Sheria inavyovibana vicoba, vikundi vya kusaidiana

Vilio, kupoteza fedha, usiri uliokithiri ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa na bado yanaendelea kuvikabili baadhi ya vikundi vya huduma ndogo za kifedha ikiwamo vile vya kuweka akiba na mikopo (Vicoba).

Vikundi hivi mbali na kuwa msaada wa kuinua watu wengi kiuchumi lakini wakati mwingine viligeuka shubiri baada ya walioaminiwa kukimbia na fedha au kuzitumia wakiwa na imani ya kurejesha kabla ya wakati unaotakiwa jambo ambalo baadaye huibua tafrani kubwa.

Jambo hilo liliacha vilio kwa watu wengi, miongoni mwao ni kinamama wa kikundi cha ‘Tuinuane’ kutoka Goba ambao walijikuta njia panda baada ya mhasibu waliyekuwa wakimwamini kutumia akiba yao yote na kufanyia biashara ambayo haikuweza kuleta faida.

“Hatukuwahi kupata zile fedha, tumebaki kuwa watu wa kwenda serikali za mitaa na kurudi tukibebeshwa ahadi zisizokuwa na matumaini, hatuna kwa kumpeleka huyo mtu aliyekula hela zetu kwa sababu hatukuwa tumejisajili popote,” anasema Flaviana Mathayo mkazi wa Goba.

Akiwa amepoteza Sh3 milioni aliyokuwa amepanga kuitumia kama mtaji wa kuuza batiki kuanzia Septemba mwaka huu amebaki kuwa mama wa nyumbani huku ndoto zake zikiota mbawa.

“Nipo tu hapa, kheri ningeweka fedha hizi kwenye kibubu ndani kwangu, hivi sasa nimeanza upya nikiwa sina matumaini kabisa ni kama mtu niliyekuwa nimeanza kupiga hatua ghafla nimerudi kwenye kutambaa,” anasema.

Flaviana na wenzake 25 wanasotea zaidi ya Sh30 milioni ambazo walikuwa wakizitunza tangu Agosti mwaka jana na walitakiwa kugawana fedha hizo kipindi kama hicho mwaka huu.

Kilichokikuta kikundi hiki, ni mfano wa vikundi vingine ambavyo vimeanzishwa na kuendeshwa kinyume na taratibu vinavyoendelea mitaani jambo ambalo lilifanya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuamua kutafuta mwarobaini.

Ili kukabiliana na suala hilo BoT imekuwa ikivisajili vikundi hivi kupitia Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 hatua inayolenga kupunguza vilio, malalamiko na migogoro ya kifedha iliyokuwa ikiwakabili wanachama kwa miaka mingi.

Na ili kufanya sheria hiyo iwe na makali kwa watakaokiuka kufanya hivyo faini yake ni hadi Sh10 milioni na kifungo kinachoweza kufika hadi miaka mitano kulingana na aina ya kosa na kikundi kilichofanya kosa hilo.

Meneja wa Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha wa BoT, Dickson Gama anasema katika utekelezaji wa sheria hiyo hadi Septemba mwaka huu, jumla ya vikundi 70,900 Vikundi vya Huduma Ndogo za Fedha vya Kijamii vilikuwa vimesajiliwa na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (Saccos) 987.

Vikundi hivyo vimesajiliwa kupitia Wezesha Portal, mfumo wa kidijitali unaoratibiwa na Ofisi ya Tawala za Mikoa ana Serikali za Mitaa (Tamisemi).

“Miongoni mwa changamoto tulizokuwa tunakutana nazo ni Kukosekana kwa uwazi kwa viongozi wa Vicoba, kutotendewa haki wanachama, ukosefu wa takwimu kutoka sekta ya Huduma Ndogo za Fedha,” anasema.

Anasema kupitia usajili huo vikundi vimekuwa vikisaidiwa kutunza rejista, kukagua, kufuatilia na kutathmini utendaji kazi wa vikundi na kuhakikisha ulinzi wa wanachama wa vikundi.

