Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, kutoka timu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Staff Sajenti Alphonce Simbu, ameondoka nchini leo asubuhi Novemba 27, 2025 kuelekea Ufaransa kwa ajili ya kushiriki sherehe za tuzo za wanariadha bora wa mwaka 2025 zinazoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Dunia.
Hafla hiyo itafanyika Novemba 30, 2025 jijini Monaco nchini Ufaransa, kwa kuwakutanisha wanariadha 12 walioteuliwa kushindania tuzo katika vipengele mbalimbali, Simbu akiwa ni miongoni mwao.
Nyota huyo wa mbio ndefu (marathoni), anawania tuzo ya mwanariadha bora wa mbio za nje ya uwanja kwa wanaume, akipambana kwenye hatua ya mwisho dhidi ya mpinzani wake aliyesalia, Sebastian Sawe wa Kenya, baada ya wawili hao kupenya mchujo mkali uliowahusisha makundi tofauti ya wanariadha duniani.
Katika hatua ya awali, kura zilipigwa na baraza la uongozi la riadha, wadau mbalimbali wa mchezo huo, pamoja na mashabiki waliopiga kura kupitia mitandao ya kijamii na baada ya mchujo, majina mawili ya mwisho kutoka kila kundi yalipelekwa kwenye upigaji kura wa kimataifa kupitia tovuti ya WA, huku kamati maalumu ikifanya tathmini ya mafanikio ya kila mwanariadha kabla ya kutangaza mshindi.
Tayari Simbu ameandika historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kufika hatua hii ya juu katika tuzo za dunia tangu Tanzania ilipoanza kuishiriki mashindano ya riadha ya dunia mwaka 1983. Endapo atashinda, atafungua ukurasa mpya na kuipa nchi heshima ambayo haijawahi kushuhudiwa kwenye medani ya riadha duniani.
Moja ya sababu zinazompa Simbu nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hii ni ukweli kwamba mashindano aliyoshinda msimu huu yanaratibiwa na kutambuliwa moja kwa moja na Shirikisho la Riadha la Dunia, jambo ambalo hupewa uzito mkubwa katika tathmini za tuzo.
Kwa upande wa mpinzani wake Sawe, mafanikio yake mwaka huu yametokana zaidi na ushindani katika mbio kubwa za Abbott World Marathon Majors, ambazo kwa heshima ni kubwa, lakini hazina uzito sawa na mashindano yanayotambuliwa moja kwa moja na WA, hii inampa Simbu faida ya kiufundi katika mchakato wa kumpata mshindi.
Simbu alitwaa ubingwa wa dunia katika mashindano yaliyofanyika Septemba 2025 jijini Tokyo nchini Japan, wakati Sawe yeye alishinda mbio mbili maarufu za London Marathon na Berlin Marathon.
Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kabla ya kuondoka, Simbu ameonyesha matumaini makubwa ya kufanya vizuri na kuandika historia mpya, huku akiwashukuru Watanzania na wadau wa michezo kwa kura zao.
“Ni mara ya kwanza kwa Mtanzania kuingia kwenye tuzo hizi, na kwangu pia ni mara ya kwanza, ninaamini mambo yanaweza kuwa mazuri,” amesema Simbu.
Aidha, ametumia jukwaa hilo kulitambua na kulishukuru JWTZ na Mkuu wa Majeshi, Generali Jacob Mkunda, kwa kuwawezesha wanariadha kupata mazingira mazuri ya mazoezi yaliyomsaidia kutwaa dhahabu na kufikia hatua ya fainali kwenye tuzo za dunia.