ya 216 wa kesi za uhaini, walipofutiwa mashtaka na kuachiwa huru.

Washtakiwa hao waliachiwa huru jana Jumanne, Novemba 25, 2025 baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuwasilisha taarifa mahakamani ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.

Hao wakiachiwa huru, wenzao 18 akiwamo mfanyabiashara maarufu wa vipodozi, Jennifer Jovin maarufu Niffer, wamesalia mahabusu DPP akiendelea na kesi dhidi yao.

Harakati za ndugu wa washtakiwa hao zilianza asubuhi walipokusanyika kwenye viwanja vya mahakama kwa makundi na kukaa katika banda maalumu wakisubiri kesi kuitwa mahakamani.

Mmoja wa waliofika mahakamani alionekana kubeba maua mkononi kwa ajili ya kumkabidhi mshtakiwa aliyesubiri kuachiwa kwake huru.

Mwingine alionekana akiwa amebeba maputo yenye ujumbe wa kumkaribisha nyumbani mume wake ukisomeka: “Welcome home my husband.”

Walisubiri hadi saa 8:30 mchana, kundi la kwanza la washtakiwa 116 walipofikishwa mahakamani hapo wakiwa kwenye mabasi mawili ya Jeshi la Magereza.

Kundi lingine la washtakiwa 99 lilifikishwa mahakamani saa 11:16 jioni. Walipofikishwa hapo, maofisa wa vyombo vya dola walichukua taarifa zao ikiwa ni pamoja na alama za vidole na kuwapiga picha.

Hayo yalifanyika kabla ya saa 12:20 jioni kesi zilipoanza kuitwa mbele ya mahakimu waliopangwa kuzisikiliza katika hatua ya uchunguzi wa awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za uhaini.

Washtakiwa 314 walifunguliwa mashtaka ya uhaini, katika makundi sita tofauti mahakamani hapo, wakidaiwa kujihusisha na matukio yaliyotokea kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 29, 2025.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, washtakiwa 20 waliachia huru ispokuwa Niffer na mwenzake, Mika Chavala.

Kwa uamuzi huo, mama yake Niffer aliangua kilio, akaanguka chini, hali iliyowalazimu waliokuwa naye kumpa msaada.

Mmoja kati ya walioachiwa huru aliishiwa nguvu akakaribia kuanguka akiwa kizimbani, kabla ya askari magareza kumdaka na kumkalisha chini.

Walipotoka ndani ya ukumbi wa mahakama ndugu, jamaa na marafiki walikumbatiana na wengine wakibebwa juujuu, huku wakishangiliwa.

Katika ya furaha, wapo walioangua vilio baada ya kuungana tena na ndugu zao waliopotezana kwa takribani mwezi mmoja.

Kundi la mwisho la washtakiwa liliachiwa huru saa 2:48 usiku.

Kutokana na ugeni wa mazingira ya mahakama, baadhi walihangaika kutafuta mlango wa kutoka nje ya viwanja vya mahakama, wengine wakifuata korido inayoelekea vyoo vya wanawake, hadi pale waliposhtuliwa na kuelekezwa lango la kutokea.

Joseph Martin (24), mkazi wa Kigamboni, ambaye ni mmoja kati ya walioachiwa huru amesema hakuwa kwenye maandamano.

Amesema licha ya kusoma katika moja ya vyuo vya kati, anajishughulisha na uingizaji muziki kwenye simu akitumia kompyuta yake mpakato.

Anasimulia Oktoba 29, alikwenda Kijitonyama kwenye shughuli hizo, ndipo  akashindwa kurudi nyumbani akalala kwa rafiki yake na kesho yake Oktoba 30 alikamatwa pamoja na wapangaji wa nyumba hiyo.

“Siku hiyo walipita askari, watu walipowaona wakaingia ndani, hivyo walikuja wakatutoa nje wakihoji kwa nini tunakimbilia ndani, wakatulazimisha tulale chini huku mwingine akisema atakayeinua kichwa piga risasi,” amesimulia na kuongeza:

“Wale watu japo walikuwa na sare za polisi lakini walikuwa wanaongea Kiswahili cha ajabu ajabu tu yaani Kiswahili chao hakikuwa kimenyooka.  Ndipo wakatufunga na kutuchukua wote kwenye gari lao.”

Jumla ya washtakiwa walioachiwa huru katika mahakama hiyo kuanzia Jumatatu Novemba 24, 2025 imefikia 245.