Gama anasema ufuatiliaji wa mifumo ya huduma ndogo za fedha sasa umeleta matokeo halisi, ikiwamo kupungua kwa kesi za kuvunjiana vibubu, kutokulipa mikopo, utoaji wa mikopo kandamizi na kuwekwa rehani mali kubwa kama magari na nyumba kinyume cha utaratibu.

“Sheria inasema adhabu ya kuendesha shughuli hizi bila kusajiliwa faini yake ni hadi Sh10 milioni au kifungo kinachoweza kufika miaka mitano,” anasisitiza.

Akielezea namna kikundi cha huduma ndogo za kifedha kinavyoweza kuanzishwa anasema kinapaswa kuwa na idadi ya watu 10 hadi 50 walio na malengo yanayofanana, kuwapo na mkutano wa awali ili kuchagua kamati ya muda itakayowezesha uanzishwaji wa kikundi. “Pia lazima ufanyike mkutano wa uanzishaji wa kikundi utakaokuwa chini ya uongozi wa ofisa aliyeidhinishwa na Mamlaka Kasimishwa au mhamasishaji,” anasema Gama.

Ili kukisajilia amesema wahusika wanapaswa kuomba usajili kwa Benki Kuu au Mamlaka Kasimishwa ikienda sambamba na jina la kila kikundi kujumuisha neno “kikundi cha huduma ndogo za fedha cha kijamii.

“Benki Kuu au Mamlaka Kasimishwa kushughulikia maombi husika ndani ya siku 14. Benki Kuu au mamlaka kasimishwa inaweza kukataa kusajili kikundi cha huduma ndogo za fedha endapo kimeshindwa kukidhi masharti ya usajili,” anasema.

Kwa mujibu wake, usajili unahitaji katiba ya kikundi, orodha ya wanachama, maazimio ya kuanzisha kikundi na uthibitisho kutoka ofisi ya serikali ya mtaa.

“Uidhinishaji unaligeuza kundi kuwa taasisi ya kifedha iliyo halali, yenye haki na wajibu chini ya sheria za nchi,” anabainisha.

Hata hivyo, vikundi hivi vya kijamii vya kifedha kila kimoja huendeshwa kwa miiko yake kwani kuna vingine vilivyosajiliwa vinaweza kukusanya akiba, kutoa mikopo kwa wanachama na kuendesha shughuli za ustawi wa jamii lakini haviwezi kufungua matawi wala kupokea amana kutoka kwa wasiokuwa wanachama bila leseni.

“Hii inahakikisha kuwa shughuli za huduma ndogo za fedha zinabaki salama na zinazoendeshwa na jamii,” anasema.

Wakufunzi wafunguka umuhimu

Akizungumzia umuhimu wa uwepo wa vikundi hivi, Omary Yanga ambaye ni mwalimu na mwelimishaji elimu ya fedha kutoka Buta Vicoba Endelevu anasema mbali na kusaidiana katika shida na raha lakini husimama kama soko huria la kuuza bidhaa.

Anasema kupitia vikundi hivyo, watu wamekuwa wakiuziana bidhaa wanazozalisha hivyo mtu huwa na uhakika wa soko la uhakika kila kinapofanyika kikao.

“Lengo lao kubwa huwa ni kusaidiana katika shida na raha na imekuwa ni nyenzo muhimu kwani mtu anapopata tatizo wanashiriki kwa pamoja na kugeuka wafariji. Kwa vikundi vyenye ukomavu watu hutoa hadi Sh3 milioni hadi Sh5 milioni mtu anapofiwa,” anasema Yanga.

Fedha hiyo hutokana na akiba za wanachama zinazowekwa kila mwezi kulingana na kiwango walichokubaliana sambamba na viingilio kwa wanachama wapya.

“Kama jamii inakuwa karibu, wanasaidiana, wanajuana, wanatumia kikundi kama sehemu ya kuuziana bidhaa na kununua,” anasema.

Ili kuhakikisha hayo yanafanikiwa kama mwalimu amekuwa akihakikisha wote wanaopita mikononi mwake wanajisajili ili kuwa na uhakika wa usalama wa fedha zao.

Hili linafanyika wakati ambao baadhi ya watu mtaani wameendelea kulia kutokana na kuamini viongozi wao na kuwapa mamlaka ya kukusanya hela bila kusajiliwa.